Arusha. Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imesaini hati ya makubalino (MoU) na taasisi binafsi ya Global Education Link Ltd yenye malengo la kushirikiana kwenye nyanja za kitaaluma, uwekezaji na teknolojia.
Hati hizo za makubaliano zimesainiwa leo Jumanne, Machi 10, 2026 katika taasisi hiyo na Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Maulilio Kipanyula na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Global Education Link Ltd, Abdulmalik Mollel kuwa makubaliano hayo yataongeza idadi ya wanafunzi wanaotoka nje ya nchi kusoma kwenye taasisi hiyo.
Profesa Kipanyula amesema taasisi hiyo ilianzishwa kwa dhamira moja kubwa ambayo ni kuzalisha kizazi cha wanasayansi na wabunifu mahiri ambao ni wabobevu katika eneo la sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuwa na kizazi kitakacholeta mageuzi na mapinduzi ya kiuchumi kwenye jamii ya Kitanzania.
“Msingi wa taasisi hii ulijengwa kwa imani kuwa Afrika ina vipaji na vijana wenye akili za kutosha wenye uwezo wa kutoa suluhisho kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia, leo ninasema kwa kujiamini kabisa Afrika sio bara la kusubiri majawabu ya changamoto zinazoikabili bali linaweza kuzalisha majawabu ya changamoto hizo,” amesema Profesa Kipanyula.
Amesema makubaliano hayo yanakuja kwa kutambua hakuna taasisi inayoweza kufanikiwa kwa kufanya kazi pekee yake bila kushirikiana na taasisi zingine, pia hakuna Taifa linaloweza kusonga mbele likiwa lenyewe pasipo ushirikiano na mataifa mengine duniani.
“Hakuna ubunifu unaoweza kufanywa na taasisi moja pekee yake na ukaenda sokoni bila kuhitaji wadau wengine, hivyo kupitia ushirikiano huu inalenga kama taasisi ya NM-AIST ambayo imebobea katika kutoa mafunzo katika ngazi ya uzamili na uzamivu,moja ya matokeo tunayotarajia kwenye haya makubaliano ni kuongeza idadi ya wanafunzi hasa wa kimataifa.
“Makubaliano haya ni ya kimkakati kwa sababu tunatekeleza maono ya Serikali na wizara yetu kwenye eneo hili la ‘umataifishaji’ wa elimu yetu,hivyo tunaunganisha nguvu kati ya taasisi yetu na Global Education Link Ltd ili kuongoza hii ajenda ya ‘umataifishaji’ na kuona namna tunaweza kuvutia vijana wenye vipaji waje kusoma kwetu,” amesema Profesa Kipanyula.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo unafungua milango ya kutafuta rasilimali fedha, kuandika miradi ya pamoja katika sekta ya elimu, utafiti na ubunifu hivyo kufikia malengo makubwa zaidi kwa kushirikiana na taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Global Education Link Ltd,Abdulmalik Mollel amesema taasisi yake itahakikisha inafanya yaliyo katika makubaliano kuongeza tija ya kitaaluma na uwekezaji ambao ni msingi muhimu katika kufikia malengo waliojiwekea.
“Naona vyuo vikuu vya nje jinsi vinavyotafsiri elimu,uwekezaji na teknolojia namna wanavyobadilisha uchumi wa nchi zao, pia, kupitia elimu ambayo vijana wao waliyoipata itumike kutatua changamoto za kiuchumi,” amesema Mollel.
Amesema mataifa yaliyoendelea walitengenea vituo vya kutosha vya kufanya tafiti na kuwekeza ipasavyo mitaji na teknolojia ambayo iligeuza hali ya nchi hizo kiuchumi kwasababu hakuna mabadiliko yeyote yasiyohitaji tafiti kutoka taasisi za elimu ya juu.