Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amebaini viashiria vya ubadhirifu wa fedha katika ujenzi wa mabweni ya Shule ya Sekondari ya Chala, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa unaogharimu Sh310 milioni huku akiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuanza uchunguzi.
Dk Mwigulu amehoji inakuaje mradi ambao bado haujaisha unapata nyufa na inakuwaje jengo la halmashauri vifaa vinunuliwe kwa mtumishi wa halmashauri hiyo.
Mtendaji mkuu huyo wa Serikali ameibua hayo leo Jumatatu, Machi 9, 2026 wakati akizungumza na wananchi wa Namanyele mkoani Rukwa ikiwa ni ziara yake ya kikazi mkoani hapo.
Amesema yapo majengo yaliyojengwa tangu wakati wa mkoloni hayana nyufa, inakuaje jengo ambalo ndilo limepakwa rangi na halijakauka tayari limepata nyufa.
“Hebu injinia wa wilaya tuambie…haya mambo ya uholela haya hayakubaliki, hatutamuonea mtu ngoja tufanye uchunguzi.
“Sasa mtumishi wa halmashauri ndiye anatuuzia vifaa vya kujenga jengo la halmashauri, kwa hiyo mnapanga bei ofisini mnaenda kununua nyumbani …tutaelewana tu,” amesema Mwigulu.
Mhandisi wa Wilaya ya Nkasi ambaye hakutaja jina lake, ameeleza sababu ya nyufa hiyo kuwa, “huwa inatokea baada ya muda majengo yakijengwa hutokea ‘settlement’ majengo yanasettle…”
Wakati mhandisi huyo akitoa maelezo Dk Mwigulu amesema: “Ukisikia kwenye maelezo yakiwekwa Kiingereza ujue hapo unaibiwa mambo ya settlement, adjustment.”
Mhandisi huyo ameendelea kujibu akisema:“Kunapotokea mitikisiko kwenye jengo lazima kuweko kwa nyufa hasa katika maeneo dhaifu ikiwamo maeneo ya dirisha na yenye uwazi.”
Baada ya maelezo hayo, Waziri Mkuu alimuita Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nkasi, Alfraha Hassan kueleza sababu ya nyufa hizo, akieleza asilimia kubwa ya ardhi wilayani hapo ina miamba.
Baada ya swali hilo, Dk Mwigulu alimhoji mkurugenzi huyo kama anafahamu sababu ya vifaa vya shule ya amali ya wavulana bei kuwa juu kuliko bei ya soko.
Amehoji pia, kama anafahamu vifaa wanavyonunua wanakwenda kwenye duka la mtumishi wa halmashauri.
Kutokana na maswali hayo kukosa majibu hapo hapo, Dk Mwigulu amesema ana taarifa zote, hivyo alimuagiza Kamanda wa Takukuru mkoani Rukwa kuchunguza majengo yote na vifaa kulinganisha na bei ya maduka mengine.
“Kafuatilie unipe taarifa, wakati namalizia ziara ya Mkoa wa Katavi niweze kufanya uamuzi. Mnapewa fedha, fedha zinaisha majengo hayajaisha, mmepandisha bei.
“Mmeazima vifaa kutoka mradi mwingine kwa utaratibu gani, haya mambo haya ya uholela nilisema sitamuonea mtu ngoja tupate taarifa ya uchunguzi,” amesema.
Akizungumzia tatizo la maji, Dk Mwigulu amesema miaka ya nyuma Wilaya ya Nkasi ikitaka kuchimba kisima ililazimika kusubiri mtambo uliopo Wilaya ya Namtumbo.
“Rais Samia amenunua mitambo kila mkoa na sasa kila mkoa una mtambo wake wa kuchimba maji na kila kanda ina mtambo wake wa kuchimba mabwawa.
“Kwa hiyo, nitoe maelekezo kwa mikoa na wilaya twendeni tukatumie mitambo hiyo kuwapatia wananchi maji, mama ameshatuletea mitambo twendeni ‘site’ tuwapatie wananchi maji,” amesema.
Waziri Mkuu amesema anasisitiza hilo kwa sababu anajua mambo ya nchi, wapo watu hawataki kuchimba maji kwa mitambo wanataka kutoa zabuni.
Amesema ndani ya zabuni hizo huwa kuna asilimia, ndiyo maana watu hupelekewa mitambo na kupaki.
Kutokana na hayo, ameelekeza kusiwe na mitambo itakayoachwa bila kazi badala yake zitumike kuchimba maji na baada ya miezi sita ya bajeti hataki kusikia shule au zahanati haina maji.
“Maeneo ambayo hatuwezi kuchimba maji, mitambo ya kujenga mabwawa ipo na Mungu anatupatia maji yanatapakaa, hii habari ya watoto kutembea na ndoo viunoni iishe,” amesema.
Dk Mwigulu amesema baada ya maeneo aliyopita amegundua bado watumishi wamesinzia, kulemaa, kuishi kwa mazoea na kufanya udokozi jambo ambalo halikubaliki.
Amesema hakutakuwa na mzaha wala kuvumilia uzembe, wizi, ubinafsi, ufisadi na uvivu ndani ya uongozi wa awamu ya sita.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Bazilio Mbwilo ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na vituo vitatu vya afya.
Pamoja na hayo, Mbunge huyo ametaja kata za Paramawe, Ntenga na Mashebe kukosa vituo vya afya akikumbusha ahadi ya Rais Samia ya kutaka huduma kumfuata mwananchi badala ya wananchi kufuata huduma.
Ametaja Kata ya Mkwamba ambayo ni kilomita 70 kutoka ilipo Hospitali ya Wilaya akisisitiza kutokana na ubovu wa barabara ni muhimu Serikali ikajenga kituo cha afya.
Kuhusu maji, amesema Namanyere inasumbuliwa na shida hiyo, kutokana na mabwawa kukauka akiomba chanzo cha maji kutoka Ziwa Tanganyika.
Akijibu baadhi ya changamoto, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Reuben Kwagilwa amesema Tamisemi ina mpango wa kujenga vituo vyote vya afya vilivyotajwa na mbunge huyo.