KICHAPO cha mabao 2-0 ilichopokea Namungo kutoka kwa TRA United, kimeifanya timu hiyo kutoka Ruangwa mkoani Lindi kufikisha mechi saba mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ushindi.
Timu hiyo inayonolewa na Juma Mgunda, mara ya mwisho ilishinda bao 1-0 dhidi ya KMC ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Majaliwa, Januari 31, 2026.
Zimepita takribani siku 39 Namungo ikisaka ushindi mwingine kwenye ligi, lakini kwa bahati mbaya imepokea vichapo vinne kutoka kwa Pamba Jiji (1-0), Tanzania Prisons (3-2), Yanga (1-0) na TRA (2-0), huku sare zikiwa tatu dhidi ya Fountain Gate (1-1), Mtibwa Sugar (1-1) na Singida Black Stars (1-1).
Katika mechi ya leo iliyoanza saa 8:00 mchana ikichezwa kwenye Uwanja wa Black Rhino uliopo Karatu mkoani Arusha, TRA United ikiwa nyumbani iliibuka na ushindi huo wa mabao 2-0.
Mabao hayo yalifungwa na Chamou Karaboue kwa kichwa akiunganisha faulo iliyopigwa na Valentino Nouma dakika ya 62, kisha Joseph Akandwanaho akahitimisha ushindi kwa bao kali dakika ya 90+2 akimchungulia kwa mbali, kipa wa Namungo, Mussa Malika.
Ushindi huo umeifanya TRA United kufikisha pointi 19 na kupanda kutoka nafasi ya 11 hadi tisa, ikizishusha Singida Black Stars (pointi 19) na Mashujaa (pointi 17).
Namungo yeneywe imebaki na pointi 21, lakini imeshuka nafasi moja kutoka ya sita hadi ya saba.
Matokeo hayo mabaya yanabaki kuwa mtihani mzito kwa Mgunda, hata hivyo ana muda zaidi wa kukiimarisha kikosi chake kwa takribani siku 14 kwani kituo kinachofuata ni dhidi ya JKT Tanzania, mechi ikitarajiwa kuchezwa Aprili 4, 2026 kwenye Uwanja wa Majaliwa.