Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kufuatia kuendelea kwa ongezeko la mafua makali na Uviko19, ikitahadharisha kuwa hali hiyo itaendelea hadi kipindi cha Aprili na Mei, 2026.
Februari 25, 2026, Wizara ilitangaza rasmi kuwepo kwa mlipuko huo, ikiwataka wananchi kuchukua hatua za kinga ili kudhibiti maambukizi.
Mpaka leo Jumatatu, Machi 9, 2026 bado kumeendelea na ongezeko la watu kupata mafua na magonjwa mengine yanayohusiana na njia ya hewa kama homa, kukohoa, na kuhisi baridi.
Hata hivyo, kuna maeneo ya jiji la Dar es Salaam, baadhi ya watu wamesema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wanaopata ugonjwa mkali, kuumwa na kichwa na wengine wakilazimika kupata usaidizi wa kupumua.
“Wiki iliyopita kuna mtu wa karibu yangu aliumwa sana na kubanwa na kifua hali iliyolazimu madaktari wamuwekee mashine ya kupumulia, si huyo pekee kuna wagonjwa wengine wawili waliopita hali hiyo ninawafahamu,” amesema Lahel Anthony mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi leo, Jumatatu Machi 9, 2025 Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema licha ya mlipuko huo, hadi sasa hakuna taarifa za wagonjwa waliolazwa.
“Sina taarifa za watu kulazwa wakiwa kwenye oksijeni kwa Uviko19, maana kuwekwa kwenye oksijen sababu zinaweza kuwa nyingi,” amesema.
Dk Magembe amesema msimu wa mafua utaendelea hadi Aprili na Mei kama ilivyo miaka yote kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa na kwamba hakuna mabadiliko.
“Tangu tutoe tahadhari hakuna mabadiliko, watu wanaugua mafua na kupona kila siku kulingana na hali ya hewa ya kipindi husika,” amesema.
Alipotafutwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Mohamed Mang’una, amesema mpaka sasa hakuna hospitali yoyote yenye wagonjwa wanaopewa oksijen kwa ajili ya uviko 19.
“Wagonjwa waliopo ni wale wanaopata ugonjwa usiokuwa mkali, wanahudhuria hospitalini, wanapewa matibabu na kurudi nyumbani. Mkoa wa Dar es Salaam hatujapata mgonjwa wa kulaza,” amesema Dk Mang’una.
Kwa upande wa tahadhari na elimu kwa umma amesema, “Elimu inatolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari (redio, televisheni) na vipindi vya uelimishaji vituoni vinafanyika.”
Awali, Dk Magembe alisema kuwa magonjwa hayo huenezwa kupitia majimaji yanayotoka kwenye njia ya hewa ya mgonjwa wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza na pia kwa kugusa maeneo yaliyochafuliwa.
Alizitaja dalili zake ni pamoja na homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo na uchovu.
“Wizara inazitaka jamii kufunika pua na mdomo wanapokohoa au kupiga chafya, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, kuepuka misongamano isiyo ya lazima, kuvaa barakoa wanapokuwa na dalili au wakiwa kwenye maeneo yenye msongamano, pamoja na kuzingatia usafi binafsi na wa mazingira,” alielekeza.
Aidha, wananchi wametakiwa kuwahi vituo vya afya kupata matibabu na kuepuka kutumia antibiotiki bila ushauri wa wataalamu.