Matumaini, mashaka ziara ujumbe UN Tanzania

Dar es Salaam. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa (UN), umeanza vikao vya mazungumzo na vyama vya siasa kuhusu demokrasia na utawala bora nchini, huku baadhi ya vyama vikishindwa kutoa msimamo iwapo vitashiriki au havitashiriki.

Lakini, ziara ya Parfait Onanga-Anyanga, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa UN, imewagawa wadau, wengine wanapongeza na wengine wanatilia shaka, wakisema hawataki tena mambo ya bandia, bali wanataka kuuona uhalisia.

Wanaopongeza wanasema, alihitajika msuluhishi asiye na upande ili kuleta mshikamano, hivyo ujumbe wa UN ni sahihi kwa hilo na ukizingatia ni shirika lenye mamlaka ya amani kwa mujibu wa malengo ya kuanzishwa kwake.

Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika, Parfait Onanga-Anyanga akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mahmoud Kombo



Katika ziara yake nchini,  Parfait Onanga-Anyanga, amepanga kuzungumza na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Mapinduzi (CCM), ACT Wazalendo na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Sambamba na vyama hivyo, pia anatarajiwa kuzungumza na Spika wa Bunge, Mussa Zungu, Jaji Mkuu, George Masaju na Rais Samia Suluhu Hassan, ambao ni viongozi wa mihimili mitatu ya dola.

Mazungumzo ya Onanga-Anyanga, yanatarajiwa kujikita katika hali ya kisiasa, utawala bora na kuona namna UN inavyoweza kuunga mkono juhudi za kuimarisha taasisi za kidemokrasia, kusimamia mageuzi na kuendeleza mshikamano kupitia maridhiano.

Tayari, mwakilishi huyo ambaye pia ni Mkuu wa Ofisi ya UN katika Umoja wa Afrika (UNOAU), ameshakialika Chama cha ACT Wazalendo na kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wake kuhusu hayo.

Hatua hiyo ya UN, inakuja katikati ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kuleta mshikamano wa kitaifa, hasa baada ya kutokea kwa maandamano yaliyozaa vurugu na mauaji Oktoba 29, 2025.

Katika tukio hilo, baadhi ya watu walipoteza maisha, mali za watu binafsi na umma ziliharibiwa na Rais Samia aliunda tume kufanya uchunguzi.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche amesema watakapokuwa kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo, watasema.

“Tukiwa kwenye position (nafasi) nzuri ya kulizungumzia hilo, tutazungumza, lakini sasa ni mapema sana kusema chochote,” amesema.

Alipoulizwa iwapo Chadema imepokea barua au taarifa yoyote ya mazungumzo hayo, Heche alirudia majibu yake kuwa, ni mapema sana na watakapokuwa kwenye nafasi ya kulizungumza watazungumza.

Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe, amesema bado hawajapokea mwaliko wala taarifa yoyote kuhusu mpango wa mwakilishi huyo kuzungumza na chama hicho.

Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika, Parfait Onanga-Anyanga akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mahmoud Kombo.



Kwa sababu hiyo, Rungwe amesema inakuwa vigumu kuzungumza wakati hata mwaliko hawajapokea, wanasubiri wapokee kisha watazungumza kuhusu ushiriki wao.

“Bado hatujapata taarifa na tutakujibu kama tutashiriki hayo mazungumzo baada ya kupokea taarifa rasmi. Hatuwezi kusema kitu kabla hatujapokea taarifa au mwaliko,” amesema Rungwe.

Kwa upande wa Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu amesema tayari wameshapokea mwaliko wa mazungumzo na mjumbe huyo na kwamba wanashiriki.

Ameeleza ujumbe wa chama hicho, utaongozwa naye kama kiongozi wa chama, pia atakuwepo Katibu wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa kimataifa wa chama hicho, Mwanaisha Mndeme.

“Sisi tunashiriki na tumeshapokea mwaliko, tunakutana naye leo mchana. Ujumbe wa ACT Wazalendo uko tayari kwa mazungumzo hayo,” amesema Dorothy.

Wadau wapongeza, kutilia shaka

Akilizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga amesema bado hawajapokea barua ya mwaliko, watakapopokea hawatasita kwenda.

Amekwenda mbali zaidi na kueleza, kwa hali iliyokuwepo kulihitajika msuluhishi asiye na upande, kwa kuwa kamati nyingi za ndani zina upendeleo.

