Dar es Salaam. Siku moja baada ya ada mpya ya uendelezaji wa miundombinu ya bandari (PID) kulalamikiwa, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeeleza sababu za kuianzisha na kuisogeza hadi Julai mosi mwaka huu.
Ada hizo mpya zilipaswa kuanza kutumia Machi 8, 2026 lakini baada ya kutangazwa na kuibua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau na wananchi, baadhi wakidai wameshtukizwa na wengine wakihoji nafasi ya kampuni ya DP World katika kuiendeleza, ikizingatiwa kuwa ndiyo iliyopewa nafasi ya kuendesha bandari hiyo.
Baada ya kuwapo kelele hizo, uongozi wa TPA ulisitisha ada hizo kwa muda ukisema lengo ni kuwawezesha wateja wote wa nje na ndani ya nchi, pamoja na umma kwa ujumla, kujiandaa.
“Muda uliotolewa utawawezesha watoa huduma kila mmoja kukamilisha masharti ya mikataba aliyonayo baina yake na wateja wake wa ndani na nje ya nchi ndani ya kipindi cha muda uliobaki hadi kufikia Juni 30, 2026,” imeeleza sehemu ya taarifa Taarifa ya TPA iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu, Plasduce Mbosa.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa TPA, Dk George Fasha anasisitiza kuwa hakukuwa na ushtukizaji na wadau wote muhimu walishirikishwa miezi sita iliyopita na hata maoni yao yalijumuishwa wakati wa kuunda na kutangaza ada hizo.
“Hata mdhibiti wetu ambaye ni TASAC alikutana na wadau na kupata maoni yao kabla ya kupitisha ada hizi. Lengo ni zuri, tunataka kuboresha miundombinu yetu ili kuongeza ufanisi wa bandari yetu na kurahisisha shughuli za uchukuzi kwa sasa na siku zijazo. Ada ya mazingira ni suala la uzingatiaji wa viwango vya kimataifa na inatozwa kote duniani,” alisema Dk Fasha.
Dk Fasha alisema TPA inafanya jukumu la kuendeleza miundombinu ya bandari kwa kuwa ndiyo inayofahamu maeneo ya kimkakati na yenye biashara zenye manufaa kwa Taifa na kuwa watoa huduma kama DP World, wao wanahusika tu na uendeshaji wa kibiashara.
“Uwekezaji mwingine ni wa kimkakati huwezi kusubiri utekelezwe na watoa huduma, Mathalan, ujenzi wa matenki ya kuhifadhi mafuta ambao unatekelezwa hivi sasa gharama zake ni zaidi ya Sh670 bilioni, anayepaswa kutoa pesa hizo ni TPA kwakuwa ni muhimu kwa nchi lakini kibiashara inaweza isiwe muhimu sana,” Alisema Dk Fasha.
Anasema uendelezaji mwingine unazingatia masilahi ya usalama na uchumi wa nchi, hivyo huwezi kumwachia mwekezaji, lakini masuala yanayohitaji maamuzi ya biashara ya haraka kama ununuzi wa mitambo, ndiyo wanaweza kuachiwa wawekezaji.
Kuhusu suala la kuchelewa kwa mizigo na msongamano bandarini, Dk Fasha alisema hilo linatokana na ongezeko la mizigo akisema bandari hiyo imevutia biashara kubwa mwaka 2025/2026 na kusisitiza kwa ndiyo maana TPA inaweka kipaumbele katika uboreshaji wa miundombinu, ili kuhudumia mizigo kwa haraka.
Machi 8, 2025 Mbossa aliliambia Mwananchi kuwa kupitia mabadiliko hayo ya ada, TPA itaweza kujenga magati mapya 18 ndani ya kipindi cha miezi 24 akisema baada ya kukamilika kwa mradi huo na mingine ya kuboresha shughuli za bandari hiyo, watumiaji watapata nafuu kubwa.
“Baada ya ujenzi wa magati haya tutakuwa na eneo la kutosha la kuhifadhi mizigo, gharama za kuchelewa kuchukua mizigo zitaondoka, hivyo watumiaji wa bandari watapata nafuu kwa namna nyingine huku huduma za bandari zikiboreshwa,” alisema Mbossa.
