Dkt. Mwigulu Aagiza Takukuru Kuchunguza Ujenzi Wa Hospitali Ya Wilaya Ya Kalambo

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa kina kuhusu makadirio na matumizi ya fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa.

Ametoa agizo hilo leo Jumanne (Machi 10, 2026) wakati akizungumza na wananchi wa Kasanga, Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo, ambapo baadhi ya majengo bado hayajakamilika licha ya fedha kutolewa na Serikali.

Serikali ilitoa zaidi ya Sh. bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kalambo ambapo katika awamu ya kwanza majengo saba ya huduma za afya yalijengwa, ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la mama na mtoto, maabara, duka la dawa pamoja na miundombinu mingine ya huduma za hospitali. Hata hivyo, licha ya fedha hizo kutolewa na baadhi ya majengo kukamilika, majengo mawili muhimu ambayo ni jengo la theatre (chumba cha upasuaji) na wodi ya wanaume hayajakamilika.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu ameonesha kutoridhishwa na taarifa ya kuchelewa kukamilika kwa baadhi ya majengo ya hospitali hiyo.

“Ninyi mmeomba fedha, hamjapunguziwa hata senti moja ya fedha mlizoomba, mmepewa. Halafu mnapofika kwenye utekelezaji mnasema fedha haitoshi. Hii si sawa,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, Dkt. Mwigulu amemtaka Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Rukwa Bw. Mzalendo Widege kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama kulikuwa na uzembe au udanganyifu katika makadirio na matumizi ya fedha za ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo.

“Kamanda wa TAKUKURU nenda kachunguze, angalia kama kweli makadirio yalikuwa sahihi au kuna jambo lingine limejificha. Nipate taarifa ili tuweze kuchukua hatua stahiki,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali haitavumilia uzembe, ubadhirifu au ukiukwaji wa maadili katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuwa fedha zinazotolewa ni mali ya umma na zinapaswa kutumika kwa manufaa ya wananchi.