Ziara ya Kihongosi Kanda ya Ziwa daraja kati ya CCM na wananchi

Simiyu/Mwanza. Ziara ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mwanza imeanza kuvuta hisia za wadau wa siasa na wananchi, huku wengi wakiitazama kama daraja linaloweza kuimarisha uhusiano kati ya chama na wananchi.

Ziara hiyo ya kikazi, Kihongosi ameweka kipaumbele kusikiliza kero za wananchi, kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali na kufuatilia uhai wa chama katika ngazi za chini.

Ilianza mkoani Shinyanga kuanzia Machi 4 hadi 7, 2026, kabla ya kuendelea mkoani Simiyu na baadaye kuwasili Mwanza Machi 10, ambako pia amekutana na wananchi na viongozi mbalimbali.

Katika kila eneo alilopita, mikutano ya hadhara imekuwa jukwaa muhimu kwa wananchi kueleza changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku, huku chama kikionekana kujenga ukaribu zaidi na jamii kwa kusikiliza na kutoa maelekezo ya awali kuhusu utatuzi wa baadhi ya kero hizo.

Hali hiyo imeibua mjadala kuhusu iwapo ziara za aina hiyo zinaweza kuwa chombo madhubuti cha kusikiliza sauti za wananchi na kuchochea hatua za haraka katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamezungumzia ziara hiyo kwa mitazamo tofauti, wengi wakiona inaipa CCM fursa ya kukutana na wananchi ana kwa ana na kusikia malalamiko yao moja kwa moja.

Muonekano wa daraja Sukuma wilayani Magu.



Mwananchi imezungumza na Mhadhiri na mchambuzi wa siasa, Profesa Mohammed Makame ambaye amesema mikakati ya aina hiyo si mpya katika siasa za Tanzania, akirejea ziara zilizowahi kufanywa na Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Abdulrahman Kinana ambazo zilionekana kuwa na matokeo chanya.

Kwa mujibu wa Profesa Makame, ziara kama hizo zinakipa chama picha halisi ya hali ya maisha ya wananchi na changamoto wanazokabiliana nazo.

“Ni wazi wananchi wa kawaida wanapata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa chama wanachokiamini na kukipa ridhaa ya kuendesha serikali yao. Hali hii inasaidia chama kuimarisha uhusiano wake na wananchi,” amesema.

Kwa upande wake, mchambuzi mwingine wa siasa, Dk Richard Mbunda amesema kipindi cha sasa kinahitaji chama kuimarisha mawasiliano na wananchi kwa kutumia lugha inayojenga mshikamano na utulivu.

Amesema mikutano kama hiyo inapaswa kuendelea kufanyika kwa nguvu zaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku akisisitiza umuhimu wa ajenda za amani na mshikamano wa kitaifa katika mikutano hiyo.

“Huu ni wakati ambao chama kinapaswa kusaidia juhudi za Serikali kwa kuendelea kusikiliza wananchi na kuimarisha maelewano. Ziara kama hizi zikifanywa kwa upana zaidi zinaweza kuimarisha mawasiliano kati ya viongozi na wananchi,” amesema.

Hata hivyo, mchambuzi Ramadhan Manyenko ana mtazamo tofauti kidogo kuhusu namna ziara hizo zinavyopaswa kuendeshwa.

Amesema tija ya ziara hizo itaonekana zaidi endapo zitazingatia kutatua kero za wananchi badala ya kujikita katika mijadala ya vyama vya siasa.

“Nimezifuatilia ziara hizo. Kutatua kero za wananchi kuna tija kubwa, lakini kuzungumzia vyama vingine si jambo lenye umuhimu kwa sasa. Wananchi wanahitaji kusikia suluhisho la changamoto zao,” anasema.

Katika utekelezaji wa ziara hiyo, Kihongosi alianza mkoani Shinyanga katika Wilaya ya Kahama, kisha akaendelea wilayani Ushetu, Shinyanga Mjini na baadaye Kishapu.

Katika maeneo hayo, alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo daraja la Ubangwe lililokamilika katika Halmashauri ya Ushetu. Wananchi wa eneo hilo walisema ujenzi wa daraja hilo umekuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto iliyokuwa ikijitokeza kila msimu wa mvua, huku wakieleza kuwa hapo awali mafuriko yalikuwa yakisababisha ajali na hata vifo.

Mkoani Simiyu, wananchi wa wilaya ya Maswa waliibua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, wakisema baadhi ya maeneo bado yanategemea vyanzo vya maji visivyo salama.

Kero hiyo ilijirudia pia wilayani Itilima, ambako wananchi walieleza kuwa maji wanayotumia yana kiwango kikubwa cha chumvi na kuomba Serikali kuwasaidia kupata huduma ya maji safi.

Mbali na hilo, wananchi wa Itilima waliomba ukarabati wa barabara ambazo zimeharibika wakati wa msimu wa mvua, huku wakisema hali hiyo inatatiza shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao.

