Mvutano kati ya Iran na Marekani umeongezeka baada ya viongozi wa Iran kutoa onyo kali kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, wakimtaka kuwa makini kufuatia kauli zake dhidi ya uongozi mpya wa nchi hiyo.
Onyo hilo lilitolewa na Mkuu wa usalama wa Iran, Ali Larijani, ambaye alijibu matamshi ya Trump kwa kusema Iran haiogopi vitisho vya Marekani.
“Iran haiogopi vitisho vyako visivyo na maana. Hata wale waliokuwa na nguvu kuliko wewe hawakuweza kuiondoa taifa la Iran. Jitunze usije ukaondolewa,” alisema Larijani.
Kauli hiyo ilikuja baada ya Trump kusema haamini kuwa Kiongozi Mkuu mpya wa Iran, Mojtaba Khamenei, ataweza kuishi kwa amani, akionyesha kutoridhishwa na uteuzi wake. Trump pia alionya Iran kuwa itakabiliwa na kipigo kizito endapo itaendelea kufunga njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta ya kimataifa, Strait of Hormuz.

Rais huyo alitoa kauli hizo katika mahojiano na Fox News, akisisitiza kuwa Marekani haitaruhusu Iran kudhibiti kwa nguvu njia hiyo muhimu ya bahari inayotumika kusafirisha sehemu kubwa ya mafuta duniani.
Wakati huo huo, mvutano umeongezeka zaidi baada ya taarifa kuibuka kuwa mtu aliyefundishwa na kikosi cha Iran cha Islamic Revolutionary Guard Corps alipatikana na hatia kwa kupanga jaribio la kumuua Trump wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2024.
Mtu huyo, Asif Merchant, raia wa Pakistan, alihukumiwa baada ya mahakama kubaini kuwa alikuwa sehemu ya mpango wa kumuua Trump ndani ya Marekani.
Kwa mujibu wa maafisa wa usalama wa taifa wa Marekani, timu kadhaa za watu waliotumwa na Iran zilikuwa zikiendelea kufanya ufuatiliaji wa Trump wakati wa kampeni zake za uchaguzi.

Mambo Mengine Muhimu Yanayoendelea
-
Trump ametishia kuishambulia Iran kwa nguvu kubwa endapo itazuia meli za mafuta kupita katika Strait of Hormuz.
-
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, amesema siku ya Jumanne inaweza kuwa siku yenye mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya Iran.
-
Shirika la mafuta la Saudi Arabia limeonya kuwa soko la mafuta duniani linaweza kukumbwa na “janga kubwa” iwapo njia hiyo ya bahari itafungwa.
-
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema Israel bado haijamaliza operesheni zake dhidi ya Iran.
-
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema Cyprus inaweza kutegemea msaada wa Ufaransa katika hali ya mvutano huo.
Mashambulizi makubwa ya anga pia yameripotiwa kuikumba Tehran, huku milipuko mikubwa ikisikika katika maeneo kadhaa ya mji huo, wakati Trump akiahidi kumaliza vita hiyo “hivi karibuni”.
Mvutano huu unaongeza hofu ya kuongezeka kwa mgogoro mkubwa wa kijeshi katika Mashariki ya Kati ambao unaweza kuathiri uchumi wa dunia, hasa katika sekta ya nishati.