Wanaharakati wataka uchunguzi madai ya Teresia mbele ya Waziri Mkuu

Dar es Salaam. Muungano wa mashirika yanayotetea haki za wanawake na wasichana, Tanzania Dadas Rise Coalition (TDRC), umeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu upatikanaji wa haki kwa Teresia Teofili aliyeeleza kufanyiwa unyanyasaji wa kijinsia mbele ya hadhara na kuishia kuchekwa.

Muungano huo unaojumuisha viongozi vijana wanawake na wakurugenzi wa mashirika 48 yasiyo ya kiserikali nchini, umeeleza kuwa tukio hilo linaibua maswali kuhusu namna jamii na taasisi zinavyoshughulikia malalamiko yanayohusu ukatili wa kijinsia, huduma za afya na heshima ya utu wa binadamu.

Tukio hilo lilitokea Machi 3, 2026 wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika ziara ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba wilayani Mbulu huku Teresia akipewa fursa ya kuzungumza na kueleza masuala kadhaa aliyodai kufanyiwa.

Katika mkutano huo, Teresia alidai kuwa alijifungua mtoto katika hospitali ya wilaya bila kupata msaada wa kutosha wa kitabibu kutoka kwa daktari aliyekuwa akimhudumia, hali iliyosababisha kupoteza damu nyingi pamoja na kupata madhara makubwa ya kiafya.

Aidha, alieleza kuwa alipolalamikia huduma alizopata, alipuuzwa na kupewa jina la kuwa hana akili timamu na mhudumu wa afya, bila kufanyiwa uchunguzi rasmi wa kitabibu wa afya ya akili.

Mbali na hilo, alidai kuwa amekuwa akifanyiwa vitendo vya ubakaji mara kwa mara na vijana katika jamii yake na hata alipoenda kutoa taarifa kwa polisi, malalamiko yake hayakuchukuliwa kwa uzito unaostahili.

Teresia alidai pia baadhi ya mamlaka za eneo hilo zimekuwa zikimpa dawa na sindano bila kufanyiwa uchunguzi sahihi wa afya ya akili wala kutoa ridhaa yake, huku akidai kuwa, baba wa mtoto wake hajatoa msaada wa malezi.

Akizungumza leo Jumanne, Machi 10, 2026, mjumbe wa mtandao huo, Consolata Chikoti amesema masuala yaliyotolewa na Teresia yanahusisha tuhuma nzito, ikiwamo ukatili wa kijinsia, uzembe wa kitabibu, unyanyapaa wa afya ya akili na kutowajibika katika malezi ya mtoto.

“Masuala kama haya yanahitaji majibu yanayoonyesha uzito na unyeti wa hali ya manusura. Mwitikio wa hadhara unaoweza kuonekana kama wa kubeza unapojitokeza wakati mtu anatoa tuhuma za ukatili wa kijinsia unaweza kuendeleza unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya waathirika.

“Lakini tumeona baada ya ushuhuda huo, ilishuhudiwa kwamba baadhi ya watu waliokuwepo katika mkutano huo walicheka kabla ya kiongozi wa mkutano kuelekeza mamlaka za eneo hilo kushughulikia suala hilo.

Consolata amesema iwapo tuhuma hizo zitathibitishwa, zinaweza kuhusisha ukiukwaji wa sheria mbalimbali za Tanzania.

Kwa upande wake, Magdalena Gisse ambaye pia ni mjumbe wa TDRC, amesema vitendo vya ubakaji ni makosa ya jinai chini ya Kanuni ya Adhabu (Sura ya 16) pamoja na marekebisho yaliyofanywa kupitia Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA) ya mwaka 1998.

Aidha, madai ya kunyimwa huduma stahiki wakati wa kujifungua yanaweza kuibua maswali kuhusu uwezekano wa uzembe wa kitabibu, jambo ambalo linaweza kuchunguzwa chini ya Sheria ya Wataalamu wa Tiba, Meno na Afya Shirikishi ya mwaka 2017.

Kuhusu afya ya akili, Magdalena amesema madai ya kumtaja mtu kuwa hana akili timamu bila tathmini sahihi ya kitabibu pamoja na kumpa dawa bila ridhaa yanaweza kuwa kinyume na Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008, inayolinda haki na utu wa watu wenye changamoto za afya ya akili.

“Unapozungumzia kuwa madai ya baba wa mtoto kushindwa kutoa matunzo hiyo ni ukiukwaji Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, inayowataka wazazi kuwajibika katika malezi ya watoto wao.

“Aidha, iwapo madai kwamba malalamiko ya ubakaji hayakuchunguzwa ni ya kweli, hali hiyo inaweza kuathiri wajibu wa vyombo vya dola chini ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi, pamoja na misingi ya haki na usawa mbele ya sheria iliyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,” amesema Magdalena.

Kutokana na hali hiyo, mtandao huo umezitaka mamlaka husika kufanya uchunguzi huru, wa haraka na usio na upendeleo kuhusu tuhuma zilizotolewa na Teresia.

Pia, imeitaka Serikali kuhakikisha Teresia na mtoto wake wanapata huduma za haraka za kitabibu, msaada wa kisaikolojia na ulinzi unaostahili.

Aidha, muungano huo umeitaka mamlaka kufanya uchunguzi wa jinai dhidi ya watu wanaodaiwa kuhusika na vitendo vya ubakaji iwapo tuhuma hizo zitathibitishwa, pamoja na kufanya mapitio ya kitaaluma kuhusu madai ya kunyimwa huduma wakati wa kujifungua.

“Tunatoa wito kwa taasisi zote za umma kuzingatia utawala wa sheria na kuhakikisha kila mwananchi, hasa wale walio katika mazingira hatarishi, anatendewa kwa heshima, huruma na haki,” amesema Neema Abeid ambaye ni mjumbe wa mtandao huo.