Athari za nchi wanachama kutoipa kipaumbele EAC

Dar es Salaam. Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), inasuasua kutokana na baadhi ya nchi wanachama kutoipa nafasi kubwa kama chombo chenye manufaa kwao katika masuala tofauti ikiwamo ya kiuchumi na kidiplomasia.

EAC inapoteza mvuto na nguvu ya ushawishi kwa wanachama wake na ni sahihi kusema wanachama wenyewe ndiyo wanaiua kutokana na kutoitunza na kuipa nafasi ya kuwa chombo cha kuimarisha uhusiano na ushirikiano miongoni mwao.

Katika mkutano wa wakuu wan chi uliofanyika hivi karibuni jijini Arusha, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo, akipokea kijiti kutoka kwa Rais wa Kenya, William Ruto.

Moja ya changamoto kubwa zinazoikabili jumuiya hiyo ni uhaba wa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za sekretarieti, Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki pamoja na shughuli za taasisi zake nyingine.

Baadhi ya nchi wanachama ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Sudan Kusini, Somalia na Burundi, hazichangii michango kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli zake, kwa mujibu wa mkataba wa uanzishwaji wa EAC.

Kukosekana kwa fedha hizo, kunasababisha kukwamisha shughuli za Jumuiya ikiwemo kulipa mishahara ya wafanyakazi wa sekretarieti, majaji na wabunge, kutekeleza maazimio yanayopitishwa na Bunge la Eala pamoja na kuandaa mikutano.

Changamoto nyingine ni nafasi ya EAC katika utatuzi wa migogoro baina ya nchi wanachama wake.

Kama inavyofahamika, DRC na Rwanda ziko kwenye mgogoro unaosababishwa na mapigano huko mashariki mwa DRC ambapo Rwanda inadaiwa kufadhili kikundi cha M23.

Kabla ya EAC kusuluhisha mzozo huo, viongozi wa Rwanda, Paul kagame na DRC, Felix Tshisekedi wamekuwa hawaiamini EAC katika utatuzi wa mgogoro huo, hivyo wanajielekeza katika wapatanishi wengine hasa nje ya Bara la Afrika.

Itakumbukwa kwamba Rais wa Angola, João Lourenço alikuwa mpatanishi kati ya viongozi hao, hata hivyo hakufanikiwa.

EAC iliitisha kikao cha dharura kwa njia ya mtandao, lakini Tshisekedi aliwakilishwa kwenye mkutano huo nyeti.

Kikao cha pili cha pamoja kilichofanyika Februari 8, 2025 jijini Dar es Salaam, kikihusisha EAC pamoja na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), viongozi hao wa Rwanda na DRC hawakuhudhuria, bali walituma wawakilishi.

Baada ya muda, Desemba 5, 2025, walionekana wakitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano mbele ya Rais wa Marekani, Donald Trump. Hata hivyo, mapigano bado yanaendelea katika eneo hilo.

DRC ni mwanachama wa Sadc, majukwaa ambayo yanaweza kutumika kumaliza mzozo baina ya mataifa hayo.

Hata hivyo, kutokana na kuipuuza EAC, wanakwenda kutafuta suluhisho katika majukwaa mengine ya kimataifa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Serikali Zanzibar (SUZA), Profesa Mohamed Makame amesema imekuwa kawaida kwa viongozi wa mataifa ya DRC na Rwanda kukwepana katika baadhi ya mikutano ya wakuu wa nchi wa Jumuiya hiyo.

“Imetokea mara kadhaa viongozi hawa wawili kukwepana katika vikao vinavyojumuisha wakuu wa nchi za Jumuiya hiyo. Akitokea mmoja, mwingine hatokei au hawatoki wote wawili,” amesema Profesa Makame.

Amesema sababu zinazotajwa zinaweza kuwa tofauti, lakini kiini chake ni mvutano wa usalama mashariki mwa Congo, tuhuma dhidi ya Rwanda kuunga mkono waasi wa M23 pamoja na tofauti za kidiplomasia kuhusu ushirikiano wa kikanda.