“Kwa hali tuliyonayo tulihitaji sana msuluhishi ambaye hana upande yaani objective (hana upendeleo). Kwa vile kamati za ndani nyingi ni biased (zina upendeleo),” amesema Anna.

Amesema kamati hizo zinashindwa kuaminika kwa kuwa unakuta wajumbe wake walikuwa kwenye mfumo wa Serikali iliyopo madarakani.

“UN pia ni chombo chenye mamlaka ya amani kutokana na malengo ya kuanzishwa kwake, hivyo ni sahihi kufanya inachokifanya,” amesisitiza Henga.

Kwa upande wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, amesema hawajapokea mwaliko wowote na hata kama watapokea, watatathmini malengo ya mazungumzo hayo ndio waamue kwenda.

“Kuna mengi ya kuangali,a kabla ya kufika hapo ni mapema kuzungumza lolote, hatutaki mambo ya bandia tena tunataka tuone uhalisia,” amesema.

Kwa hatua ya sasa, amesema hakuna kisichojulikana na kama mwakilishi anakuja akijifanya hajui chochote wakati vyombo vya kimataifa na waangalizi wa uchaguzi walishasema, ni mtu ambaye wanamuangalia kwa tahadhari.

“Kila jambo tunalichukulia kwa umakini mkubwa, tunachotaka Taifa lipone, kuwepo haki, uwajibikaji na ukweli,” ameeleza Mwabukusi.

Ameeleza wasiwasi wake ni mambo yaliyopo hadharani, lakini mwakilishi huyo anakuja kama mtu asiyejua chochote, hiyo inamfanya amtazame kwa tahadhari.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa upande wa UN, Kamati ya Mawaziri wa Jumuiya ya Madola (CMAG), imefanya uamuzi wa kuirudisha Tanzania katika ajenda rasmi ya jumuiya hiyo.

Uamuzi huo, umefanyika wakati wa mkutano wa 72 wa kamati hiyo, uliofanyika Machi 7, 2026 nchini Malta, huku Tanzania ikiwakilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Palamagamba Kabudi na .

Hatua hiyo inakuja kutokana na tathmini ya hali ya kisiasa na malalamiko ya uvunjifu wa demokrasia na haki za binadamu nchini, ikiwemo matukio ya Oktoba 29, 2025.

Katika tamko la kuhitimisha mkutano huo ulioongozwa na Naibu Waziri Mkuu wa Malta, Dk Ian Borg, CMAG imekaribisha utayari wa Serikali ya Tanzania kumpokea na kumpa ushirikiano Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola.

Mjumbe huyo anatarajiwa kuwasili nchini mwezi huu kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina kuhusu masuala mbalimbali yaliyoibuliwa na jumuiya hiyo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha nchi wanachama zinaheshimu Mkataba wa Jumuiya ya Madola.

Mawaziri hao wameitaka Serikali ya Tanzania kuchukua hatua za kutekeleza maeneo yaliyoainishwa katika mkutano uliopita wa Desemba 2025.

Jumuiya hiyo, imesisitiza ziara ya Mjumbe Maalum itatoa picha kamili na tathmini ya hali halisi, jambo litakalosaidia kutoa mapendekezo ya jinsi ya kuimarisha utawala wa sheria, demokrasia na nafasi ya kiraia nchini.

Mbali na Tanzania, CMAG pia ilijadili hali ya kisiasa nchini Uganda, ambayo pia imewekwa kwenye ajenda rasmi kutokana na ripoti za hivi karibuni za uvunjifu wa haki za binadamu.

Jumuiya hiyo, imepanga kufanya mkutano wake ujao Novemba mwaka huu, nchini Antigua na Barbuda na taarifa za maendeleo kuhusu nchi hizo zitatolewa na kufanyiwa uamuzi zaidi.


Mwishoni mwa mwaka jana, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Botchwey alimteua Rais mstaafu wa Malawi, Lazarus Chakwera kuwa mjumbe maalumu wa jumuiya hiyo kuja Tanzania.

Ziara ya Chakwera na ujumbe wake nchini Tanzania, ilipangwa kuwa ya siku nne kuanzia Novemba 18 hadi 21, mwaka jana, lakini hakuna taarifa rasmi kama ilifanyika au la.

Uamuzi wa kikao hicho cha 72 cha mawaziri, utafanya ziara hiyo ifanyike, ingawa haijajulikana ujumbe wa Jumuiya ya Madola utaongozwa nani.