STRATEGIS INSURANCE TANZANIA LIMITED YATOA MILIONI 15/- KUKARABATI VYOO SHULE YA MSINGI MSASANI B

Na Mwandishi Wetu

SHULE ya Msingi Msasani B imepokea ufadhili wa kukarabati vyoo 12, hatua inayolenga kuboresha usafi na kuunda mazingira salama na yenye afya kwa wanafunzi na walimu.

Msaada huo wenye thamani ya Sh.milioni 15 umetolewa na kampuni ya Strategis Insurance Tanzania Limited kama sehemu ya mchango wake katika maadhimisho ya kimataifa ya Siku ya Wanawake Duniani(IWD), ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8 ya kila mwaka.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Dkt. Flora Minja amesema mpango huo umechochewa na kaulimbiu ya IWD ya mwaka huu, Give to Gain” (Toa ili Upate), ambayo inahamasisha watu kurudisha fadhila kwa jamii.

Amesema waliamua kusaidia shule hiyo baada ya kubaini hitaji la haraka la kuboresha miundombinu ya vyoo wakati wa ziara yao shuleni hapo.

“Kupitia kaulimbiu ya mwaka huu, ‘Give to Gain,’ tuliona ni muhimu kufanya jambo lenye maana kwa wanafunzi kwa kuchangia kuboresha miundombinu ya usafi ili waweze kusoma katika mazingira safi na salama,” amesema.

Ameongeza ingawa mradi huo unawanufaisha wavulana na wasichana, pia unaakisi dhamira pana ya maadhimisho ya IWD kwa kusaidia kuunda mazingira yanayowawezesha vijana kustawi.

Dkt. Minja pia amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha wanawake zaidi kufikia nafasi za juu za uongozi, akibainisha kuwa wanawake bado ni wachache katika ngazi za juu za usimamizi.

“Katika ngazi za juu za uongozi, wanawake bado ni wachache. Sisi tuliopo katika nafasi hizi tunajitahidi kutoa ushauri na kuweka sera zitakazowasaidia wanawake wengine kupanda hadi ngazi za juu za maamuzi,” amesema.

Kwa mujibu wake, kaulimbiu ya mwaka huu pia inawahimiza wanawake walioko katika nafasi za uongozi kuwainua wengine ili katika miaka ijayo kuwe na uwakilishi mkubwa zaidi wa wanawake katika nafasi muhimu za uongozi.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msasani B, Bw. Badru Musoke, ameishukuru kampuni hiyo kwa msaada huo, akieleza wakati kampuni ilipotembelea shule waliwasilisha maeneo matatu ya kipaumbele yaliyohitaji msaada, ambapo ukarabati wa vyoo uliteuliwa.

“Msaada huu ni muhimu sana. Serikali inafanya juhudi kubwa kuboresha elimu, lakini haiwezi kufanya kila kitu peke yake. Inahitaji msaada wa wadau kama Strategis Insurance,” ameongeza.

Pia amesema ukarabati huo utasaidia kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma bora za usafi na salama, ambazo ni muhimu kwa mazingira bora ya kujifunzia. Pia alibainisha kuwa shule inakabiliwa na changamoto ya kuboresha miundombinu ya michezo ili kukuza vipaji vya wanafunzi.

“Lengo letu si kuhakikisha tu wanafunzi wanafanya vizuri kitaaluma, bali pia kukuza vipaji vyao. Tuna uwanja wa michezo, lakini bado haujafikia kiwango tunachotamani. Kama wadau zaidi watajitokeza kutusaidia, itasaidia sana kuuboresha,”amesema.