Dar es Salaam. Wakati kesho Alhamisi, Machi 12, 2026 ikiwa ni siku ya figo duniani, wataalamu wa afya nchini wameonya mtindo wa maisha unaohusisha matumizi makubwa ya soda, vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) na vilevi, huku watu wakipunguza unywaji wa maji ya kutosha, unaongeza hatari ya kupata magonjwa ya figo.
Kwa mujibu wa wataalamu, tofauti na zamani ambapo matatizo ya figo yalionekana zaidi kwa wazee, sasa yanaanza kuonekana kwa vijana kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha.
Huku takwimu zikionyesha wagonjwa wanaopata huduma ya kusafisha damu imeongezeka kutoka 1,017 mwaka 2019 hadi kufikia 3,342 mwaka 2026.
Mkuu wa Kitengo cha Figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dodoma, Dk Kessy Shija, amesema unywaji wa maji angalau lita mbili hadi tatu kwa siku ni hatua muhimu ya kulinda afya ya figo kwa mtu ambaye hana tatizo lolote la figo.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne Machi 10, 2026, Dk Shija amesema maji husaidia mwili kutoa takamwili kupitia mkojo, jambo linalosaidia kuzuia maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI), mawe kwenye kibofu pamoja na madhara mengine yanayoweza kuathiri figo.
“Maji yanasaidia kutoa uchafu mwilini kwa njia ya mkojo. Kiwango cha maji kinapokuwa kidogo mwilini, uchafu huo unaweza kujikusanya na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo mawe kwenye kibofu au figo,” amesema.
Amesema pamoja na maji kuwa muhimu kwa mwili, watu wengi wamekuwa wakitegemea zaidi vinywaji laini kama soda au juisi wakiamini vinaweza kuchukua nafasi ya maji, jambo ambalo si sahihi kiafya.
“Watu wengi wanapohisi kiu huomba soda baridi wakiamini itawasaidia, wakati kimsingi vinywaji vingi vina sukari nyingi na haviwezi kuchukua nafasi ya maji mwilini,” amesema.
Kwa mujibu wa daktari huyo, matumizi makubwa ya vinywaji vyenye sukari yanaweza kuchochea matatizo mengine ya kiafya kama uzito kupita kiasi, kisukari na shinikizo la damu, ambayo pia ni miongoni mwa sababu kuu zinazosababisha magonjwa ya figo.
“Sukari ikizidi mwilini inaweza kuleta uzito kupita kiasi na kusababisha magonjwa kama kisukari na presha. Magonjwa hayo huathiri mishipa ya damu na hatimaye figo,” amesema.
Dalili za awali za figo kufeli
Dk Shija amesema tatizo la figo mara nyingi halionyeshi dalili katika hatua za mwanzo, hali inayofanya watu wengi kugundua wakiwa tayari katika hatua za mwisho za ugonjwa.
Amesema figo zinaposhindwa kufanya kazi yake ya kuchuja na kutoa takamwili mwilini, taka hizo huanza kujikusanya na kuwa sumu kwa mwili.
“Dalili zinaanza kuonekana zaidi kuanzia hatua ya tatu hadi ya tano. Mgonjwa anaweza kupata kichefuchefu, kutapika, kupoteza hamu ya kula au kupata vidonda vya tumbo,” amesema.
Kwa mujibu wa daktari huyo, takamwili zinapoongezeka mwilini zinaweza pia kuathiri mfumo wa fahamu ambapo mgonjwa anaweza kuanza kuchanganyikiwa au kupoteza kumbukumbu.
Ameongeza dalili nyingine ni pamoja na kuwashwa kwa ngozi, upungufu wa damu kutokana na figo kushindwa kuzalisha kichocheo kinachosaidia utengenezaji wa damu, pamoja na mifupa kuwa dhaifu kutokana na upungufu wa madini ya calcium.
“Wagonjwa wengine huanza kuvimba mwili kutokana na maji kushindwa kutoka mwilini. Maji yanaweza kukusanyika usoni, miguuni na hatimaye mwili mzima,” amesema.
Hata hivyo amesema wagonjwa waliofikia hatua ya tano ya ugonjwa wa figo hushauriwa kupunguza unywaji wa maji ili kuepuka maji kujikusanya mwilini na kuathiri mapafu.
Vijana nao waanza kuathirika
Dk Shija amesema tofauti na zamani ambapo matatizo ya figo yalionekana zaidi kwa wazee, sasa yanaanza kuonekana kwa vijana kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha.
“Tunapokea wagonjwa wengi wenye umri kati ya miaka 35 hadi 55. Huko nyuma wagonjwa wengi walikuwa na umri wa miaka 60 hadi 95,” amesema.
Amesema matumizi ya vinywaji vyenye sukari nyingi, maisha ya haraka na kutofanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ni miongoni mwa sababu zinazochangia ongezeko la matatizo ya figo kwa vijana.
Miongoni mwa changamoto zinazowasibu wagonjwa wenye magonjwa sugu ya figo ni usafishaji damu, huduma ambayo mgonjwa hupatiwa mara tatu kwa wiki, ili aendelee kuishi wakati akisubiri upandikizaji wa figo.
Gharama za usafishaji figo zimeendelea kushuka mwaka hadi mwaka mpaka kufikia kiasi cha Sh150,000 kwa mzunguko mmoja, hivyo mgonjwa kuhitaji Sh450,000 kwa mizunguko mitatu ya kila wiki.
Ili kukabiliana na gharama kubwa ya huduma ya usafishaji wa damu kwa wenye ugonjwa sugu wa figo, mashine mpya aina ya SWS 6000 ziliingizwa nchini ambazo zilishusha gharama ya tiba hiyo kutoka Sh250,000 mpaka Sh150,000.
Takwimu za huduma za figo
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya zilizotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Maghembe, huduma za figo nchini zimeimarika, huku vituo vya kusafisha damu (dialysis) vikiongezeka hadi kufikia 73 vyenye mashine 749 zinazohudumia zaidi ya wagonjwa 3,300.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa wagonjwa 177 wamefanikiwa kupandikizwa figo nchini.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaonya kuwa ugonjwa huo unaongezeka kwa kasi na unakadiriwa kuwa miongoni mwa magonjwa matano yatakayosababisha vifo vingi duniani ifikapo mwaka 2050 endapo hatua za kinga hazitachukuliwa.
WHO inaeleza kuwa mtu mmoja kati ya watano wenye shinikizo la damu huathiriwa na ugonjwa wa figo, huku watu wanne kati ya 10 wenye kisukari pia wakikumbwa na tatizo hilo.
Kutokana na hali hiyo, Dk Shija ametoa wito kwa wananchi kubadili mitindo ya maisha kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya ili kulinda afya ya figo.
“Ni muhimu wananchi kuzingatia ushauri wa wataalamu, kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuepuka matumizi kupita kiasi ya vinywaji vyenye sukari,” amesema.
Amesema pia ni muhimu jamii kuepuka “mtindo wa maisha wa haraka” unaohusisha ulaji usio na mpangilio na matumizi makubwa ya vinywaji vyenye sukari, akisisitiza kuwa kinga ndiyo njia bora ya kupunguza mzigo wa magonjwa ya figo nchini.