NI Elie Mpanzu ambaye dakika 15 za mwisho zilitosha kwake kuimaliza mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa leo Jumatano Machi 11, 2026 ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Airtel mkoani Singida.
Wakati ambao kocha wa Simba, Steve Barker alikuwa akiumiza kichwa mchezaji wa kuamua mechi hiyo ambayo hadi dakika ya 75 mzani ulikuwa sawa, alifanya hesabu za vidole.
Alimuinua Mpanzu ambaye alionekana kuitaka mechi tangu wakati akipasha na kumpa alichotaka, akiwa amevunja mtego wa kuotea katika dakia ya 84 kufuatia pasi ya Clatous Chama.
Mkongomani huyo amewafanya mashabiki wa Simba kuondoka mkoani Singida kifua mbele kutokana na ushindi huo uliowafanya kujikita nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 27 baada ya mechi 12, ikiachwa moja na JKT Tanzania (pointi 28) na tano dhidi ya Yanga yenye 32. Huku ikiiacha Azam ikiwa na 24 ambayo baadaye usiku itakipiga na Dodoma Jiji.
Kwa zaidi ya dakika 30, licha ya kuwa na umiliki mkubwa katika kipindi cha pili, Simba haikuonekana kuwa na mtu hatari eneo la mwisho licha ya mabadilko kadhaa ambayo Barker aliyafanya eneo.
Barker alianza na Inno Loemba, baadae akamtumia Mwangosi kabla ya Mpanzu ambaye aliingia na kuongeza namba, hakutokea pembeni kama ilivyozoeleka, iliibia na kusogea kati.
Dakika 45 za kwanza zilianza kwa Simba kulisakama lango la Singida Black Stars huku ikitumia zaidi maeneo yake ya pembeni ambako walikuwa wakicheza Anicet Oura na Libasse Gueye.
Hesabu kwa Simba zilijipa katika dakika ya saba tu baada ya Anicet Oura kumalizia mpira ambao Singida BS ilikuwa katika hekaheka za kuondoa hatari hiyo.
Simba ilikuwa bora ndani ya dakika 30 za kipindi hicho cha kwanza kabla ya Singida Black Stars kuzinduka mwishoni mwa kipindi hicho cha kwanza kufuatia bao la Ndumumwe Mossi.
Mossi aliisawazishia Singida BS kwa kichwa kufuatia krosi ya Lamine Jarjou dakika ya 38.
Simba ilirejea kipindi cha pili na kufanya mabadiliko, alitolewa Alasane Kante na kuingia Baraka Mwangosi.
Mabadiliko hayo yalimfanya Loemba kubadilisha majukumu kutoka eneo la mshambuliaji wa mwisho na kutumika katika eneo la kiungo ambalo awali alikuwa akicheza Kante sambamba na Yusuph Kagoma.
Huku Mwangosi akisimama kama mshambuliaji wa mwisho. Hata hivyo licha ya mabadiliko bado mambo hayakuwa mazuri kwa Simba katika dakika 15 za kwanza katika kipindi cha pili.
Badala yake Singida BS ilionekana kuwa bora zaidi huku ikinufaika na uzoefu wa Khalid Aucho katika eneo la kiti la uwanja na eneo la winga ya kulia ambako alikuwa akicheza Jarjou.
Katika dakika ya 69, Singida BS ilifanya mabadiliko mawili kwa mpigo kwa kuwatoa Khalid Aucho na Mossi huku wakiingia Elvis Rupia na Linda Mtange.
Simba nayo ilifanya mabadiliko katika chache baadaye kwa kutoka Libase Gueye na kuingia Morice Abraham.
Dakika ya 77, Mwangosi alipoteza nafasi ya wazi kufuatia kushindwa kutumia vyema krosi ya Kapombe ambapo kichwa chake kiliokolewa na Metacha Mnata. Katika dakika 15 za mwisho Simba ilionekana kulisakama lango la Singida BS huku pia akiingia Mpanzu aliyefunga bao la ushindi akichukua nafasi ya Loemba.
Kipigo hicho ni cha pili mfululizo kwa Singida Black Stars ikiwa nyumbani katika Ligi Kuu Bara ikiruhusu jumla ya mabao matano baada ya awali kufungwa 3-0 na Yanga, kabla ya leo kupigwa 2-1 na Simba.