Orodha ya mabilionea duniani iliyotolewa na Forbes imeonyesha kuwa utajiri wa mabilionea barani Afrika unaendelea kuongezeka kwa kasi. Kwa sasa, matajiri wakubwa 23 wa bara hilo wana utajiri wa pamoja unaokadiriwa kufikia dola bilioni 126.7.
Aliko Dangote bado anaongoza kama mtu tajiri zaidi Afrika akiwa na utajiri wa takribani dola bilioni 28.5. Utajiri wake umeongezeka kwa dola bilioni 4.6 mwaka huu kufuatia kupanda kwa karibu asilimia 69 kwa hisa za kampuni yake ya saruji, Dangote Cement, ambayo pia iliongeza mara mbili faida zake mwaka 2025 hadi kufikia rekodi ya naira trilioni moja.
Miongoni mwao pia ni Mohammed Dewji, maarufu kama “Mo”, ambaye mwaka 2026 utajiri wake unakadiriwa kufikia dola bilioni 2.1, sawa na takribani shilingi trilioni 5.45 za Kitanzania. Kwa utajiri huo, anaendelea kushika nafasi ya kwanza nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Dewji ni Mkurugenzi Mtendaji wa MeTL Group, kampuni kubwa ya biashara ya Tanzania iliyoanzishwa na baba yake katika miaka ya 1970.
Kampuni hiyo inajihusisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji na biashara, zikiwemo utengenezaji wa nguo, usagaji wa nafaka kuwa unga, uzalishaji wa vinywaji pamoja na mafuta ya kula katika maeneo ya Afrika Mashariki, Kusini na Kati. Mbali na Tanzania, MeTL pia inaendesha shughuli zake katika nchi 10 za Afrika, zikiwemo Uganda, Ethiopia na Kenya.
Aliyepata ongezeko kubwa zaidi la utajiri ni Abdulsamad Rabiu, ambaye utajiri wake uliongezeka kwa asilimia 120 na kufikia dola bilioni 11.2, na hivyo kuwa mtu wa tatu tajiri zaidi Afrika. Mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kupanda kwa asilimia 135 kwa hisa za kampuni yake ya BUA Cement katika soko la hisa la Nigeria.
Miongoni mwa waliopata mafanikio pia ni Michiel Le Roux, mwanzilishi wa Capitec Bank, kutokana na kupanda kwa hisa za benki hiyo. Hata hivyo, bilionea pekee ambaye utajiri wake haukuongezeka wala kupungua mwaka huu ni Nassef Sawiris wa Egypt, ambaye pia anamiliki hisa katika klabu ya soka ya Aston Villa pamoja na kampuni ya mavazi ya michezo Adidas.