ACT – Wazalendo yafikisha kilio cha demokrasia UN

Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, ameeleza wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa kisiasa uliojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 29, mwaka jana.

Katika mazungumzo hayo na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika, Parfait Onanga-Anyanga, yaliyofanyika leo Jumanne Machi 10, 2026 jijini Dar es Salaam, Semu amesema hali ya kisiasa nchini kwa sasa si ya kuridhisha.

Amedai kumekuwa na ukandamizaji wa demokrasia, uminyaji wa haki na uhuru wa vyombo vya habari.

“Kumekuwa na wizi wa kura, kukanyagwa kwa haki za kisiasa, vitisho na matumizi ya nguvu dhidi ya wananchi wanaodai haki zao za kidemokrasia. Haya yameendelea kutawala nchini,” amedai Semu katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa chama hicho, Mwanaisha Mndeme.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye ofisi za ubalozi wa UN jijini Dar es Salaam, Semu pia alirejea msimamo wa chama chake wa kutoitambua Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani ya Oktoba 29, 2025 iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Mapendekezo ya chama ni kuundwa kwa chombo huru na cha kimataifa kinachoaminika ili kufanya uchunguzi wa kweli wa vitendo hivyo na kuchukuliwa hatua dhidi ya waliohusika,” amesema.

Semu pia ameomba UN kulipa uzito suala hilo na kuweka msukumo utakaosaidia utekelezaji wake ili kufikia uwajibikaji na kurejesha amani na utengamano wa Watanzania.

Aidha, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufuatilia kwa karibu hali ya kisiasa na kidemokrasia nchini Tanzania na kusaidia juhudi za kuhakikisha haki, uwajibikaji na utawala wa sheria vinazingatiwa.

“Ili kujenga misingi ya kweli ya demokrasia, suluhisho la kudumu la changamoto za kisiasa nchini linahitaji mageuzi ya msingi ya kisiasa na kikatiba, hususan kuharakishwa kwa mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya na kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi,” amesema.

Kwa upande wake, Onanga-Anyanga amesema nia ya Katibu Mkuu wa UN ni kuona nchi zinakuwa na mifumo ya kuzuia na kudhibiti migogoro ili kudumisha amani.

Amesema pia ni muhimu wadau wa demokrasia kutumia yaliyotokea Oktoba 29, 2025 kama funzo la kuboresha misingi ya demokrasia na haki ili kuhakikisha matakwa ya wananchi yanaheshimiwa na mamlaka zinaongoza nchi kwa kuzingatia Katiba.

Katika ziara yake nchini, Onanga-Anyanga anatarajiwa pia kukutana na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Viongozi wengine anaotarajiwa kukutana nao ni Spika wa Bunge, Mussa Zungu, Jaji Mkuu, George Masaju na Rais Samia Suluhu Hassan.