Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imesitisha kuendelea na usikilizaji wa kesi ya kampuni ya uagizaji mafuta ya Prestige Investment SA ya nchini Burundi dhidi ya kampuni ya uuzaji na usambazaji mafuta ya Lamar Commodity Trading DMCC ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Badala yake imeamuru kesi hiyo inayohusu mgogoro wa malipo ya shehena ya mita za ujazo 20,000 za mafuta ya petroli yaliyokuwa yamehifadhiwa nchini kabla ya kusafirishwa kwenda Burundi; ipelekwe Mahakama ya Usuluhishi wa Kimataifa ya London, Uingereza.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Abdallah Gonzi kufuatia shauri la maombi lililofunguliwa na Kampuni ya Lamar kupinga usikilizwaji wa kesi hiyo ya kibiashara namba 130 ya mwaka 2023 iliyofunguliwa na Kampuni ya Prestige.
Katika uamuzi huo na nakala yake kupatikana Machi 6, 2026, Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na hoja za wakili wa Lamar, Stephen Axwesso kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
“Kwa jumla, ombi hili linakubaliwa,” amesema Jaji Gonzi baada ya kupitia na kujadili hoja za pande zote, vifungu vya Sheria ya Usuluhishi na kesi mbalimbali za rejea na kuamuru.
“Ninatoa amri ya kusimamisha mwenendo wa kesi ya kibiashara namba 130/2023 kati ya wahusika hawa mpaka mgogoro utakapopelekwa kwenye usuluhishi katika Mahakama ya Usuluhishi wa Kimataifa ya London, kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha Mkataba wa Usambazaji mafuta wa tarehe 24 Juni 2022,”amesema Jaji Gonzi.
Kampuni ya Prestige na Lamar ziliingia mkataba Juni 24, 2022 kwa ajili ya Lamar kuiletea na kuiuzia Prestige mafuta kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Pia, Prestige iliingia mkataba na Benki ya KCB Kenya Limited iliyotoa hati ya dhamana ya malipo ya bidhaa hiyo kwa Lamar (SBLC) na SBLC pia ilidhaminiwa na Benki Kuu ya Burundi.
Hata hivyo, kampuni hizo ziliingia katika mgogoro baada ya Lamar kukataa kuikabidhi Prestige shehena ya tatu ya mafuta hayo kwa madai ya kushindwa kukamilisha malipo.
Hivyo, Prestige ilifungua kesi ya kibiashara namba 130/2023, Mahakama ya Biashara nchini, ikidai kuwa kampuni hiyo ya Lamar imekiuka mkataba huo.
Wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Kampuni ya Nomura Trading PTE Limited (mzalishaji wa mafuta hayo), KCB (mdhamini) na Lake Oil Limited (mhifadhi wa mafuta hayo nchini) baada ya kupakuliwa bandarini, waliounganishwa kama wadaiwa muhimu.
Pia, Prestige imeomba na kupata amri ya Mahakama iliyoiamuru Lamar iielekeze Lake Oil iikabidhi (Prestige) mafuta hayo wakati kesi hiyo ya msingi ikisubiri kusikilizwa.
Hata hivyo, Lamar imedai kuwa, ilikuwa imeshauza mafuta hayo kwa mnunuzi mwingine kwa kuwa, ilikuwa ikipata hasara ya gharama za kila siku za kuhifadhi mafuta hayo baada ya Prestige kushindwa kukamilisha malipo kwa wakati.
Baadaye ndipo Lamar ikafungua shauri hilo la maombi ya kusimamishwa kwa mwenendo wa kesi hiyo kusubiri mgogoro huo kupelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ya London, Uingereza.
Shauri hilo la maombi namba 8964/2025 limefunguliwa chini ya kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Usuluhishi pamoja na Kanuni ya 63(1)(a-e) na kifungu cha 63(2) cha Kanuni za Mwenendo wa Usuluhishi na lilisikilizwa kwa njia ya maandishi.
Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, Lamar iliwakilishwa na Wakili Stephen Axwesso huku Prestige ikiwakilishwa na wakili Seni Malimi.
Kila mmoja ametoa hoja kuishawishi Mahakama ikikubaliane na msimamo wake, wakirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa mashauri mbalimbali kuhusiana na hoja husika.
Wakili Axwesso alieleza kwamba, kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha mkataba huo wa usambazaji mafuta baina ya Lamar na Prestige, mgogoro au mabishano yoyote yatashughulikiwa kwa Sheria za Uingereza katika Mahakama ya Usuluhishi wa Kimataifa London, Uingereza.
Wakili Prestige, Seni Malimi pamoja na mambo mengine alidai kuwa, kuruhusu maombi ya kusimamisha kesi kusubiri usuluhishi ni suala la busara ya Mahakama kwa misingi ya sababu thabiti na si kwa uamuzi wa kiholela, ya hisia au huruma.
Hivyo aliiomba Mahakama itumie busara yake kukataa kusimamisha kesi hiyo kwa kuzingatia kwamba, makubaliano ya usuluhishi hayawezi tena kutekelezwa kwa kuwa, kesi hiyo imefikia hatua ya juu na amri mbalimbali tayari zimetolewa na Mahakama.
Mahakama katika uamuzi wake, imesema katika maombi ya kusimamisha shauri kusubiri usuluhishi, mwombaji anapothibitisha kuwepo makubaliano ya usuluhishi, kanuni ya jumla ni kwamba shauri linapaswa lisimamishwe.
Jaji Gonzi amesema upande unaopinga amri ya kusimamisha shauri unawajibika kuthibitisha kuwepo mojawapo au zaidi ya mazingira yaliyotajwa katika kifungu cha 15(4) cha Sheria ya Usuluhishi, yaani ubatili wa makubaliano ya usuluhishi husika na kwamba hayafanyi kazi au hayawezi kutekelezwa.
Hata hivyo, amesema kuwa katika shauri hilo, wakili wa Prestige hakuwahi hata kuibua hoja ya kuwepo mojawapo au zaidi, mazingira yanayobainishwa katika kifungu cha 15(4) cha Sheria ya Usuluhishi, kuifanya Mahakama isisimamishe kesi hiyo.
“Kushindwa kuthibitisha misingi hiyo kunaiacha Mahakama bila hiari nyingine isipokuwa kuruhusu maombi ya kusimamisha shauri hadi usuluhishi,” amesema Jaji Gonzi na kuongeza kuwa sababu zote zilizotolewa na wakili wa Prestige kupinga kesi hiyo kusimamishwa hazina msingi wa kisheria.