Kwa hali hii matumizi ya gesi yetu hayaepukiki

Niliwahi kuulizwa na rafiki wa Kijerumani: “kinywaji chenu asilia ni kipi? Tulikuwa katika mapumziko nje ya Motel Agip. Ili kumjibu haraka nilimuita muuza madafu. “Mchongee moja laini huyu mgeni wangu.” Muuza madafu alitomasa bidhaa zake, akauliza, “maji au nyama?” Nilimwambia maji maana mgeni huyu hakuuliza chakula, bali kinywaji. Akachongewa dafu na kuyafurahia maji yake.

Wakati akiendelea na ladha ya dafu aliniuliza tena: “Je, mmeliingiza kiwandani kuona kama mnaweza kukuza biashara yake?” Kwa maringo na kujihami nilimjibu kuwa sisi tunakula vitu asilia kutoka shamba.

Ni vitu vichache tunavyoingiza kiwandani na kusafirisha kama chakula. Alionekana kuridhika. Baada ya muda tuliingia Hotelini kwa chakula cha mchana. Mgeni aliagiza soda ya Kijerumani iliyoandikwa Schweppes, mimi nikaulizia Fahari ilimradi nitoe sare.

Nilitaka kumuonesha kuwa hata sisi tuna vinywaji vyetu. Lakini nilizodolewa kwa jibu “mbona soda hiyo ilishaacha kuzalishwa miaka mingi sasa!” Potelea mbali nikaagiza soda ya Kimarekani. Nilianza kuona aibu maana mpaka kufika hapo Motel Agip, tulitumia gari yake ya Kijerumani, Volkswagen Audi.

Tulipoteremka alichomoa pakiti ya sigara ya Reemtsma Imperior na kibiriti cha Erdgas. Alionekana kujali zaidi bidhaa zao kuliko za nchi nyingine.

Nikafikiria mbali. Kwa sasa kuna tishio la upungufu wa mafuta kutokana na vita huko Mashariki ya Kati.

Hawa wageni wangetuheshimu sana kwa matumizi ya gesi asilia inayotoka na kuzalishwa nchini mwetu. Kwanza tusingewababaikia na nishati zao, halafu tungewalazimisha wao kuagiza gesi yetu maana si wote waliobarikiwa kuwa nayo.

Pia tungekuwa na uhakika wa viwanda vingi vinavyotumia nishati safi na salama.

Tanzania isingekuwa na tatizo la ajira kwa vijana kutokana na uwepo wa viwanda vingi nchini.

Lakini pia tungekuwa wa mwanzo kupiga hatua kubwa katika uhifadhi wa mazingira. Tunachokihitaji hapa ni uthubutu na kujiamini kuwa na sisi tunaweza. Kule Uarabuni wapo watu wa mataifa ya Ulaya na Marekani walioajiriwa kutumikia uchimbaji, usafishaji na usambazaji wa bidhaa zitokanazo na mafuta.

Watanzania na Waafrika kwa ujumla wamefundishwa kutokujiamini. Wana kila raslimali inayoweza kuwafanya wategemewe na wageni, lakini kinyume chake wao wapo tayari kuwategemea wageni kwa raslimali hizo. Tuna maeneo makubwa ya kilimo lakini yameshikwa na wawekezaji wageni. Siku tunapopatwa na janga la njaa, tunathubutu kuagiza chakula kutoka kwa wawekezaji hao.

Hivi tunavyozungumza, tayari bei ya mafuta imeshapanda. Mpaka leo bado tunahisi kuwa njia ya kulikabili tatizo hilo, ni kuhifadhi mafuta kwa kupunguza matumizi yake. Mimi nahisi kuwa hili si suluhisho la moja kwa moja kwani kwa upande mwingine, kupunguza matumizi ni kupunguza pato la Taifa linalotokana na kodi ya mafuta. Fisi alipunguza kula hadi chakula kikamwishia. Mwishowe akaamua kujila mwenyewe!

Wazo langu ni kuwekeza zaidi kwenye gesi asilia. Inaonesha kuwa hapa nchini tuna gesi nyingi kuliko tunavyohisi. Kuna mahala wananchi wa kawaida wamekuwa wakiripoti dalili za kuashiria uwepo wa gesi asilia.

Tukiwa na visima vingi vipya tukichanganya na vile vilivyokwisha kutangazwa, hatutalazimika kuumiza vichwa sana pale vita zinapoibuka kule kwa wasambaza nishati. Nadhani hii inaweza kuwa njia bora zaidi ya kuondokana na utegemezi wa mafuta.

Njia nyingine ni kuruhusu mashirika binafsi yafanye uatafiti wa vyanzo vya mafuta hapahapa nchini. Kuna kipindi TPDC walianza kushughulikia jambo hilo mkoani Singida.

Inasemekana katika maeneo yale kuna dalili za zao hilo. Pia upo mwamba unaofanana sana na miamba ya mafuta iliyopo Mashariki ya Kati. Inawezekana utafiti wa TPDC usiende haraka kwa sababu Serikali ina mambo mengi ya kufuatilia.

Hii ndiyo maana hasa ya kutumia raslimali zetu kwa faida yetu. Waarabu wanaitumia vema raslimali yao, mafuta ndio msingi wa uchumi wao. Dunia inatazama kupanda na kushuka kwa thamani ya fedha kwa kuzingatia uzalishaji wa mafuta.

Waarabu waliweka tahadhari kubwa katika mikataba yao ya usambazaji wa bidhaa hiyo nje ya mataifa yao. Hivi sasa dunia nzima itaathirika iwapo milango ya mafuta itafungwa.

Sisi bado hatujachelewa. Hata kama pale mwanzoni tulilegeza masharti ya gesi, bado kuna gesi inayochomoza hadi kwenye mito. Kuna mahala (kama sikosei Mtwara) watu wamekuta moto ukiwaka juu ya maji.

Huko kwenye hifadhi za misitu kila siku tumekuwa tukilaumiana kwa mioto inayozuka mara kwa mara. Mara nyingi wakazi wa maeneo hayo wameshutumiwa bure, lakini kumbe chanzo ni gesi asilia.

Na hakuna ubishi kwamba katika dunia tunayoishi leo, gesi ndiyo suluhisho ka kudumu katika matatizo yetu. Katika malengo ya kupunguza uchafuzi wa hewa, tunaona magari na mitambo vikibadilishiwa uelekeo na kutumia gesi badala ya mafuta.

Ni jambo la wazi kuwa gesi ina mahitaji makubwa sana katika uchumi wa kisasa. Serikali iliangalie hilo kwa macho makubwa. Tusikubali “mikataba-umiza” iturudishe nyuma tena. Pengine hii ndiyo turufu ya mwisho itakayofunga kizazi chetu.