Wakati hayo yakielezwa, Mwenyekiti wa Jkumuiya ya Wafanyabiashara Taanzania (JWT), Hamis Livembe amesema kwa kawaida gharama hazipaswi kuwa kubwa kwani Serikali hupata fedha nyingi katika ushuru wa forodha na VAT, lakini ada iliyoanzishwa itamgusa kila mtu hata kama si mfanyabiashara.
“Malalamiko yatakuwa mengi, kuna watu wananunua magari na wengine wanakwenda kuchukua vitu vyao vya kujengea au majumbani na hii haichagui na haina msamaha kama kodi. Sasa sijui kigezo gani kimetumika kuongeza hizi kwa sababu ada ikiongezwa inakuwa shida. Na mwisho wa siku kusogeza mbele ni kuahirisha tatizo, siyo kutatua tatizo waangalie namna ya kufanya,” amesema.
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Bandari Kavu Tanzania (CIDAT), Meleck Shange amesema changamoto kubwa inayoonekana, mwaliko unapotolewa baadhi ya taasisi husika zimekuwa zikipeleka watu wa chini ambao wanakuwa hawawezi kusikiliza na kuchanganua kwa ufanisi athari za jambo husika litakapofanyika
Hali hiyo imefanya baadhi ya mambo kupita na kuleta malalamiko makubwa licha ya wao kupewa nafasi ya kuzungumza lakini wakashindwa kuitumia.
“Kwa mfano sisi tulipokwenda kuna viti vilikuwa vimewekwa vikawa vinatuathiri katika utendaji wetu, tukapaza sauti na havikuwekwa tena. Ni kama wengine hawakubeba kwa uzito suala hili japokuwa tulijaribu kuwasemea, inakuwa haibebwi kwa uzito kama wangezungumza wenyewe,” amesema.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha (Taffa), Edward Urio amesema kabla ya kuanza kutozwa kwa ada hiyo walishirikishwa lakini kasumba iliyojengeka wanachama wengi hudhani baadhi ya mambo ni kwa ajili ya viongozi.
Amesema Taffa ilipopata pendekezo hilo iliandaa dodoso ambalo walilituma kwa wanachama wake zaidi ya 1,500 ili watoe maoni yatakayokwenda kuwasilishwa katika kikao husika.
“Lakini waliotoa maoni ni wanachama wawili tu. Ukipewa nafasi ya kutoa maoni ili yakaboreshe sheria halafu usiipe umuhimu kwa kuona haikuhusu na kila mmoja anajiona yuko na kazi nyingi na kuona ni la viongozi si vyema, likimgusa ndiyo anakuja kushtuka hii ni mbaya,” amesema.
Taffa ilipoona ada hiyo inaanza kutozwa iliandika barua ya kuomba mizigo iliyokuwa imekwama bandarini ikiwa imefika tangu Januari hadi Februari na walipewa muda hadi Julai mosi mwaka huu.
“Tulifanya hivyo kwa sababu tuliona baadhi ya watu wataingia katika matatizo ambayo hayajajengwa na wao na tumepewa ahueni hadi Julai mosi. Lakini bado tumeomba tuzungumze nao namna ambayo itakuwa na athari na kiuchumi,” amesema.
Kutokana na wengi kutoelewa, Urio amesema wamelazimika kuitisha mkutano wa dharura wanachama Machi 11, 2026 kujadili suala hilo na kuja na azimio moja kama chama na kwa ajili ya hatua zinazofuata.
Wakati wadau wakisema hayo, Mtaalamu wa Uchumi, Oscar Mkude amesema ada hiyo haina athari kwa wanaopeleka mizigo nje ya nchi, isipokuwa mzigo anaubeba mlaji wa kawaida, kwa kuwa gharama za bidhaa zitaongezeka.
“Wafanyabiashara wa ndani watajikuta wanapunguza uuzaji wa biashara zao kutokana na kuwepo kwa kitu kama hiki,” amesema.
Kuhusu suala la DP World, Mkude ameasema “uwepo wa waendeshaji binafsi hakuiondoi TPA bandarini isipokuwa katika uhudumiaji wa mizigo pekee.”