Yanga ilivyomchomoa kocha Uingereza | Mwanaspoti

KATIKA mpango wa kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana, Yanga imeonyesha kuwa siriazi na jambo lake baada ya kumchomoa Kocha Mohamed Badru huko Uingereza ambako alikuwa akiinoa May & Baker F.C.

Badru atakuwa kocha mkuu wa mradi wa Yanga Soccer School, uliozinduliwa Novemba 15, 2025, ukilenga kutafuta wachezaji wenye vipaji kati ya umri wa miaka 15 hadi 17 na kuviendeleza.

Uamuzi wa Yanga kumleta Badru umetokana na rekodi yake katika soka la vijana. Mbali na kuzinoa klabu za Ligi Kuu Bara, Mtibwa Sugar na Gwambina kwa vipindi tofauti, kocha huyo alijizolea umaarufu kufuatia kuiongoza Azam U17 msimu wa 2023-2024 na kutwaa ubingwa wa Ligi ya Vijana ikiwa hajapoteza mchezo wowote. Huo ulikuwa ubingwa wa tatu mfululizo.

Moja ya matokeo ya mradi ambao alipewa huko Chamazi ni Cyprian Kachwele, ambaye sasa anaichezea Vancouver Whitecaps ya Canada. Pia, Mohamed Shilla ambaye wiki chache zilizopita alijiunga na Allsvenskan ya Sweden.

Akizungumzia uamuzi wa kumrejesha nchini kocha huyo ambaye alitua Jumamosi iliyopita usiku na juzi Jumapili kuanza kazi ya kutafuta vipaji, Rais wa Yanga, Hersi Said, alisema: “Tunajua namna ambavyo amebobea kwenye soka la vijana, tunaamini atakuwa msaada katika kusimamia maono yetu.”

Hersi alieleza wazi Badru ndiye chaguo la kwanza kwa ajili ya kuongoza mradi huku pia akiongelea mchakato mzima ulivyo na kwa sasa upo katika hatua ya kusaka vipaji kabla ya kuendelezwa.

Aidha, rais huyo alifafanua kuwa wachezaji watakaochaguliwa kati ya 630 ambao walijisajili watapata muda wa kutazamwa kwa karibu, ndani ya mwezi mmoja ili kupata idadi ya wachezaji ambao wataendelea nao katika mradi huo.

“Inawezekana kupata watoto 100 halafu tutaendelea kuwachuchuja kwa ukaribu, mwanzo tulikuwa na changamoto za kifedha, unajua kulea na kuendeleza vipaji ni gharama sana lakini kwa sasa tumekaa sawa kwa sababu ya mdhamini, huyu mtoto ambaye atapatikana, atakuwa chini ya Yanga na taasisi ambayo tumeingia nayo mkataba,” alisema.

Akizungumzia majukumu yake mapya ndani ya Yanga, Badru alisema: “Hakuna kitu ambacho nimekuwa nikifurahia zaidi katika soka kuliko kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana na ndiyo sababu sikuwa na tabu kuacha kila kitu Uingereza na kuamua kurejea nyumbani kwa ajili ya kazi hii maalum.”

Aliongeza mradi wa Yanga Soccer School ni fursa kwa vijana wenye ndoto za soka na anaona wajibu wake ni kuhakikisha kila mchezaji anapata mwongozo na msingi bora ya kuwa mchezaji wa kulipwa.