Rostam ainunua Nation Media Group

Dar es Salaam/Nairobi. Mfanyabiashara wa Afrika Mashariki, Rostam Azizi, kupitia kampuni yake ya Taarifa Ltd amenunua hisa zote zilizokuwa zikimilikiwa na Aga Khan Fund for Economic Development (AKFED) katika kampuni ya NPRT Holdings Africa Limited, hatua inayomfanya kuwa mbia mkuu wa Nation Media Group (NMG).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 10, 2026, inaeleza kuwa uamuzi huo unahitimisha ushirikiano wa zaidi ya miaka 66 kati ya AKFED na kampuni ya habari ya Nation Media Group (NMG) uliodumu tangu mwaka 1959. 

Kupitia makubaliano hayo, Taarifa Ltd itanunua hisa 92,618,177 za kawaida zinazomilikiwa na NPRT katika NMG, huku mchakato wa kukamilisha ununuzi huo ukitarajiwa kuchukua miezi mitatu hadi minne baada ya kupata vibali vya kisheria kutoka kwa mamlaka husika.

NPRT Holdings Africa Limited inamiliki asilimia 54.08 ya hisa za NMG, sawa na hisa za kawaida 92,618,177.

NMG ni moja ya kampuni kubwa ya habari Afrika Mashariki, yenye shughuli zake nchini Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda.

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi wa AKFED, Sultan Allana, amesema taasisi hiyo inajivunia mchango wake katika kujenga moja ya taasisi zinazoheshimika zaidi za habari barani Afrika.

Kwa upande wake, Rostam amesema ana heshima kubwa kuwa mbia mkuu wa NMG, akisisitiza kuwa ataendeleza misingi ya uhuru wa uhariri huku akiwekeza katika mageuzi ya kidijitali ili kuimarisha nafasi ya kampuni hiyo katika tasnia ya habari.

 “NMG ni taasisi muhimu sana kwa Afrika Mashariki. Tutahakikisha tunalinda uhuru wa uhariri na kuwekeza zaidi ili kuimarisha mafanikio yake kama taasisi inayoongoza ya habari huru katika ukanda huu,” amesema Rostam.

Rostam ana uzoefu katika sekta mbalimbali zikiwemo madini, mawasiliano, kilimo, nishati, ujenzi na vyombo vya habari.

Aliwahi kuwa miongoni mwa waanzilishi na wanahisa wa Mwananchi Communications Limited (MCL) kati ya mwaka 2000 na 2006, kampuni iliyoanzisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, ambayo baadaye yalinunuliwa na NMG.

NMG kuendelea kuorodheshwa sokoni

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kampuni ya Taarifa Ltd haina mpango wa kutoa ofa ya kununua hisa zote zilizobaki wala kuiondoa NMG katika masoko ya hisa.

Hivyo, hisa za NMG zitaendelea kuuzwa Nairobi Securities Exchange, pamoja na masoko mengine ya hisa ya Dar es Salaam Stock Exchange, Uganda Securities Exchange na Rwanda Stock Exchange.

Taarifa ilieleza mbali na uwekezaji huo, mtandao wa maendeleo wa Aga Khan utaendelea kusaidia maendeleo ya taaluma ya uandishi wa habari kupitia Chuo Kikuu cha Aga Khan, hususan kupitia Shule ya Uzamili ya Mawasiliano na Vyombo vya Habari.

Hata hivyo, kukamilika kwa ununuzi huo kunategemea kupatikana kwa idhini kutoka kwa mamlaka za udhibiti wa sekta mbalimbali.