Imani za kishirikina zatishia wananchi kudai haki zao Tanga

Tanga. Baadhi ya wananchi jijini Tanga wameeleza hofu ya imani za kishirikina, imekuwa kikwazo kwao kudai haki zao katika migogoro mbalimbali inayowakabili ikiwemo masuala ya ardhi.

Mara kadhaa wananchi wamekuwa wakisikiliza malalamiko ya wenzao, lakini wengi hushindwa kuchukua hatua kwa hofu ya madhara yanayodaiwa kuhusishwa na ushirikina.

Malalamiko haya yamejitokeza katika kliniki ya sheria inayosimamiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayoendelea katika viwanja wa Tangamano jijini humo, ambayo imezinduliwa Machi 9, 2026 na inatarajiwa kufikia tamati Machi 15, 2026.

Wakizungumza na Mwananchi Machi 10, 2026, baadhi ya wakazi wamesema kuna wakati wanashindwa kudai haki zao kwa hofu ya kufanyiwa vitendo vya kishirikina.

Mkazi wa Handeni, Mohamed Shafii, amesema mara kadhaa wananchi wamekuwa wakisikiliza malalamiko ya wenzao, lakini wengi hushindwa kuchukua hatua kwa hofu ya madhara yanayodaiwa kuhusishwa na ushirikina.

Wakazi wa jiji la Tanga wakiwa wanasikilizwa na mawakili wa Serikali na binafsi katika kliniki ya sheria inayoendelea katika viwanja wa Tangamano jijini humo.



“Watu wengi wanaogopa kudai haki zao kwa sababu wanaamini wanaweza kufanyiwa mambo mabaya ya kishirikina na ikiwepo vifo vya utata,” amesema Shafii.

Amesema hali hiyo imefanya baadhi ya watu kubaki kimya hata wanapohisi kunyimwa haki zao, wakihofia madhara yanayoweza kuwapata wao au familia zao.

Kwa mujibu wa mkazi huyo, wakati mwingine watu hujaribu kuwashauri wenzao wachukue hatua au kufuatilia haki zao kupitia viongozi au vyombo husika, lakini hofu bado kubwa.

“Unaweza kumwambia mtu aende kudai haki yake, lakini anakwambia anaogopa kwa sababu kuna mambo yanafanyika ambayo hayafahamiki wazi,” amesema.

Hali hiyo, wanasema inarudisha nyuma jitihada za kujenga jamii yenye uwazi na haki, kwani baadhi ya watu hushindwa kushiriki kikamilifu katika mijadala au uamuzi wa jamii.

Aidha, amesema ni muhimu jamii kuendelea kuelimishwa ili kuondoa hofu zinazotokana na imani hizo na kuwahamasisha wananchi kutumia njia rasmi za kutatua migogoro na kudai haki zao.

“Bila kuondoa hofu hiyo, baadhi ya watu wataendelea kuonewa au kunyimwa haki zao huku wakikosa ujasiri wa kuzungumza hadharani,” amesema Shafii.

Mkazi wa Amboni, Mwanahawa Salim, amesema migogoro ya ardhi katika eneo lao mara nyingi huishia kusameheana ili kuepuka kurogwa na hatimaye kukumbwa na maradhi ya ghafla.

Amesema katika jamii yao baadhi ya watu huamini kuendelea kushikilia migogoro ya ardhi kunaweza kuleta madhara yasiyoelezeka.

Wananchi wa Amboni, jijini Tanga wakiwa wanasikilizwa na Wakili wa Serikali katika kliniki ya sheria inayoendelea katika viwanja vya Tangamano kuhusu mgogoro wa ardhi wa eneo lao



“Baba yetu alikuwa anagombania shamba na dada yake, siku moja ghafla alianza kupiga kelele akisema anatishiwa kuuliwa kwa sababu ya shamba mpaka anafariki alikuwa akimtaja ndugu yake,” amesema Mwanahawa.

Kwa mujibu wa Mwanahawa, tuhuma zimekuwa zikielekezwa kwa baadhi ya viongozi wa vijiji kuwa wanahusika katika migogoro ya ardhi kwa kushirikiana na watu wengine kuchukua mali za wananchi.

“Viongozi wanaotuhumiwa mara nyingi ni mwenyekiti wa kitongoji na kijiji, wananchi wanapowauliza kuhusu migogoro hiyo, wakati mwingine huwa wakali na kutafuta sababu za kuwatoa watu kwenye vijiji au kuwabambikiza kesi,” amesema.

Amesema kutokana na matukio kama hayo, baadhi ya wananchi wamekuwa wakiamua kusamehe au kuachana na madai yao ili kuepuka hofu.

Hivyo, misafara ya viongozi wakubwa inawasaidia kutoa kero bila woga kwa sababu ya ulinzi wanaokuwa nao wakati wa ufuatiliaji wa migogoro yao na viongozi wa vijiji na familia kwa ujumla.

Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu Kliniki ya Sheria, Ipyana Mlilo amewataka wananchi kuondoa hofu ya vitisho wanapodai haki zao migogoro inayowasilishwa katika vyombo husika itaendelea kushughulikiwa hata kama wananchi watahisi kutishwa.

“Tuwaondoe wasiwasi wananchi wa Tanga kuhusu vitisho, kila jambo lao litaendelea kushughulikiwa na kamati za ushauri wa kisheria za wilaya na mkoa, wananchi wanapaswa kuwafikia viongozi na taasisi husika ili kupata msaada wa kisheria,” amesema Mlilo.

Amesema wananchi wanapaswa kutumia njia rasmi za kisheria katika kutatua migogoro yao badala ya kukata tamaa kutokana na hofu ya vitisho au imani zinazoweza kuwazuia kudai haki zao.