Njombe. Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (Rea) umewaalika wadau wa sekta binafsi kutumia fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini kuwekeza katika miradi ya uzalishaji wa umeme vijijini.
Wakala huo umeeleza kuwa kuna fursa nyingi hasa katika mikoa ya Njombe, Ruvuma na Iringa ambako kuna vyanzo vingi vya maji vinavyoweza kutumika kuzalisha umeme hatua itakayosaidia kuchochea shughuli za uchumi katika maeneo yatakayofikiwa na miradi hiyo.
Kaimu Meneja wa Usaidizi wa Kiufundi kutoka Rea, Mhandisi Emmanuel Yesaya, ametoa wito huo leo, Machi 11, 2026, alipozungumza na wahariri baada ya kutembelea mradi wa uzalishaji umeme wa kilowati 317 wa Lupali, uliopo katika Kijiji cha Boimanda, Kata ya Matola, wilayani Njombe.
Mradi huo unatekelezwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe kupitia Shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent Imiliwaha.
Amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi inayozalisha umeme na kuuingiza katika Gridi ya Taifa.
Mratibu wa mradi wa uzalishaji umeme wa Lupali, Sista Imakulata Mlowe (kulia) akielezea mradi huo.
Amesema Serikali kupitia Rea imetoa ruzuku kwa awamu tano zenye jumla ya Sh5.4 ambazo zimewezesha ujenzi wa kituo cha uzalishaji wa umeme na miundombinu ya usambazaji kwenye kituo hicho pamoja na vijiji vya jirani vya Boimanda, Kitulila na Matola sambamba na kuwezesha tafiti za mradi huo.
‘Utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 99 na kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja na ujenzi wa kizuizi na mtaro wa kupitisha maji ya mafuriko ambao tayari umekamilika.”
“Kilichosalia ni kuunganisha mtambo kwenye Gridi ya Taifa na kuuwasha ili kuongeza kilowati 317 kwenye gridi,” amesema.
Ameeleza kuwa ujenzi wa mradi huo ulianza mwaka 2021 na baada ya miezi mitatu ijayo mtambo utawashwa na umeme kuingizwa katika Gridi ya Taifa.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amewahimiza Watanzania kuitumia fursa hiyo ya uwekezaji katika miradi ya uzalishaji umeme nchini badala ya kuiachia kwa wawekezaji wa kigeni.
“Masista hawa wameonesha njia kwa kuanzisha mradi huu. Vijana na wazee wamealikwa kuwekeza; tuitumie fursa hii vizuri,” amesema.
Awali, Mratibu wa mradi huo, Sista Imakulata Mlowe, amesema baada ya mradi kukamilika, umeme utakaozalishwa utauzwa moja kwa moja kwa Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) na tayari mkataba wa kuuziana umeme umeshasainiwa.
Sista Imakulata amesema kazi iliyobaki ya kuunganisha miundombinu ya mradi itakayogharimu Sh1.08 bilioni, na tayari maombi ya ruzuku yameshawasilishwa Rea.
Amesema mradi utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi kwa matumizi ya nyumbani na biashara na kupunguza matumizi ya nishati isiyo rafiki na mazingira.