Profesa Makame ameongeza kuwa mara kadhaa Rais Kagame amekuwa akionyesha kutokuwa tayari kukutana ana kwa ana na Tshisekedi, akieleza kuwa mazungumzo hayo hayawezi kuwa na tija bila kupatikana kwa suluhisho la msingi kwa mgogoro huo.

Aidha, amesema wakati DRC ilipojiunga na EAC, Rais Tshisekedi alitarajia kuona msaada mkubwa wa kikanda katika kukabiliana na changamoto za usalama, lakini mvutano uliopo umeendelea kuathiri matarajio hayo.

Wataalamu pia wanasema tofauti kati ya viongozi hao si za kisiasa pekee bali zinaonekana kuwa na sura ya mvutano wa kibinafsi unaochangia ugumu wa kufanikisha mazungumzo ya moja kwa moja.

“Bado ipo haja kwa EAC kuendeleza mazungumzo ya upatanishi ili kuimarisha uhusiano na mshikamano wa kisiasa ndani ya Jumuiya,” anasisitiza mchambuzi huyo wa masuala ya siasa na diplomasia.

Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema changamoto nyingine ni mipaka ya mamlaka ya EAC katika kushughulikia masuala ya ndani ya nchi wanachama.

Anasema kwa kuwa jumuiya hiyo haina nguvu ya moja kwa moja ya kuamua masuala ya ndani ya nchi wanachama, hali hiyo inaweza kuifanya ishindwe kusukuma kwa nguvu suluhu ya mgogoro huo.

“Tatizo kubwa ni kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki haina mamlaka ya kuamua mambo ya ndani ya nchi mwanachama, hivyo mgogoro unaweza kuendelea iwapo hakutakuwa na dhamira ya kisiasa kutoka pande zote,” anasema.

Kuhusu masuala ya kifedha, mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Salim Ahmed Salim, Denis Konga anasema bila nchi wanachama kujizatiti katika ulipaji wa michango, jumuiya hiyo itapoteza mwelekeo na hatimaye kuvunjika kwa mara nyingine.

Anasema jumuiya ya awali iliyovunjika mwaka 1977, ilivunjika kwa sababu mbalimbali ikiwamo tofauti za kimtazamo baina ya viongozi wa nchi wanachama na sasa ukata unaweza kuwa sababu nyingine katika hilo. “Suala la fedha za uendeshaji ni muhimu sana, bila hivyo mambo yatakuwa yanajadiliwa lakini hayatekelezwi kama inavyotakiwa.

Tukifika huko basi hatutakuwa na hii jumuiya, tunahitaji viongozi watakaotimiza wajibu wao na kukiona chombo hiki kama kitu muhimu kwao,” amesema.

Anaongeza kuwa kumalizika kwa mzozo wa mashariki mwa DRC kunahitaji utashi wa kisiasa wa viongozi wa Rwanda na DRC kwa sababu wao ndiyo wana sauti kwa vikosi kwa wapiganaji katika eneo zima la mashariki ya Congo, hivyo watawasikiliza na kusitisha mapigano. Viongozi hawa wana nafasi ya kipekee ya kushawishi pande zinazohusika kwa sababu sauti zao zina uzito mkubwa kwa makundi ya wapiganaji yanayofanya shughuli zake katika eneo hilo.

Ikiwa watatumia mamlaka na ushawishi wao kwa dhamira ya dhati ya kutafuta amani, wana uwezo wa kuyahimiza makundi hayo kusitisha mapigano na kuanza njia ya mazungumzo ya kudumu. Hatua hiyo inaweza kuwa mwanzo wa kurejesha utulivu, usalama na maendeleo kwa wananchi wa mashariki mwa Congo ambao kwa muda mrefu wameathiriwa na migogoro ya silaha.