Tabora. Wanawake wanaojishughulisha na kilimo mkoani Tabora wamepewa zana za kilimo na pembejeo, pamoja na ufuatiliaji wa kilimo chenye tija, kwa lengo la kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.
Zana vilivyotolewa ni pamoja na pampu za unyunyiziaji wa dawa, mabomba na pampu za maji kwa ajili ya umwagiliaji pale panapokua changamoto ya upatikanaji wa maji, pamoja na buti za shamba, mbolea na viuatilifu.
Lengo kuu ni kuendeleza kilimo bora na chenye tija miongoni mwa wanawake wa mkoa huo.
Zana na pembejeo za kilimo zimetolewa leo, Machi 10, 2026, na Benki ya Kilimo (TADB) mkoani Tabora ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya kilimo.
Kikundi cha Peace and Love, kilicho na wanachama zaidi ya 50, ni miongoni mwa wanufaika wa vifaa hivyo.
Kikundi hicho kinajishughulisha hasa na kilimo cha zao la mpunga, ambapo wanalima hadi ekari 10 kila msimu.
Akizungumza na Mwananchi, Swaumu Mohamedi, mwanakikundi na mnufaika wa vifaa hivyo, amesema kuwa zana na pembejeo hizi zitasaidia kuboresha kilimo chao.
“Tulikua tunakodisha vifaa hivi,sasa mpaka kufikia muda wa mavuno faida inakua imebaki kidogo jambo ambalo linafanya tusionekane kama tunaendelea kiuchumi.”
Chausiku Kananda, TADB inapaswa kuongeza juhudi za kuwaunga mkono wakulima, hususan wanawake, kutokana na gharama kubwa za pembejeo na zana za kilimo.
Amesema ili kupata mavuno mazuri mkulima anapaswa kutumia mbolea angalau mara mbili kwa msimu, lakini kutokana na gharama kubwa za uzalishaji hulazimika kuitumia mara moja tu, hali inayosababisha mavuno kuwa madogo.
“Tunatumia mbolea mara moja tu ili kupunguza gharama. Kwa mfano, kwa wakulima wa mahindi ili kupata mavuno mazuri unapaswa kuweka mbolea mara mbili, lakini kutokana na gharama tunashindwa kufanya hivyo. Hali ni hiyo hiyo kwa mpunga; maji yakipungua tu, mavuno yanakuwa ya mashaka,” amesema.
Ofisa Masoko wa TADB, Richard Steven, amesema lengo la kuwawezesha wanawake hao wakulima ni kuwasaidia kunufaika na pembejeo hizo ili baadaye waweze kuchukua mikopo kutoka benki hiyo na kujiinua kiuchumi kwa haraka.
“Wanawake ni nguvu kazi muhimu sana kiasi kwamba akiwa na fedha za kutosha basi mahitaji ya familia na jamii hayatokua na shida kwani zitastawi vizuri,” amesema.
Amesema vifaa na viuwatilifu hivyo vimegharimu Sh10 milioni ambavyo vimetolewa bure kwa wakulima hao, kuwawezesha kulima kilimo chenye tija na kupata maendeleo kwa haraka zaidi ikilinganishwa na sasa ambavyo wanatumia fedha nyingi kuendesha kilimo halafu faida ndogo.