Dar es Salaam. China imeeleza nia ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza maendeleo ya viwanda, hususan katika uzalishaji, uhamishaji wa teknolojia na maendeleo ya ujuzi.
Akizungumza Machi 11, 2026 wakati wa ziara katika kiwanda cha kuunganisha malori ya Howo kinachomilikiwa na Saturn Corporation Limited kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian amesema nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo yanayolenga kuunga mkono ajenda ya Taifa ya uendelezaji wa viwanda.
Katika ziara hiyo, balozi huyo alitembelea kiwanda hicho kufuatia mwaliko wa uongozi wa Saturn Corporation, inayomiliki kituo cha kuunganisha malori ya Sinotruk nchini Tanzania. Kampuni hiyo ni miongoni mwa wasambazaji wa malori ya chapa hiyo kutoka China, yakiwemo malori ya kumwaga mizigo (tippers), malori ya kuvuta mizigo (tractor trucks) pamoja na vipuri.
Mkurugenzi wa kiwanda cha Saturn Corporation, Chirag Tanna (wa pili kulia), akifafanua kuhusu shughuli mbalimbali za kampuni hiyo kwa Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian (katikati) wakati wa ziara ya balozi huyo katika kiwanda hicho kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Chen amesema China na Tanzania zimeingia katika makubaliano yanayolenga kuunga mkono maendeleo ya viwanda barani Afrika, huku Tanzania ikitajwa kuwa miongoni mwa washirika katika utekelezaji wa mipango hiyo.
Pia amegusia umuhimu wa ushirikiano katika kukuza ujuzi kwa vijana kupitia taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET), akisema China itaendelea kuunga mkono mipango inayolenga kuwajengea Watanzania uwezo wa kiufundi unaohitajika katika sekta ya viwanda.
Saturn Corporation ilianzishwa mwaka 2021 ikiwa na lengo la kusaidia sekta ya usafiri na usafirishaji wa mizigo nchini kwa kutoa malori mazito pamoja na huduma za matengenezo na vipuri.
Kiwanda cha kuunganisha malori cha Kigamboni kilizinduliwa rasmi Mei 2024 na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na ni miongoni mwa vituo vinavyounganisha malori katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa Saturn Corporation, Mehul Sachdev amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuunganisha hadi malori ya kuvuta mizigo 22 kwa siku, sawa na takribani malori 536 kwa mwezi.
Amesema shughuli za kiwanda hicho zinahusisha pia ushirikiano na kampuni ya Sinotruk International katika masuala ya uhandisi na uzalishaji wa malori.
Kwa sasa kampuni hiyo imetoa ajira kwa zaidi ya Watanzania 330 wakiwemo mafundi, wahandisi na wafanyakazi wa huduma mbalimbali. Watu wengine pia wananufaika kwa njia zisizo za moja kwa moja kupitia huduma za usafirishaji, usambazaji wa vipuri na shughuli nyingine za ugavi.
Saturn Corporation inatarajia kufikia uzalishaji wa jumla wa malori mazito 10,000 ifikapo mwaka 2027. Hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa malori kwa sekta za usafiri na usafirishaji wa mizigo pamoja na kuchangia maendeleo ya viwanda nchini.