Dar es Salaam. Katika jamii nyingi za leo, imezuka dhana potofu kwamba kazi ya kulea watoto ni ya walimu. Wazazi wengi wamejikuta wakitelekeza jukumu lao la msingi, wakikabidhi watoto wao kwa walimu kana kwamba shule ndiyo nyumba ya pili ya mtoto kwa kila jambo.
Mtoto anaposhindwa kimaadili au kielimu, lawama huelekezwa kwa walimu kwa haraka mno, kana kwamba wao ndiyo waliomleta mtoto duniani au wanaishi naye saa zote. Hii ni changamoto kubwa inayohitaji mjadala wa kina na mabadiliko ya mtazamo katika jamii.
Mzazi ndiye mlezi na mwalimu wa kwanza wa mtoto. Kabla mtoto hajaingia darasani, tayari ameshajifunza mengi kutoka kwa mzazi kama kuongea, kujieleza, tabia, maadili, hata namna ya kujihusisha na watu wengine.
Ikiwa mtoto amekulia katika familia inayothamini heshima, adabu, bidii, na uadilifu, hali hiyo itajitokeza hata shuleni. Lakini ikiwa malezi nyumbani ni duni, basi walimu hawana miujiza ya kubadilisha tabia za msingi zilizoasisiwa tangu utotoni.
Kumekuwa na ongezeko la matukio ambapo walimu hugundua tabia potofu kwa baadhi ya wanafunzi kama kutojiheshimu, kusema uongo, wizi, hata matumizi ya lugha chafu, lakini cha kushangaza, wazazi wanapoitwa na kuelezwa kuhusu hali hiyo, huonyesha mshangao mkubwa kana kwamba hawajawahi kuishi na huyo mtoto.
Mzazi anaweza kwa mfano kusema: “Haiwezekani! Mtoto wangu hawezi kufanya hivyo.” Ukweli ni kwamba mtoto huyo anayeonekana mtulivu nyumbani anakuwa na tabia tofauti kabisa shuleni kwa sababu mzazi hakujishughulisha kumlea kwa karibu wala kumtambua tabia zake.
Mfano halisi ni mwalimu mmoja wa shule ya msingi aliyeona mwandiko wa ajabu kwenye daftari la mwanafunzi wa darasa la sita.
Alipomhoji, alikiri kuwa ni picha za matusi alizochora wakati wa somo. Alipoitwa mzazi wake, alikasirika na kudai kuwa mwanawe ni mtulivu na ni “mwenye heshima nyumbani.”
Huu ni mfano wa wazi wa mzazi asiyehusika kikamilifu katika malezi ya mtoto wake. Inashangaza kwamba mzazi huyo hajui anachofanya mwanawe akiwa mbali naye.
Malezi si kazi ya mtu mmoja. Ni mchakato unaohusisha jamii nzima, lakini msingi wake mkubwa uko nyumbani. Walimu wana wajibu wa kielimu na kiasi fulani cha kinidhamu, lakini mzigo wa msingi wa maadili unapaswa kubebwa na mzazi.
Ikiwa mtoto anafundishwa heshima, nidhamu na maadili tangu awali, walimu watakuwa na kazi rahisi ya kuendeleza tu.
Wapo wazazi wanaodhani kuwapeleka watoto shule nzuri au ghali ndiyo kilele cha malezi bora. Hawatambui kuwa hata shule ya gharama ya juu haina uwezo wa kubadilisha tabia ya mtoto asiyelelewa vizuri nyumbani.
Shule inaweza kumpa maarifa, lakini haimjengi mtoto kiutu kwa undani. Asili ya utu wa mtoto inaasisiwa nyumbani kupitia katika maneno, vitendo, na mifano anayoiona kila siku kwa wazazi wake.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba baadhi ya wazazi wanaonekana kukwepa majukumu yao hata katika mambo ya msingi.
Wanaacha watoto wao kuangalia runinga au kutumia simu bila udhibiti, wanawapuuza wanapoonyesha mabadiliko ya tabia, au hata kutohudhuria mikutano ya wazazi shuleni. Wazazi wengine wanaacha hata kufuatilia maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao wakiamini kazi hiyo ni ya walimu pekee. Hali hii ikiachwa iendelee, itazidi kuathiri kizazi kijacho.
Ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha anakuwa karibu na mtoto wake. Hili linaweza kufanyika kwa njia mbalimbali: kuzungumza na watoto kila siku, kujua marafiki zao, kufuatilia mahudhurio yao shuleni, na kuchunguza mienendo yao mitandaoni.
