Kihongosi Akagua Mradi wa Soko la Milioni 577 Buchosa

Global Publishers
March 11, 2026
0 Comments

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Cha Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi akiongea jambo akiwa na Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo (Mwenye shati la Kitenge).

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Cha Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi amesema uwekezaji katika miundombinu ya masoko ni muhimu kwa sababu unasaidia kukuza shughuli za kiuchumi za wananchi na kuongeza mapato ya Halmashauri ambayo yanatumika kuleta maendeleo nchini.

Kihongosi ameeleza hayo leo Machi 11,2026 alipokagua mradi wa ujenzi wa maduka 60 na vizimba 69 uliopo katika soko la Bukokwa Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza ambao unagharimu zaidi ya Sh milioni 577 na tayari umeanza kufanya kazi.

Akizungumza baada ya kukagua soko hilo Kihongosi amesema mradi huo utasaidia kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri pamoja na kuboresha mazingira ya biashara kwa wananchi.


Akifafanua kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia kuboresha miundombinu ya biashara na kuongeza vyanzo vya mapato kwa halmashauri.

“Tumejionea kazi nzuri iliyofanyika hapa, soko hili litasaidia wajasiriamali kufanya biashara katika mazingira bora na wakati huohuo halmashauri kupata mapato yatakayosaidia kutekeleza miradi mingine ya maendeleo,” amesema Kihongosi.

Ameongeza miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ni matokeo ya sera na mipango ya serikali chini ya uongozi wa Rais dkt. Samia Suluhu Hassan, inayolenga kuboresha huduma za kijamii na kukuza uchumi wa wananchi.

Amesema kuwa serikali imekuwa ikizihamasisha halmashauri kote nchini kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ili fedha hizo ziweze kutumika kuleta maendeleo kwa wananchi na ndicho kilichofanyika katika Halmashauri ya Buchosa.