Dar es Salaam. Baada ya malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi kuhusu migogoro ya ardhi nchini, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amewataka viongozi na mawaziri wa kisekta kutafakari na kupendekeza mbinu itakayoleta suluhu ya kudumu.
Waliopewa jukumu hilo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Hamza Johari, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe.
Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, viongozi hao wanapaswa kukaa kwa dharura na kuja na mapendekezo yatakayomaliza migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka mingi.
Mtendaji mkuu huyo wa Serikali, ameyasema hayo leo Jumanne, Machi 10, 2026 wilayani Sumbawanga Mjini mkoani Rukwa, akiendelea na ziara yake mkoani humo.
Amesema Serikali haiwezi kuendelea kuvumilia hali inayosababisha wananchi kulalamika na kukosa haki katika umiliki wa ardhi.
“Nimuelekeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Ardhi na Waziri wa Tamisemi kaeni kwa dharura na wataalamu wenu mfanye tathmini kama tatizo hili ni la kisera, kisheria au kimuundo. Lazima tupate jawabu na tufute machozi ya wananchi,” amesema.
Katika maeneo mengine, amesema migogoro ya ardhi imekuwa chanzo cha malalamiko kutoka kwa wananchi, huku baadhi yao wakipoteza mali na haki zao kutokana na udhaifu uliopo katika mifumo ya usimamizi wa ardhi.
Waziri Mkuu, amesema Serikali inakusudia kupata mapendekezo yatakayowezesha kuchukuliwa hatua za haraka na za kudumu ili kurekebisha mfumo uliopo.
“Haiwezekani kila nilikopita kilio ni ardhi, karibu asilimia 98 ya kero kwenye maeneo yote niliyotembelea ni migogoro ya ardhi. Ardhi haiwezi kuongezeka, lakini watu wanaendelea kuongezeka. Hivyo lazima tuwe na mfumo ulio wazi na wa haki ili kila mmoja apate stahiki yake bila migogoro,” amesema.
Ameongeza, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa mawaziri na wataalamu wanaohusika, Serikali itakuja na utaratibu maalumu wa kumshauri Rais ili maelekezo yatolewe na utekelezaji wake uanze mara moja.
“Niwaahidi Watanzania kwamba tutakapopata taarifa kutoka kwa viongozi hawa tutakuja na utaratibu wa kumshauri Rais ili aelekeze utekelezwe mpango wa kukomesha mambo haya,” amesema.
Dk Mwigulu, amesema moja ya changamoto inayochochea migogoro hiyo ni kuwepo watu wanaotumia udhaifu wa mfumo wa ardhi kujipatia maeneo kwa njia zisizo halali.
Amesema katika baadhi ya maeneo kumekuwapo na utaratibu usio rasmi ambapo watu wanaotamani ardhi huanza kwa kumchunguza mmiliki halali na kupima uwezo wake wa kufuatilia haki yake.
“Hiki kimekuwa kama kichaka. Wanajua mtu atafuatilia halafu atachoka ataacha mwenyewe. Watu wakishalitamani eneo wanamuangalia mmiliki, wanampima uwezo wake wa kufuatilia halafu wanalichukua,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu ameeleza katika baadhi ya maeneo kumekuwa na tuhuma za watu kupanga hata bajeti za kushawishi wajumbe wa mabaraza ya ardhi ili kupata maamuzi yanayowawezesha kumiliki maeneo wanayotamani.
“Maeneo mengine wanaenda wanawahesabu kabisa wajumbe wa baraza la ardhi na kuwawekea bajeti. Hii ni hatari na haiwezi kuendelea kuvumiliwa,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali imeazimia kuanza upya katika namna ya kushughulikia masuala ya ardhi ili kuondoa mianya ya rushwa na udanganyifu inayochangia migogoro hiyo.
“Hii lazima tuanze upya na lazima tumalize haya,” amesisitiza.
Waziri Mkuu, amesema katika ziara na mikutano mbalimbali aliyofanya nchini, karibu kila eneo wananchi wamekuwa wakilalamikia masuala ya ardhi, hali inayoonyesha ukubwa wa tatizo hilo.
“Nimepita kila kona ya nchi, malalamiko makubwa ni ardhi. Wananchi wanalia kila mahali,” amesema.
Migogoro ya ardhi imekuwa miongoni mwa changamoto kubwa nchini, ikihusisha wakulima na wafugaji, wananchi na wawekezaji pamoja na migogoro ya mipaka ya maeneo ya makazi na hifadhi.
Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zikiwemo upimaji wa ardhi, utoaji wa hati miliki na kuimarisha mabaraza ya ardhi, hata hivyo malalamiko bado yanajitokeza katika maeneo kadhaa.