Mzazi anapaswa kuwa mlezi wa karibu, rafiki wa kweli, na mshauri wa daima kwa mtoto wake. Kwa kufanya hivyo, atakuwa amepunguza kwa kiwango kikubwa mzigo wa malezi kwa walimu.
Walimu tayari wanabeba majukumu mengi. Wanafundisha madarasa yenye wanafunzi wengi, wanapimwa kwa matokeo ya kitaaluma ya wanafunzi wao, wanahitajika kufanikisha mtalaa unaobadilika kila mara, na pia kukabiliana na changamoto za kijamii kama ukosefu wa vifaa vya kufundishia, mshahara mdogo na mazingira magumu ya kazi. Ni wazi kwamba kuongeza mzigo wa malezi kwao ni kuwaonea.
Jamii inayotegemea walimu kulea watoto wao inajidanganya. Mafanikio ya mtoto kitaaluma na kimaadili hayawezi kufikiwa bila ushirikiano wa karibu kati ya shule na familia.
Shule na walimu ni washirika wa mzazi katika safari ya malezi, lakini mzazi ndiye anayepaswa kuwa nahodha wa meli hii. Tukiwapa walimu kila jukumu, tutajikuta tunazalisha kizazi kisicho na mwelekeo, kinachokosa msingi wa maadili na utu.
Katika hali ya sasa ya mabadiliko ya kijamii, kiteknolojia na kiutamaduni, watoto wanakumbwa na mitazamo mingi potofu kutoka mitandao ya kijamii, vyombo vya habari, na marafiki.
Hali hii inahitaji mzazi awe mstari wa mbele kufuatilia na kurekebisha mienendo ya watoto wao kabla mambo hayajaharibika. Ulimwengu wa sasa una changamoto nyingi ambazo mtoto hawezi kuzishinda bila uongozi na uangalizi wa karibu kutoka kwa mzazi.
Tusisahau kuwa kila mtoto ni kielelezo cha familia yake. Malezi bora huanzia nyumbani na huonekana kwa namna mtoto anavyojiheshimu, anavyowaheshimu wengine, na jinsi anavyoshughulika na majukumu yake.
Tukiendelea kuwaachia walimu mzigo wote wa malezi, tutakuwa tunasababisha kudorora kwa maadili na kuwalemea watu ambao tayari wamechoka na wana majukumu lukuki.
Walimu ni nguzo muhimu katika jamii, lakini si miujiza. Tuwaunge mkono kwa kuwasaidia kulea watoto wetu kwa kuwajibika kikamilifu kama wazazi.
Tuwapunguzie angalau mzigo huu wa malezi ambao kimsingi ni wetu. Tujenge familia imara, tuweke maadili mbele, na tushirikiane ili kuleta kizazi chenye maarifa na tabia njema. Malezi ni kazi ya moyo, na moyo huo unapaswa kuanzia nyumbani.
Katika mazingira ya sasa yanayobadilika kwa kasi, watoto wanakabiliwa na changamoto nyingi zaidi kuliko hapo awali. Teknolojia, mitandao ya kijamii, shinikizo la rika na mabadiliko ya kimaadili vinaathiri kwa kiasi kikubwa namna wanavyokua na kufikiri.
Ni vigumu kwa mwalimu peke yake kuyadhibiti yote haya ndani ya saa chache za darasani. Hapo ndipo jukumu la mzazi linapopaswa kuwa la msingi na endelevu, si la msimu wala la kulaumu pale mambo yanapoharibika.
Mzazi anayewajibika huanza kwa kuwa mfano bora. Watoto hujifunza zaidi kwa kuona kuliko kusikia. Kama tunataka waishi kwa nidhamu, heshima na bidii, ni lazima tuonyeshe hayo katika maisha yetu ya kila siku. Maneno matupu hayatoshi bila matendo yanayoendana nayo.
Zaidi ya hayo, tuwape watoto wetu muda. Muda wa kuzungumza nao, kuwasikiliza na kuelewa mahitaji yao ya kihisia. Katika dunia yenye pilikapilika, wazazi wengi wamejikuta wakibadilisha malezi kwa zawadi au pesa, wakisahau kuwa upendo na uwepo wa mzazi haviwezi kununuliwa.
Tukianza nyumbani, tutawapunguzia walimu mzigo mkubwa, na kwa pamoja tutajenga taifa lenye misingi imara ya maadili, elimu na uwajibikaji.