Rais Samia ateta na mwakilishi UN

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania imejizatiti kuhakikisha mchakato wa kufuatilia matukio ya maandamano yaliyozaa vurugu Oktoba 29, 2025 unafanyika kwa kuzingatia utawala wa sheria, uwajibikaji na haki.

Amesisitiza hayo yanafanyika huku nchi ikiendelea kulinda amani, umoja wa kitaifa na utulivu wa kisiasa ambao umekuwa msingi wa wakati wote wa maendeleo ya nchi.

Mkuu huyo wa nchi, ameeleza hayo kwa Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Parfait Onanga-Anyanga, wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika leo Jumatano, Machi 11, 2026, Ikulu ya Dodoma, yakijikita zaidi kwenye  matukio hayo na hali ya siasa na demokrasia nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Parfait Onanga-Anyanga, leo Jumatano, Machi 11, 2026, Ikulu ya Dodoma.



Hayo yameelezwa katika taarifa iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu.

Onanga-Anyanga yupo nchini kusikiliza maoni ya wadau na kutathmini hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha utulivu wa kisiasa, mshikamano wa kitaifa na kuendeleza misingi ya utawala wa sheria baada ya Oktoba 29, 2025.

Tayari mjumbe huyo, ameshazungumza na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahakama ya Tanzania, Bunge, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na viongozi wa vyama vya siasa.

Aidha, amekutana na kuzungumza na Mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchunguzi na wadau wengine wa kisiasa na kijamii ili kupata maoni na mitazamo tofauti kuhusu masuala yaliyotokea na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali.

Samia amesema Tanzania imejizatiti kuhakikisha mchakato wa kufuatilia matukio ya maandamano yaliyozaa vurugu Oktoba 29, mwaka jana unafanyika kwa kuzingatia utawala wa sheria, uwajibikaji na haki.


“Tutafanya hivyo huku nchi ikiendelea kulinda amani, umoja wa kitaifa na utulivu wa kisiasa ambao umekuwa msingi wa wakati wote wa maendeleo ya nchi,” amesema.

Ametumia mazungumzo hayo, kutuma salamu za shukurani na pongezi kwa hatua ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, kutuma ujumbe maalumu nchini ili kupata uelewa wa kina kuhusu hali ya nchi na kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali.

Mkuu huyo wa nchi, amesema Serikali ipo tayari kupokea na kuyafanyia kazi mapendekezo yatakayowasilishwa na Tume ya Uchunguzi baada ya kukamilika kwa kazi yake.

Amesema mapendekezo hayo yatakuwa sehemu muhimu ya mchakato wa kuimarisha maridhiano ya kitaifa na marekebisho ya Katiba.

Amesisitiza Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa na jumuiya za kimataifa katika kukuza demokrasia, utawala bora na maendeleo jumuishi.

Kwa upande wake, Onanga-Anyanga amesema UN inatambua na kupongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali baada ya matukio ya Oktoba 29, hasa uundwaji wa tume ya uchunguzi na dhamira ya kufanya mazungumzo jumuishi ya kitaifa.

Amesema UN inaendelea kuitambua Tanzania kama nchi yenye historia ya muda mrefu ya amani, utulivu wa kisiasa na mshikamano wa kitaifa na inathamini mchango wake katika juhudi za kulinda na kuimarisha amani barani Afrika.

Onanga-Anyanga, amesema mashauriano hayo yatauwezesha Umoja wa Mataifa kupata taswira halisi kuhusu uhalisia wa matukio ya Oktoba 29 na juhudi zinazofanywa na Serikali katika utatuzi wa changamoto zilizojitokeza wakati na baada ya matukio hayo.

Ameeleza hatua hizo zina mchango muhimu katika kuimarisha maridhiano ya kitaifa, kurejesha imani ya wananchi na kuendelea kujenga taasisi imara za kidemokrasia nchini.

Ameahidi kuwasilisha tathmini ya mashauriano hayo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ili kuendelea kuimarisha mashauriano baina ya umoja huo na Tanzania.