KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Hussein Ahmada Vuai amesema shirikisho hilo linaendelea na jitihada za kuleta mabadiliko katika Ligi Kuu Soka Zanzibar ili kutambulika zaidi Afrika.
Alisema mbali na ubora wa wachezaji, ligi hiyo inanufaika kwa kuboreshwa kwa miundombinu ya michezo na makocha wazoefu ambao wamewahi kufanya kazi kwenye baadhi ya klabu za Tanzania Bara.
Aliongeza, uwezekano wa ligi hiyo kukua na kupata umaarufu upo kwani kila msimu wanatoa wachezaji wenye vipaji kutoka Zanzibar huhamia Ligi Kuu Bara na wengi wao wanafanya vizuri.
“Kujitokeza mara kwa mara wachezaji wenye ubora kutoka Zanzibar kunaonyesha haja ya kuinua hadhi ya ligi hiyo na kuifanya ivutie zaidi kwa kutumia nafasi hii kukuza mafanikio na ushindani wake,” alisema
Alisema uongozi wa ZFF umejipanga kuanzisha utawala unaofanya kazi kwa weledi na uwazi katika shughuli zake zote.
Alifichua moja ya mipango hiyo shirikisho hilo kushirikiana na TSL kutafuta njia za kuongeza thamani ya soko la katika ligi hiyo.
Katika mpango huo, wataweka hadharani thamani ya ligi hiyo ili wadhamini waweze kuwekeza kwa kiasi kikubwa kuliko washirika wa sasa.
Aidha, alibainisha kuwa juhudi zinazoendelea za kuboresha miundombinu ya michezo zikiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi zinatoa fursa kwa shirikisho hilo kuanzisha mikakati ya kibunifu ya kuendeleza zaidi soka visiwani humo.