Musoma. Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila amelaani tukio la Jeshi la Polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanachama, wafuasi na viongozi Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) katika eneo la Kanisa Kuu la jimbo hilo mjini Musoma, akisema kitendo hicho kinazidisha chuki kwa jeshi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Jumanne Machi 10, 2026, Askofu Msonganzila amesema Jeshi la Polisi lilipaswa kutumia busara na hekima badala ya kutumia nguvu kuwatawanya watu hao, ambao hawakuwa na aina yoyote ya silaha.
Ameeleza kuwa kitendo hicho hakikuwaathiri walengwa hao pekee, bali kiliathiri jumuiya nzima ya waumini wa kanisa hilo ambao walikuwa wakiingia kwenye ibada kwa misa iliyokuwa inafuata, sambamba na wale waliokuwa wakitoka kwenye misa iliyokuwa imeisha wakati huo.
“Walioathirika si wanawake wa Chadema pekee, bali waumini wetu, watoto na wazee. Waliathirika na yale mabomu ambayo nasema yalitumika bila sababu yoyote, kwani wale wanawake hawakuwa na aina yoyote ya silaha na ningekuwa polisi, wale wanawake ningewachapa na kanga na vitenge badala ya kutumia nguvu nyingi,” amesema.
Mapema, Polisi Mkoa wa Mara walipiga marufuku kongamano la Bawacha la maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani lililopangwa kufanyika kitaifa mkoani humo Machi 8, 2026.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo alisema sababu ya zuio hilo ni kuwa chama hicho kinakiuka kwa amri ya Mahakama ya Juni 10, 2025, inayokizuia kufanya masuala ya kisiasa.
Alisisitiza lengo la Polisi ni kuhakikisha amri hiyo ya mahakama inaheshimiwa. Katika tukiuo hilo wanawake 27 waliripotiwa kutiwa mbaroni.
Hata hivyo, wanawake walijikusanya mkoani humo na kufanya jumuiko lao kanisani hapo, huku wengine mamia wakizuiwa katika mikoa mbalimbali.
Kufuyatia tukio hilo, Askofu Msonganzila amesema Jeshi la Polisi linahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa ili kurejesha imani kwa wananchi na kwamba muda wa kufanya hivyo bado.
Amesema kitendo kilichofanywa na jeshi hilo kinazidi kutonesha majeraha ya Watanzania yaliyotokana na matukio ya Oktoba 29, 2025.
Amesema katika mazingira kama hayo, polisi walitakiwa kutumia busara na hekima badala ya kupiga mabomu katika eneo la kanisa kwa kuwa kanisa lina mchango mkubwa katika ujenzi wa nchi, ikiwepo suala la amani na utulivu.
“Polisi wanatakiwa kutumia amani katika kulinda amani, polisi wanapotumia mabavu wanajenga uadui na jamii na hiyo ina hatari kubwa, kwani wanajiwekea wigo mkubwa wa maadui kutoka ndani na nje, ambao watatumia fursa hiyo ya uadui kati ya polisi na jamii kufanikisha malengo yao,” amesema na kuongeza:
“Tunazuiliwa kuongelea ya Oktoba 29, lakini ukweli ni kuwa majeraha ni makubwa sana, wengi wamejeruhiwa kwa maana ya kwamba jamii, polisi na makundi mengine, polisi wasiendelee kutonesha majereha, narudia tena, tutumie amani kujenga amani.”
Amesema kitendo kilichofanyika katika maeneo ya ibada si utu wala ubinadamu bali ni ukatili na unyanyasaji.
Amesema Polisi wanapaswa kutambua mchango wa dini katika malezi ya jamii hususan katika suala zima la Amani, hivyo vitendo vya aina hiyo havitakiwi kuendelea kutokea nchini.
Kuhusu siasa na dini, Askofu Msongazila amesema kanisa hilo halifungamani na upande wowote wa siasa nchini, isipokuwa lina waumini ambao ni wana siasa wa vyama mbalimbali nchini.
Amesema kanisa hilo pia haliruhusu kikundi chochote cha wanasiasa kuingia kanisani kikiwa kimevaa sare za chama cha siasa, akieleza kuwa siku ya tukio wajumbe wa Bawacha kabla ya kuingia ndani ya kanisa wakiwa wamevaa sare zao, waliingia katika eneo la kanisa wakiwa wamevaa nguo za kawaida.
“Waliingia katika mazingira ya kanisani wakiwa wamevaa kawaida lakini baadaye wakavaa hizo nguo zao na kuingia nazo ndani ya kanisa na hata wakati wa ibada, aliyekuwa anaendesha ibada siku hiyo hakuwatambua kwani alidhani ni moja ya vikundi vyetu vya kitume ndani ya kanisa,” amesema.
Amesema baada ya ibada kwisha na wajumbe hao kutoka nje ya kanisa, walianza kufanya mahojiano na waandishi wa habari katika viwanja vya kanisa, kabla paroko kuwazuia kufanya hivyo, kwa kuwa hilo lilikuwa kinyume na taratibu za kanisa ambalo haliruhusu mambo ya kisiasa kufanyika kanisani au katika maeneo ya kanisa.
Kuhusu kuruhusu Bawacha kutumia viwanja vya Matumaini kwa vijana kwa ajili ya kongamano lao, Askofu Msonganzila amesema waliruhusu uwanja huo kutumika kwa vile hawakujua kama kuna katazo la Serikali kuhusu kongamano hilo.
“Vile viwanja vinatumika kwa shughuli mbalimbali za kijamii, kidini, michezo na mambo mengine kwa hiyo walipokuja sisi tukawaruhusu lakini baada ya kufahamu kuhusu hilo katazo, nasi tukawazuia kwani tusingependa kuingia knweye mgogoro na upande wowote,” ameeleza.
Baadhi ya wakazi wa mji wa Musoma wamesema inahitajika busara na hekima ili kuendelea kuleta umoja na mshikamano katika jamii.
“Naungana na Askofu, pale polisi walitumia nguvu nyingi, walitakiwa kuongozwa na busara na hekima badala ya kupiga mabomu, walitakiwa kuangalia namna nzuri ya kumaliza jambo hilo,” amesema Upendo Joel, mkazi wa Musoma.
Kwa upande wake, Hamisi Malima amesema polisi na vyombo vingine vya dola vinatakiwa kuona namna nzuri ya kurejesha amani umoja na mshikamano wa kitaifa, kuliko kutumia mabavu na Bawacha walitakiwa kuruhusiwa kuendelea na maadhimisho yao.
“Wangewaruhusu wakaendelea na kama kungekuwa na matamshi au vitendo vibaya ndipo wangechukua hatua, hawa wanawake wameonewa na hii inazidi kuleta mpasuko katika jamii,” amesema.