Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) leo imekutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, katika kikao cha kimkakati kilicholenga kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili kuunga mkono mageuzi ya uchumi wa Tanzania na kukuza uwekezaji kwa maendeleo ya muda mrefu.
Kwa Upande wa SBL mazungumzo hayo yaliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Paul Makanza, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Obinna Anyalebechi.
Mazungumzo yalijikita katika nafasi muhimu ya sekta binafsi katika kusaidia utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya taifa, ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ambayo inalenga kuifanya Tanzania kuwa uchumi wa dola trilioni moja kupitia uwekezaji, kukuza viwanda na mageuzi ya mfumo wa uchumi.

Kama moja ya kampuni kubwa za uzalishaji nchini na miongoni mwa walipa kodi wakubwa, SBL inachangia zaidi ya shilingi bilioni 220 kila mwaka katika uchumi wa taifa kupitia kodi, uwekezaji, ushirikiano na wazabuni pamoja na miradi ya maendeleo ya jamii.
Katika miaka ya hivi karibuni, kampuni hiyo imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 165 na kuimarisha shughuli zake nchini Tanzania, jambo linaloonesha dhamira yake ya muda mrefu katika kuendeleza uzalishaji wa ndani, kukuza viwanda na kuimarisha mnyororo wa thamani wa ndani.
Mbali na shughuli zake za utengenezaji wa bia, SBL pia inaendelea kuwekeza katika ununuzi wa malighafi kutoka kwa wakulima wa ndani, ikijumuisha shayiri, mahindi na mtama vinavyolimwa nchini katika mchakato wake wa uzalishaji. Hatua hizi zinasaidia kuongeza kipato cha wakulima, kuimarisha mnyororo wa thamani wa ndani na kuchangia juhudi za taifa za kukuza uchumi wa viwanda.

Kupitia shughuli zake, kampuni hiyo imetoa ajira rasmi kwa watnzania 800 , huku trakribani watu 140,000 wakinufaika na mnyororo wa ajira unaotokana na kampuni hiyo kote nchini.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi, alisema:“Tanzania itaendelea kuleta mageuzi ya kiuchumi kupitia ushirikiano imara kati ya serikali na sekta binafsi.
Sisi kama Kampuni ya Bia ya Serengeti tunaendelea kujizatiti kuwekeza katika uzalishaji wa ndani, kuimarisha mnyororo wa thamani wa ndani na kusaidia ukuaji wa uchumi shirikishi.
Mazingira ya uwekezaji yaliyo thabiti na yenye ushindani yataendelea kuwa muhimu katika kufungua fursa kubwa zaidi za uchumi wa Tanzania.”
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na sekta binafsi katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa.
“Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inalenga kuifanya Tanzania kuwa uchumi wa dola trilioni moja, ambapo sekta binafsi itakuwa na nafasi kubwa katika kuchochea uwekezaji, ajira na ukuaji wa uchumi.
Mazungumzo na ushirikiano unaoendelea na wadau wa sekta binafsi kama Kampuni ya Bia ya Serengeti ni muhimu katika kusaidia kuboresha mazingira ya uwekezaji na kukuza uchumi” alisema Mkumbo.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa makubaliano ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na kukuza uwekezaji, kuimarisha uthabiti wa mifumo ya udhibiti na sera, kukuza uzalishaji wa ndani pamoja na maendeleo yake ya uchumi jumuishi, hatua itakayochangia kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya taifa kupitia ushirikiano imara kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.