Kipa Mlandege aja na mawili ZPL

KIPA wa Mlandege ambayo ni bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, Hamad Ubwa ‘Baro’ amesema ana kibarua cha kutetea ubingwa na timu hiyo na kuwa kipa bora wa msimu.

Pia, Baro amesema ana mkakati wa kuhakikisha anakuwa kipa bora kwenye msimu huu wa 2025-2026.

Matumaini ya Mlandege kutetea ubingwa huo yapo katika mechi 10 zilizobaki ambapo Baro alisema mechi tano zijazo zitawapa muelekeo mzuri wa timu hiyo na atahakikisha anasimama vizuri bila kupoteza.

“Kwasasa tupo nyuma kwa alama saba na kinara wa ligi Fufuni mwenye pointi 38 huku Mlandege tukiwa nafasi ya saba tukivuna pointi 31, bado tuna matumaini baada ya michezo mitano kati ya kumi iliyobaki itatupa dira,” alisema.

Kati ya michezo 16 aliyocheza Baro msimu huu, amefungwa mabao tisa, huku michezo 11 amecheza bila kuruhusu bao na kumfanya kuwa na cleansheet 11. Baro alisema, msimu huu anaona kiwango chake kimeongezeka zaidi kwani anajitahidi kufuata maelekezo ya kocha wake na kufanya mazoezi binafsi.

Akizungumzia msimu huu, Baro alisema umekuwa bora kutokana na ushindani uliopo ndani na nje ya uwanja lakini anaamini baada ya Mwezi mtukufu wa Ramadhan kumalizika, watarudi wakiwa imara zaidi. Ameliambia Mwanaspoti kuwa, anatamani kuchukua tuzo ya kipa bora wa msimu na anaamini hilo litatimia na timu hiyo itachukua ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo.

Kwa sasa, Ligi Kuu Zanzibar imesimama kupisha Mfungo wa Mwezi Mtufuku wa Ramadhan ambapo inatarajiwa kuendelea Machi 28, 2026.