Mo Dewji akomaa orodha ya mabilionea Afrika Mashariki, Motsepe apanda

Mohammed Dewji anaendelea kuongoza katika orodha ya mabilionea wenye umri mdogo zaidi Afrika lakini pia ndiye anaongoza kwa utajiri katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Rais wa Heshima wa Simba na mfanyabiashara Mohammed Dewji, ameshuka kwa nafasi mbili katika chati ya mabilionea Afrika kwa mujibu wa ripoti ya jarida na mtandao wa Forbes ambayo imetoka jana, Jumatatu, Machi 9, 2026.

Kwa sasa Dewji anashika nafasi ya 14 akiwa na utajiri ambao unatajwa kufikia kiasi cha Dola 2.1 bilioni (Sh5.4 trilioni) ukichangiwa na uwekezaji katika viwanda vya nguo, unga wa ngano na sembe, mafuta ya kupikia, sabuni, sukari, vinywaji na biashara ya katani.

Kabla ya orodha hiyo ya mabilionea ya kwanza kutolewa kwa mwaka 2026, Dewji alikuwa nafasi ya 12 katika orodha ya mwisho kwa mwaka 2025 iliyotoka Desemba 8, 2025 akiwa na utajiri uliokadiriwa kufikia Dola 2.2 bilioni (Sh5.7 trilioni).

Pamoja na kuanguka kwa nafasi mbili, Dewji anaendelea kuongoza katika orodha ya mabilionea wenye umri mdogo zaidi Afrika lakini pia ndiye anaongoza kwa utajiri katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Wakati Dewji akishuka kwa nafasi mbili, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe amependa kwa nafasi moja kutoka ile ya tisa aliyokuwepo Desemba mwaka jana hadi ya nane.

Utajiri wa Motsepe umepanda hadi kufikia kiasi cha Dola 4.3 bilioni (Sh11 trilioni) kutoka ule wa Dola 3.6 bilioni (Sh9 trilioni) aliokuwa nao Desemba, 2025.

Orodha hiyo ya mabilionea Afrika inaendelea kuongozwa na Aliko Dangote wa Nigeria ambaye utajiri wake umepanda hadi kiasi cha Dola 28.5 milioni (Sh74 trilioni).

Desemba mwaka jana, Dangote alikuwa kinara kutokana na utajiri uliokadiriwa kufikia kiasi cha Dola 25.6 bilioni (Sh66 trilioni) katika orodha ya mwisho kabla ya hii ya sasa.

Nafasi ya pili katika orodha hiyo inashikiliwa na Johann Rupert na familia yake akiwa na utajiri wa Dola 16.1 bilioni (Sh42 trilioni).

Anayeshika nafasi ya tatu ni Abdulsamad Rabiu ambaye an utajiri unaokadiriwa kufikia kiasi cha Dola 11.2 bilioni (Sh29 trilioni).

Thamani ya utajiri inayotolewa na Forbes huwa inakokotolewa kwa kutumia bei za hisa na viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni vilivyokuwepo mwishoni mwa shughuli za kibiashara Machi Mosi, 2026.