Katika Wilaya ya Bariadi Vijijini, wananchi walieleza changamoto ya tembo kuvamia mashamba yao na kuharibu mazao.

Akizungumzia suala hilo, Kihongosi alisema tayari amezungumza na Mbunge wa Bariadi Vijijini, Masanja Kadogosa na kwamba Serikali itapeleka teknolojia ya ndege nyuki (drones) ili kuwafukuza tembo katika maeneo yaliyoathirika na kulinda mazao ya wakulima pamoja na usalama wa wananchi.

Kuhusu changamoto za maji na barabara, aliwaelekeza viongozi wa wilaya na mkoa pamoja na taasisi zinazohusika kuhakikisha zinatafutiwa ufumbuzi ili wananchi waweze kunufaika na huduma hizo.

Mbali na kusikiliza changamoto za wananchi, ziara hiyo pia imehusisha ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali.

Mkoani Shinyanga, Kihongosi alikagua ujenzi wa bandari kavu pamoja na stendi mpya ya Mbulu wilayani Kahama.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, alikagua daraja la Ubangwe pamoja na mradi wa umeme wa REA uliopo katika Kata ya Kisuke unaoingiza megawati tano kwenye gridi ya Taifa.

Akiwa Shinyanga Mjini, alikagua ujenzi wa stendi mpya iliyofikia asilimia 35 ya utekelezaji na ujenzi wa uwanja wa ndege uliokamilika kwa asilimia 95, miradi yote ikiwa katika Kata ya Kizumbi.

Wilayani Maswa mkoani Simiyu, alikagua ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Shishiyu lililojengwa kwa gharama ya Sh160 milioni.

Katika wilaya hiyo pia alitembelea shamba darasa la pamba katika kijiji cha Mwatumbe, ambako wakulima wameanza kutumia teknolojia ya ndege nyuki kunyunyuzia dawa za kuua wadudu waharibifu.

Wakulima walieleza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yameongeza uzalishaji kutoka kilo 200 hadi kilo 1,000 kwa ekari moja, hali inayotarajiwa kuongeza kipato chao na kuimarisha kilimo cha pamba katika eneo hilo.

Kihongosi alisema matumizi ya teknolojia hiyo ni sehemu ya mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo wa kuongeza tija katika sekta ya kilimo na kuwainua wakulima kiuchumi.

Akiwa wilayani Itilima, alikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Mwamapalala kinachojengwa kwa fedha za Serikali kiasi cha Sh250 milioni pamoja na miradi mingine ya elimu na kilimo.

Wananchi wa eneo hilo walisema kwa muda mrefu wamekuwa wakilazimika kutembea zaidi ya kilomita 30 kufuata huduma za afya katika vituo vya Zagayu au Misheni, hali inayosababisha wagonjwa kuchelewa kupata matibabu na kuongeza gharama za usafiri.

Mkazi wa eneo hilo, Martha Petro alisema kukamilika kwa kituo hicho kutawasaidia hasa kina mama wajawazito kupata huduma kwa wakati na kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa kujifungua.

Kihongosi aliagiza kituo hicho kuanza kutoa huduma ifikapo Juni mwaka huu, akisema chama kimeridhika kwa asilimia 100 na maendeleo ya ujenzi wake na kinatarajia wananchi kuanza kunufaika na huduma hizo haraka.

Ziara hiyo ilihitimishwa katika wilaya ya Bariadi ambako alikagua ujenzi wa Soko Kuu la Wilaya unaogharimu Sh26.5 bilioni, fedha ambazo pia zinahusisha ujenzi wa barabara za kilomita 8.6 pamoja na ofisi, huku mradi huo ukiwa umefikia asilimia 25 ya utekelezaji.

Wananchi, hususan kina mama wafanyabiashara, walisema soko hilo litakapokamilika litawapa fursa kubwa za biashara, huku wakifurahishwa na uwepo wa chumba maalumu cha kunyonyeshea watoto.

Walisema kwa mara ya kwanza katika wilaya hiyo, soko linajengwa likiwa na eneo maalumu kwa ajili ya kina mama kunyonyesha watoto wao wachanga kwa faragha.

“Zamani tulilazimika kunyonyesha chini ya mti au kwenye vibanda vya muda, lakini soko hili jipya limetukumbuka sisi wazazi kwa kutenga chumba maalumu cha kunyonyeshea,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao.

Katika ziara hiyo, Kihongosi alisisitiza usawa katika ugawaji wa nafasi za biashara katika soko hilo, akiagiza wafanyabiashara wa zamani walioondolewa kupisha ujenzi kupewa kipaumbele pindi mradi utakapokamilika.

Aliwaeleza wananchi wa Simiyu kuwa Serikali itaendelea kusikiliza changamoto zao na kuzifanyia kazi, huku akisisitiza kuwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa inapaswa kuleta matokeo chanya katika maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa maeneo husika.

Akiwasili mkoani Mwanza, Kihongosi alianza ziara yake katika Wilaya ya Magu kwenye Kijiji cha Masanza Nsola ambako alipokelewa na mamia ya wananchi.