Dickson Job mambo magumu Yanga, daktari afafanua

UNAWEZA kusema nahodha msaidizi wa Yanga, Dickson Job, ni kama ameumaliza msimu kutokana na jeraha la goti alilopata huku taarifa zikibainisha, hadi kupona kwake na kurejea uwanjani akiwa fiti, itamchukua miezi miwili hadi mitatu.

Kukaa kwake nje muda mrefu kunatokana na taarifa zilizobainishwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa goti.

Msimu huu wa Ligi Kuu Bara utakaofikia tamati Juni 18, 2026, maana yake Job akikaa nje kwa miezi mitatu, basi atakuwa fiti wakati ligi imemalizika, lakini ikiwa pungufu ya hapo, atawahi mechi za mwisho kumalizia msimu ikiwamo fainali ya Kombe la FA itakayochezwa Juni 21, 2026 endapo Yanga itafika hatua hiyo.

Lakini wakati kukiwa na taarifa hizo mbaya kutoka kwa Job, mashabiki wa Yanga wanashusha presha baada ya kuthibitika, kiungo mshambuliaji wa kikosi hicho, Pacome Zouzoua kwa sasa yupo fiti baada ya kupona bega.

Taarifa kutoka Yanga ni, Job wakati wowote kuanzia sasa anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa goti, matibabu yatakayofanyika Afrika Kusini ambako Yanga ilimsafirisha kwa ajili ya hatua hiyo ya kumaliza maumivu yake.

Job aliumia kipindi cha kwanza kwenye mechi ya Kariakoo Dabi dhidi ya Simba iliyochezwa Machi Mosi 2026, baada ya kugongwa na kiungo wa Simba, Inno Loemba wakati wakiwania mpira, kisha kushindwa kuendelea na mechi hiyo, akatolewa.

Taarifa za awali kutoka Afrika Kusini ni, Job atakuwa nje kwa miezi miwili mpaka mitatu akiuguza jeraha hilo, ikiwa ni majeraha ya kwanza makubwa tangu asajiliwe na timu hiyo aliyojiunga nayo Januari 11, 2021 akitokea Mtibwa Sugar.

Taarifa zaidi zilisema, kuna uwezekano mkubwa kwa Job kuukosa msimu huu endapo Ligi Kuu Bara itamalizika Juni 18, 2026 kama ambavyo ratiba ya sasa inavyoonyesha, hivyo litakuwa ni pigo kwa Yanga kumkosa mlinzi huyo tegemeo.

Baada ya kuumia bega, Pacome alikuwa nje ya uwanja akiuguza jeraha hilo na kukosa mechi tano zikiwemo nne za Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo, JKT Tanzania, Simba, Singida Black Stars na moja ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Polisi Tanzania.

Hata hivyo, taarifa kutoka benchi la ufundi la Yanga ni, kiungo huyo wakati wowote anaweza kuwa sehemu ya timu hiyo kwenye mechi zijazo kuanzia ya kesho dhidi ya Tanzania Prisons itakayopigwa Machi 12, 2026 na ile dhidi ya Azam, Machi 15, 2026.

Iko hivi; taarifa ziliambia Mwanaspoti, Pacome ameshusha presha kwa viongozi na hata mashabiki baada ya kuonyesha anaweza kurudi uwanjani haraka hata kwenye mchezo ujao dhidi ya Prisons au Azam FC.

Pacome aliumia bega kwenye mechi ya mwisho hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie ya Algeria iliyochezwa Februari 15, 2026 pale Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar akichezewa vibaya na kipa Seif Benrabah dakika ya 39, wakati akiitengenezea Yanga penalti iliyozaa bao la kwanza.Kwenye mechi hiyo Yanga ilishinda mabao 3-0.

“Pacome maendeleo yake ni mazuri, hizi mechi mbili zijazo tunaweza kumuona, kilichokuwa kinaepukwa ni kumharakisha kupona ili yasitokee kama yaliyotokea kwa Clement Mzize, tulitaka apone sawasawa,” alisema mtaalamu huyo aliyeko kwenye benchi la ufundi la Yanga.

“Tulikuwa tunaangalia kupona kwake kwanza, sasa ni uamuzi wa kocha kama atataka kumtumia kwenye mchezo upi hapo mbele, lakini hakuna tishio kwamba anaweza kukaa nje kwa muda mrefu kama ambavyo ilielezwa awali.”

Akizungumza na Mwanaspoti, Dokta Samweli Shita, alisema jeraha la goti (knee injury) ambalo linamsumbua Job, linaweza kumfanya mchezaji akae nje kwa muda tofauti kutegemea ukubwa wake na eneo lililoathirika.

“Jeraha dogo (Minor sprain/strain), hapa ni misuli au mishipa (ligaments) inakuwa imevutika au kupata maumivu bila kupasuka. Muda wa kuwa nje unaweza kuwa wiki 1–3.

“Jeraha la kati (Moderate ligament injury/meniscus tear ndogo), hapa mishipa kama meniscus inachanika. Muda wa kuwa nje ni wiki 4–8 (mwezi 1 hadi 2).

“Jeraha kubwa (ACL tear, meniscus tear kubwa, fracture), hapa mishipa mikubwa kama ACL (Anterior Cruciate Ligament) au PCL ikipasuka, au kukatika kwa cartilage. Muda wa kuwa nje huwa unategemea kama utafanyiwa upasuaji, basi ni kuanzia miezi 3–6,” alisema daktari huyo.

Yanga baada ya kesho Alhamisi kucheza dhidi ya Tanzania Prisons, itapambana na Azam katika Dar es Salaam Dabi itakayochezwa Machi 15, 2026, saa 1:30 usiku kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar.

Timu hizo hadi sasa ndiyo pekee katika Ligi Kuu Bara hazijapoteza mechi zikishuka dimbani mara 12 kila moja. Yanga inaongoza msimamo wa ligi ikikusanya pointi 32, wakati Azam ni ya tatu na pointi 24.