Global Publishers
March 10, 2026
0 Comments
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Jumanne (Machi 10, 2026) amekagua miundombinu na utendaji kazi wa Bandari ya Kasanga iliyopo Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.
TPA ilifanya upanuzi wa bandari ya Kasanga mwaka 2019 kwa kuongeza urefu wa gati kutoka mita 20 hadi 120 ya kina cha mita 14 pamoja na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na jengo la kuhudumia abiria 200 kwa wakati mmoja kwa gharama ya shilingi bilioni 4.7. Pia kumejengwa maghala mawili ya kuhifadhi mizigo yenye uwezo wa tani 2,500 kila moja.

Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Desemba 2025, bandari hiyo imehudumia jumla ya tani 3,418 za mizigo, abiria 3,648, meli 11 pamoja na maboti 337. Miongoni mwa mizigo inayohudumiwa katika bandari hiyo ni saruji, makaa ya mawe pamoja na mazao ya chakula kama mahindi, mchele na unga wa sembe.
Bandari hiyo ni miongoni mwa miundombinu ya kimkakati inayochochea shughuli za usafirishaji na biashara katika ukanda wa Ziwa Tanganyika na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Rukwa na maeneo jirani. 