Arusha. Mkoa wa Arusha umepitisha rasimu ya mapendekezo ya mpango wa bajeti ya Sh503.595 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwa ni ongezeko Sh9.88 bilioni kutoka bajeti ya mwaka uliopita 2025/2026 iliyokuwa Sh493.71 bilioni.
Aidha, katika bajeti hiyo, Sekretarieti ya Mkoa wa Arusha imepangiwa Sh14.72 bilioniĀ huku Sh488. 867 bilioni zikielekezwa kwa Mamlaka za serikali za mitaa.
Akiwasilisha taarifa hiyo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Maendeleo ya Mkoa (RCC), katibu tawala msaidizi mipango na uratibu Mkoa wa Arusha, Apolinary Seiya amesema fedha hizo zitatumika katika matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Tukiidhinishiwa fedha hizi, tunatarajia kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya huduma za kijamii, miradi ya kiuchumi pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi katika halmashauri zote za mkoa wa Arusha.”
Amesema kati ya fedha hizo Sh371 bilioni, sawa na asilimia 73.8 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, huku Sh132 bilioni sawa na asilimia 26.2 zikielekezwa katika miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla amesema kuwa wataifikisha rasimu hiyo kwa ofisi ya Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) kwa ajili ya kuidhinishiwa kiasi hicho cha fedha.
“Bila kuongeza uwezo wa mapato kero zitazidi na uwezo wa kutimiza malengo ya Rais wetu kuwapa wananchi tabasamu litakuwa gumu,” amesema.
Pia, Makalla amewataka watendaji wa halmashauri kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 katika maeneo yao yanatolewa kwa haki, usawa na uwazi ili kupunguza manung’uniko na malalamiko kwa wanaostahili kunufaika.
Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, amesema atahakikisha miradi yote ya maendeleo inatekelezwa ipasavyo ili kuondoa malalamiko ya wananchi.
“Mimi ni Mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Arusha, nitahakikisha bajeti hii inatekelezwa kwa vitendo ili kuleta maendeleo kwa wananchi wetu,” amesema Makonda, ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas ole Sabaya, amewataka watendaji kuhakikisha mipango ya mkoa inatekelezwa ili kuondoa kero za wananchi kutokana na viongozi wakubwa wanaotembelea mkoa huo.
“Ni aibu anakuja Waziri Mkuu hapa unakaa kwa wasiwasi kuwa wananchi watatoa kero zipi wakati nyingi ziko ndani ya uwezo wenu.
“Tunaomba utekelezaji uende kwa kasi ya mabadiliko ya kadri ya mipango ya utekelezaji mliyojiwekea na sisi kama chama tuko tayari kwa ushirikiano,” amesema.