Mvutano wazuka mabasi kuhamishiwa kituo cha Kange Tanga

Tanga. Mvutano umeibuka katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Tanga (RCC) baada ya wajumbe kutofautiana kuhusu mpango wa kuhamishia mabasi ya abiria yanayokuwa katikati ya jiji kwenda kwenye kituo kikuu cha mabasi cha Kange.

Kikao hicho kilikuwa kikijadili mapendekezo ya makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.

Katika mitazamo miwili tofauti, wapo waliounga mkono mpango huo wakisema utaongeza mapato ya jiji, na wengine wakisema hatua hiyo itawaumiza wananchi wa kawaida.

Meya wa Jiji la Tanga, Mustapha Selebosi, amesema jiji lilitarajia kukusanya zaidi ya Sh586 milioni kupitia jengo la kitalu cha kiuchumi lililojengwa katika kituo cha mabasi cha Kange, lakini matarajio hayo yamekwama kutokana na mabasi mengi kutotumia kituo hicho.

Meya wa jiji la Tanga Mustapha Selebosi akipambana na hoja ya halmashauri ya jiji la Tanga ya kuhamisha huduma huduma za usafiri wa abiria inayofanywa na magari ya mikoani  kuhamishiwa  kwenye kituo kikuu cha mabasi cha Kange.picha na Mbonea Herman.  



“Kwa makusudi tu kuna watu wanaonekana kama vile wameishika nchi kwamba hawaendi kwa kanuni za halmashauri.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwezekana leo tutoe tamko kwa Latra (Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini) ili watusaidie, kwa sababu wapo wamiliki ambao maeneo wanayoegesha mabasi yao hayana sifa ya kuwa vituo ‘terminal’,  lakini wapo katikati ya jiji ,” amesema Selebosi.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian amesema baada ya kufanya tafakari ya kina ameona mpango huo unaweza kuwaumiza wananchi zaidi kuliko kuwasaidia.

“Mheshimiwa Mstahiki Meya, kwenye mpango huu tulikuwa wote, lakini nimerudi nyuma baada ya kutafakari. Tukitekeleza hili anayeathirika ni nani, mwenye basi au mwananchi wetu? Ni wazi ni mwananchi wetu. Sasa tukizuia mabasi yasichukue abiria aliyepo mjini si tunamtesa mwananchi wetu?” amesema Dk Burian.

Amesema uzoefu kutoka maeneo mengine unaonesha kuwa kuwalazimisha abiria wote kwenda moja kwa moja stendi kuu kunaweza kuongeza usumbufu kwa wananchi.

“Juzi tulikwenda kusuluhisha mgogoro Korogwe baada ya waendesha magari kugoma wakitaka ruhusa ya kupakia na kushusha abiria kwenye vituo. Tuliona kuzuia magari yote yaende hadi stendi kunaleta adha kubwa kwa wananchi wetu,” alisema.

Shughuli za wasafiri na wasafirishaji zikiendelea katika kituo kikuu cha mabasi cha Kange jijini Tanga.



Amefafanua kuwa katika mfumo uliokubalika, mabasi yanaweza kushusha na kupakia abiria kwenye vituo vilivyokubalika kisheria kabla ya kuendelea na safari zao.

“Tuliruhusu vituo vya mabasi vitumike kama vituo vya kushusha na kupakia abiria, kisha gari liende kwenye kituo kikuu kulipa ushuru na kuendelea na safari. Wanaoshuka njiani washushwe kwenye vituo vinavyokubalika kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Dk Burian pia amekumbusha kuwa juhudi za awali za kuhamisha mabasi yote kwenda Kange ziliwahi kufanywa na viongozi waliomtangulia, lakini hazikufanikiwa.

“Hata wakuu wa mikoa waliotangulia walijaribu kutekeleza mpango huu. Martine Shigella (2016-2021) alijaribu, Mwantumu Mahiza (2011-2016), alijaribu, lakini haikuwezekana. Hivyo ni lazima tujiulize shida ni nini kabla ya kufanya maamuzi,” amesema.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Kassim Amar Makbel amependekeza suluhisho la kati kwa kuruhusu mabasi kuendelea kupakia abiria katika vituo vyao, lakini kwa kulipa ushuru mara mbili katika vituo vyao na katika kituo cha Kange.

“Sisi tuliwekeza fedha nyingi sana kujenga stendi ya Kange, lazima ifanye kazi. Hatuwezi kusema tumekosea halafu tubomoe. Tunatakiwa kutafuta suluhisho litakaloifanya ifanye kazi,” amesema Makbel.

Mkuu wa mkoa Tanga,Dkt Batilda Burian akizungumzia mpango uliokuwepo wa kuhamisha huduma za usafiri wa abilia wa mikoani kutoka katikati ya jiji la Tanga hadi kituo kikuu cha mabasi Kange. picha na Mbonea Herman   



Ameongeza kuwa mfumo huo unaweza kuwahamasisha wamiliki wa mabasi kuanza kuitumia zaidi stendi hiyo.

“Mtu akitaka kupakia kwenye terminal yake alipe ushuru, halafu akiingia Kange alipe tena. Taratibu wataanza kuona ni rahisi zaidi kutumia stendi ya Kange,” amesema.

Mbunge huyo pia amependekeza mabasi ya mikoani yafike katika kituo cha Kange angalau saa moja kabla ya kuanza safari ili kuongeza shughuli za kibiashara katika kituo hicho.

“Kwa sasa Kange ni kama sehemu ya kupita tu. Hakuna shughuli za biashara kwa sababu abiria hawakai pale. Tukisema basi lifike saa moja kabla ya safari, abiria watahudumiwa, wataingia madukani na hata mapato yataongezeka,” amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Latra Mkoa wa Tanga, Shedrack Malale amesema wamiliki wa mabasi wenye vituo vinavyokidhi viwango vya kisheria wanaweza kuendelea kutoa huduma huku wale wasio na vituo halali wakitakiwa kuhamia Kange.

“Ni vyema kuziondoa gari zote ambazo hazina stendi katikati ya jiji. Ofisi zao zibaki kama sehemu za kukatia tiketi tu. Pia, tutapita kukagua vituo vilivyopo kuona kama vinakidhi viwango vya kisheria,” amesema Malale.

Amesema mpango huo pia utasaidia kupunguza msongamano wa magari katika baadhi ya barabara za katikati ya jiji.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Mkoa wa Tanga, Abdi Hussein amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kubadilisha msimamo kuhusu mpango huo.

“Hili kwetu lilikuwa ni kilio kikubwa sana. Uamuzi huu utaleta nafuu kwa wananchi kwa sababu kwa sasa kufika kituo cha Kange kunaweza kugharimu hadi Sh15, 000, hasa kwa wanaosafiri usiku,” amesema.