Iringa.Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ameagiza viongozi wa halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa mapendekezo yaliyotokana na utafiti wa sekta ya misitu na mnyororo wa thamani.
Amesisitiza kuwa lengo ni kuboresha biashara ya mazao ya misitu na kuongeza kipato cha wakulima wa miti ambao ndio nguzo kuu ya sekta hiyo mkoani humo.
James ametoa maagizo hayo leo Jumatano, Machi 11, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati wa kikao maalumu cha kuwasilisha matokeo ya utafiti huo uliofanyika kwa uwezeshaji wa Mradi wa Maendeleo ya Misitu, Matumizi ya Ardhi na Mnyororo wa Thamani nchini Tanzania (Forland).
Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi kutoka halmashauri zote za mkoa, wataalamu wa sekta ya misitu pamoja na wadau wa biashara ya mbao waliokutana kujadili matokeo na mapendekezo ya utafiti huo.
Akizungumza katika kikao hicho, James amesema sekta ya misitu ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochochea uchumi wa Mkoa wa Iringa kutokana na uwepo wa mashamba makubwa ya miti pamoja na biashara ya mbao, magogo na nguzo za umeme zinazotokana na rasilimali hiyo.
James amesema ni muhimu kuhakikisha sekta hiyo inasimamiwa vizuri ili kuwasaidia wakulima na kuongeza mapato ya Serikali.
“Licha ya umuhimu mkubwa wa sekta hii bado kuna changamoto kadhaa zinazowakwamisha wakulima wadogo kunufaika ipasavyo na mazao yao. Changamoto hizo ni pamoja na mfumo usio na uwazi wa biashara, ukosefu wa taarifa sahihi za soko pamoja na changamoto za pembejeo zinazohitajika katika uzalishaji wa miti yenye ubora,” amesema James.
Wakurugenzi na Viongozi mbalimbali wa Halmashauri mkoani Iringa wakisikiliza taarifa ya utafiti wa sekta ya misitu na mnyororo wa thamani. Picha na Christina Thobias
Ametaja changamoto nyingine zinazohitaji kushughulikiwa ni pamoja na malalamiko ya utozwaji wa tozo mbalimbali katika biashara ya mazao ya misitu, changamoto za usimamizi wa udhibiti na uzimaji wa moto katika mashamba ya miti pamoja na upatikanaji wa mbegu bora za miche kwa wakulima.
Aidha, utafiti huo umeeleza kuwa kuna changamoto katika uratibu wa biashara ya magogo kati ya wakulima na wanunuzi.
“Mara nyingi wakulima wamekuwa wakilalamikia kukosekana kwa uwazi wa bei na wakati mwingine hulazimika kuuza mazao yao kwa bei ndogo kutokana na kukosa taarifa sahihi za soko,” amesema.
Kwa mujibu wake, matokeo ya utafiti huo hayapaswi kuishia kwenye makaratasi bali yawe chachu ya mabadiliko ya kweli katika sekta ya misitu ili kuhakikisha wakulima wanapata manufaa zaidi kutokana na juhudi zao za kuzalisha miti.
Katika hatua nyingine, James ameagiza halmashauri zote za Mkoa wa Iringa kuhakikisha zinarejesha asilimia tano ya mapato yatokanayo na sekta ya misitu ili fedha hizo zitumike kuboresha shughuli za sekta hiyo, ikiwemo utoaji wa elimu kwa wakulima na usimamizi wa misitu.
Awali, Mshauri Elekezi wa Forland, Ignatus Matofali wakati akiwasilisha taarifa ya utafiti huo amesema wamebaini kuwa sekta ya misitu inategemea kwa kiasi kikubwa wakulima wadogo ambao wanachangia asilimia 89 ya uzalishaji wa miti katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Mshauri elekezi wa Forland, Ignatusi Matofali akitoa taarifa ya utafiti wa sekta ya misitu na mnyororo wa thamani. Picha na Christina Thobias
Matofali amefafanua kuwa wakulima hao wanamiliki takribani hekta 170,000 za mashamba ya miti katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa na ndio wanaochangia kwa kiwango kikubwa cha upatikanaji wa malighafi katika viwanda vinavyochakata mazao ya misitu.
Hata hivyo, amesema pamoja na mchango wao mkubwa, wakulima hao hupata takribani asilimia 10 tu ya thamani ya mauzo ya nje ya mazao ya misitu, jambo linaloonyesha kuwepo kwa pengo kubwa la kiuchumi katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
“Utafiti huu ulifanyika kwa kuwahoji wakulima 214 kutoka wilaya za Kilolo, Mufindi na Mafinga. Tulitumia mbinu za takwimu pamoja na mahojiano ya kina ili kupata picha halisi ya hali ya biashara ya mazao ya misitu,” amesema Matofali.