Magu. Mikopo ya kausha damu na mikopo ya vijana ni miongoni mwa kero zilizotawala mkutano wa hadhara wa Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika Nyanguge, wilayani Magu, mkoani Mwanza.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi ambaye alisikiliza kero za wananchi, baadhi akizitolea majibu papo hapo huku nyingine akitoa maelekezo kwa watendaji kuzifanyia kazi kabla hajamaliza ziara yake mkoani humo Machi 12, 2026.
Wananchi walilalamikia mikopo ya kausha damu wakisema inawaumiza, huku baadhi ya wanawake wakilazimika kukimbia nyumba zao hadi miaka miwili wakiwakwepa wanaowadai.
“Ukishindwa kulipa ndani ya muda unanyang’anywa kila kitu, imefikia kina mama wanakimbia nyumba zao hadi miaka miwili,” amesema mmoja wa wazee wa Nyanguge akiwakilisha wananchi.
Wananchi pia wamehoji namna Serikali inavyosaidia vijana kupata ajira. Akijibu, Kihongosi amesema hakuna Serikali inayoweza kuajiri kila kijana, lakini inaendelea kuandaa fursa mbalimbali za ajira na kujiajiri.
Amewahoji vijana kama wanafahamu mikopo ya Serikali kwa ajili yao, lakini wengi walisema hawaifahamu. Hali hiyo ilimfanya amwite ofisa maendeleo na kumtaka kesho yake (Machi 12) aje kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kupata mikopo hiyo.
Kihongosi amesema baadhi ya watendaji hushindwa kutimiza wajibu wao kwa kujifungia ofisini badala ya kuwahudumia wananchi.
Kuhusu mikopo ya kausha damu, amewataka wananchi kuachana nayo akisema inaweza kuwafilisi.
“Dawa ya deni ni kulipa, si kukimbia, lakini nawasihi muachane na mikopo kausha damu, itawafilisi,” amesema.
DMO abananishwa na kero za afya
Katika mkutano huo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Magu (DMO), Dk Raphael Mhana amebananishwa na wananchi waliolalamikia kukosekana kwa wodi ya kujifungulia, upungufu wa madaktari na madai ya wajawazito kutozwa kati ya Sh10,000 na Sh15,000 licha ya Serikali kutangaza huduma hizo ni bure.
Akijibu, Dk Mhana amesema Serikali inakamilisha ujenzi wa wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya Mwabuye ambayo imefikia asilimia 95 na inatarajiwa kukamilika Aprili mwaka huu.
Kihongosi ameagiza wodi hiyo ianze kutoa huduma ifikapo Mei Mosi.
Kuhusu malalamiko ya kutozwa fedha, DMO amesema ada hiyo ni kwa vipimo vya awali siku ya kwanza ya kliniki ili kuthibitisha ujauzito, na baada ya hapo huduma zote hadi kujifungua ni bure. Hata hivyo, Kihongosi amemwagiza kufanya uchunguzi na kuchukua hatua kama kuna wanaotoza kinyume na maelekezo ya Serikali.
Upungufu wa madaktari na huduma hospitalini
Wananchi pia wamelalamikia ukosefu wa madaktari katika Kituo cha Afya Mwabuye. DMO amesema changamoto hiyo ipo karibu wilaya nzima kutokana na upungufu wa watumishi, lakini madaktari wapya watatu wanatarajiwa kuripoti Nyanguge.
Katika malalamiko kuhusu Hospitali ya Nyanguge kudaiwa kupunguzwa huduma kama upasuaji na mochwari, DMO amesema Serikali inaendelea na mradi wa ujenzi wa miundombinu, tayari Sh250 milioni zimetolewa kwa ajili ya jengo la wazazi na zinatarajiwa kupatikana Sh500 milioni zaidi kwa wodi ya wanaume, maabara, X-ray na mochwari.
Maagizo kwa viongozi na watendaji
Kihongosi pia amemkumbusha diwani wa kata hiyo kufanya mikutano ya hadhara akisema nafasi ya uongozi ni ya wananchi.
Amesema atawasiliana na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuhusu changamoto ya maji Nyanguge.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi akizungumza katika mkutano wa hadhara Nyanguge, Wilayani Magu mkoani Mwanza.
Aidha, ameelekeza nyumba ya mzee wa miaka 75 aliyeibiwa betri ya sola kuunganishiwa umeme na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa gharama za chama, pamoja na kumpa Sh200,000 kununua tochi.
Pia amemuagiza OCD kufuatilia vibaka wanaolalamikiwa eneo hilo na kudhibiti vitendo vya wizi.
Katika mkutano huo, Kihongosi pia amemsaidia mgonjwa mwenye tatizo la mguu kupata bima ya afya ya zaidi ya Sh900,000 baada ya viongozi na watendaji waliokuwepo kuchangishana.
Ziara ya Kihongosi mkoani Mwanza ilianza wilayani Magu na itaendelea Sengerema, akifuatilia uhai wa chama, kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.