Dar es Salaam. Wakati msuguano ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Moshi Mjini ukiendelea kushika kasi ikiwamo viongozi 70 kusaini barua ya kutokuwa na imani na kigogo wa chama hicho ngazi ya wilaya, Mkoa wa Kilimanjaro umesema inafanyia kazi madai yote na hatua zitachukuliwa.
Taarifa za uhakika zilizolifikia Mwananchi, zinaeleza miongoni mwa waliosaini barua hiyo iliyotumwa kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro ni madiwani na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho wilaya ya kichama ya Moshi Mjini.
Baadhi ya waliosaini barua hiyo wanadai kutishwa na kuelezwa watakutana na rungu kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho mwakani.
Mwenyekiti CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema wanafanyia kazi madai yote yanayotolewa.
Wajumbe hao wanamtuhumu kiongozi huyo kwa kutengeneza majungu na kufitinisha viongozi wenzake jambo linalosababisha mpasuko na kugawa wanachama na viongozi.
Ujumbe wa kiongozi huyo (jina linahifadhiwa kwa sasa) aliouweka kimakosa katika ukurasa wake wa WhatsApp Jumapili ya Februari 22,2026 akitamba kumshughulikia Meya Zuberi Kidumo na Mkurugenzi wa Manispaa, Mwajuma Nasombe umekoleza moto huo.
Katika ujumbe huo ambao aliufuta baadaye ulikuwa unasomeka: “Hii ndio habari ya mjini kaeni mkao wa kula. Tumeshawasha taa nyekundu, hatutabakisha mtu, tunawatoa wote,” unasomeka ujumbe huo uliosambaa mitandao ya kijamii.
Wanadai kwa kuwa jambo hilo ni zito na linaleta mpasuko na mgawanyiko kwa wanaCCM na linavunja mahusiano mema kati ya CCM na Serikali, wameamua kukijulisha chama kuwa kiongozi huyo anakivuruga chama hicho na kukishushia hadhi.
Kwa mujibu wa andiko hilo, wanadai kiongozi huyo ameonesha wazi hamuungi mkono meya na mkurugenzi wa manispaa na kushindwa kuwaunganisha wanachama na viongozi kwa madai ya kuendekeza majungu na mpasuko.
Machi 9, 2026, wajumbe wote waliosaini andiko hilo walitakiwa kufika mbele ya sekratarieti ya CCM mkoa ili kuhojiwa juu ya malalamiko yao, lakini waliofika walikuwa watatu pekee.
Waliosaini andiko hilo la Februari 23, 2026 ambalo ndio kiini cha purukushani zilizoibuka katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa Kilimanjaro iliyoketi Machi 7, 2026, walitaka suala hilo lijadiliwe kwanza kabla ya kuanza kikao.
Jumanne, Machi 10, 2026 kulifanyika kikao cha kamati ya siasa Mkoa wa Kilimanjaro kilichoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho mkoa, Boisafi. Pamoja na mambo mengine kilijadili msuguano huo unaoendelea.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Boisafi amesema CCM ina utaratibu katika kufanya mambo yake, hivyo sio kila kinachotokea hatua zinachukuliwa papo hapo, bali unafanyika uchambuzi na kuzisikiliza pande zote.
“Kwenye chama chetu kuna utaratibu, sio kila kitu kinachotokea unachukua hatua hapohapo, lazima uchambue kisha uchukue hatua,” amesema.
Boisafi amesema kikao hicho hakijalimaliza jambo hilo, wanatarajia kuendelea nalo hadi Ijumaa ya Machi 13, 2026 kisha atakuwa na cha kuzungumza kuhusu hatua stahiki.
“Tunaendelea nalo hadi Ijumaa huenda tukawa na la kusema, lazima tuwasikilize bila kusema nani mwenye haki kisha tukipata jawabu tutajua kinachofuata,” amesema.
Kuhusu madai ya kutishwa kwa baadhi ya madiwani walioandika pingamizi hilo, Baisafi amesema hana taarifa hizo na kama zingekuwepo zimefikishwa kwake au kwa Katibu wa CCM Mkoa.
Baadhi ya wajumbe waliosaini barua hiyo wakizungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina wamedai baada ya kusaini barua hiyo waliitwa na baadhi ya viongozi wa CCM kujiridhisha kama kweli walisaini bila kushinikizwa na walipothibitisha hilo, walitishwa uchaguzi wa ndani ya chama 2027, majina yao hayatarudi.
“Wengi walieleza hawakulazimishwa, bali walifanya hivyo kwa hiari kutokana na kile walichodai ni mwenendo usioridhisha (anamtaja kigogo huyo), ikiwamo madai ya kuendesha makundi ndani ya chama,” amedai.
Aidha, amedai baadhi ya walioitwa walilalamika kutishiwa hatua yao ya kusaini barua hiyo inaweza kuwaathiri kisiasa, ikiwamo kudaiwa huenda wasiruhusiwe kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ifikapo mwaka 2027.
Ameeleza vitisho hivyo vilitolewa wakati wa mahojiano yaliyofanywa na baadhi ya viongozi wa chama ngazi ya wilaya na sekretarieti ya mkoa.
“Jana (juzi) baadhi ya madiwani wameitwa, makatibu na baadhi ya waenezi lakini hoja ni kwamba walikuwa wanaulizwa kama kuna watu wamewalazimisha kusaini lakini kila mmoja alijieleza kwamba amesaini kwasababu mwenendo wa (kiongozi huyo) sio mzuri,” amedai mjumbe mwingine.
Mwingine amesema: “Jana (juzi) nilizungumza na watu watatu ambao waliitwa lakini walikuwa wanalalamika wanatishwa kwamba ni kwanini wasaini na nani aliwaambia wasaini, na kuambiwa huwatagombea 2027 na watakata majina yao na wataweka timu zetu ambao watawasikiliza.”