Njombe. Wananchi wa vijiji saba wilayani Makete mkoani Njombe wananufaika na upatikanaji wa umeme wa uhakika kufuatia mradi wa uzalishaji umeme wa Ijangala uliofadhiliwa na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea).
Umeme unaozalishwa katika mradi huo unatajwa kusaidia kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wa eneo hilo.
Hayo yameelezwa leo Machi 10, 2026 na Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi wa Rea, Mhandisi Emanuel Yesaya, wakati wa ziara ya wahariri katika mradi huo uliopo kijiji cha Nasisiwe, kata ya Ukwama wilayani Makete.
Mradi huo unaendeshwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Kati kupitia kituo cha Diakonia cha Tandala.
Yesaya amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya uzalishaji umeme inayoungwa mkono na Serikali ili kuongeza uzalishaji wa nishati vijijini.
Amesema Serikali kupitia Rea imekuwa ikitoa ruzuku kwa waendelezaji wa miradi ya nishati kuanzia hatua za awali za maandalizi, ikiwemo kugharamia tafiti za awali za uwekezaji kama upembuzi yakinifu, tathmini ya athari za mazingira na maandalizi ya mpango wa biashara.
“Serikali kupitia REA inasaidia taasisi za Serikali na sekta binafsi kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme vijijini ili kuongeza kiwango cha umeme katika Gridi ya Taifa na kuimarisha ubora na uimara wa nishati,” amesema Yesaya.
Amesema REA imetoa ruzuku ya Sh1.63 bilioni kusaidia ujenzi wa miundombinu ya mradi wa Ijangala.
Aidha, kupitia Mpango wa Upanuzi wa Umeme Vijijini Tanzania, mradi huo ulipata mkopo nafuu wa Sh922 milioni kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za utekelezaji wake.
Amesema mbali na mradi huo kuimarisha huduma ya upatikanaji wa umeme, pia umetoa ajira kwa wananchi wa maeneo hayo.
“Rea inasaidia kuongeza uwekezaji katika miradi ya umeme vijijini ya Serikali na sekta binafsi ili kuongeza uzalishaji wa umeme katika Gridi ya Taifa. Mradi huu pia umepatiwa mkopo wa REA wa masharti nafuu wa Sh922 milioni,” amesema Yesaya.
Amesema mkoani Njombe, Rea imefadhili miradi mitano ya uzalishaji umeme inayozalisha jumla ya megawati tatu ambazo zinaingizwa katika Gridi ya Taifa.
Kwa upande wake, Mchungaji Silvia Sanga, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi wa Dayosisi hiyo, amesema wazo la kuanzisha mradi huo lilitokana na changamoto ya ukosefu wa umeme wa uhakika katika eneo hilo.
Amesema awali walikuwa wakitumia jenereta umeme unapokatika, hivyo kuwa na gharama kubwa za uendeshaji, lakini sasa hali ni tofauti.
Meneja wa kituo hicho, Daud Sanga, amesema miundombinu yote ya mradi imekamilika, ikiwemo jengo la kuzalisha umeme (power house), bwawa la maji, mabomba ya kusafirisha maji na kituo cha kupozea umeme.
“Tangu Machi 2025 tumeanza kuuza umeme kwa kupeleka katika Gridi ya Taifa,” amesema Sanga.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo ulianza kama wazo lililoonekana kuwa gumu, lakini msaada wa REA katika hatua za awali za maandalizi uliwezesha kufanikisha mradi huo.
“Sehemu kubwa ya fedha za ujenzi zimetoka Rea. Bila msaada huo, pengine tusingefika tulipo sasa,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema miradi ya wazalishaji wadogo wa umeme ina mchango mkubwa kwa taifa kwa kuongeza umeme katika Gridi ya Taifa na pia kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii kupitia ajira.
Balile ameishauri REA kuendelea kuunga mkono miradi kama hiyo kwa kuwa inaonyesha jinsi taasisi, makanisa na watu binafsi wanavyoweza kushiriki kikamilifu kukuza uchumi wa nchi.