Dar/Nairobi. Mfanyabiashara Rostam Azizi amesema uwekezaji wake katika kampuni ya Nation Media Group (NMG) hautaathiri weledi wa uandishi wa habari uliojengwa na vyombo vya habari nya kampuni hiyo kwa muda mrefu.
Amesema uwekezaji wake utaendelea kuheshimu misingi ya uhariri, viwango vya taaluma ya uandishi wa habari na imani ya umma, ambayo imeijengea heshima kampuni ya NMG tangu miaka ya 1950.
Nation Media Group ni moja ya kampuni kubwa za habari Afrika ikiwa na shughuli katika nchi za Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda. Kampuni hiyo inachapisha magazeti mbalimbali yakiwemo Daily Nation, Sunday Nation, The East African, The Business Daily na Taifa Leo ya Kenya; Daily Monitor na Sunday Monitgor ya Uganda pamoja na Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti ya Tanzania.
Pia inamiliki Televisheni ya NTV Kenya na Uganda na vituo vya redio Kenya, Uganda na Rwanda
Rostam amesema nguvu kubwa ya Nation Media Group iko katika rasilimali watu wake, ikiwemo waandishi wa habari, wahariri na wataalamu wengine wa tasnia ya habari pamoja na uaminifu mkubwa walioujenga kwa wasomaji na watazamaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Urithi huo wa kitaaluma na uaminifu wa muda mrefu, ndio msingi wa mafanikio ya Nation Media Group katika kuhabarisha jamii na kuchangia maendeleo ya kidemokrasia katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki,” amesema.
Akitangaza uwekezaji wake wa kimkakati na ushirikiano wa umiliki wa hisa katika Nation Media Group na Kampuni ya Taifa Group mbele ya waandishi wa habari jijini Nairobi, Kenya, mfanyabiashara aliyenunua hisa asilimia 53.08 NMG, Rostam amesema huo ni uwekezaji katika mustakabali wa uandishi wa habari barani Afrika.
Amesema tasnia ya vyombo vya habari duniani inapitia mabadiliko makubwa. Teknolojia ya kidijitali inabadilisha namna ambavyo taarifa zinatengenezwa, kusambazwa na kutumiwa na jamii.
“Leo, nina furaha kutangaza uwekezaji wa kimkakati katika Nation Media Group PLC, moja ya taasisi zinazoheshimika zaidi za vyombo vya habari barani Afrika.
“Taasisi hii, yenye makao makuu hapa nchini Kenya, kwa miongo kadhaa imekuwa na nafasi ya msingi katika kuunda mijadala ya umma katika Afrika Mashariki na kuimarisha uhusiano kati ya watu wa ukanda wetu.
“Kupitia uwekezaji huu, nitajiunga na kampuni hiyo kama mwanahisa na mshirika wa kimkakati wa muda mrefu, nikiunga mkono ukuaji wake endelevu, ubunifu na mabadiliko katika enzi ya kidijitali,” amesema.
Amesema ushirikiano huu unaleta pamoja Taifa Group na Nation Media Group kwa dhamira ya pamoja ya kuimarisha mfumo wa vyombo vya habari Afrika Mashariki na kusaidia ukuaji endelevu wa uandishi wa habari unaoaminika na simulizi za Kiafrika katika ukanda wetu.
“Uandishi wa habari imara hujengwa juu ya uaminifu, taaluma na uongozi wa uhariri unaowajibika. Taasisi ya habari hupata imani ya umma kupitia utafiti makini wa habari, mitazamo iliyosawazishwa na kujikita katika ukweli.
“Jukumu langu kama mwekezaji ni kuunga mkono uimara wa taasisi, kwa kuhakikisha inakuwa na rasilimali, uongozi na uthabiti unaohitajika ili kuendelea kulitumikia taifa kwa weledi na uadilifu,” amesema na kuongeza;
“Tangazo la leo pia linaakisi jambo muhimu zaidi kuhusu mabadiliko ya tasnia ya vyombo vya habari Afrika Mashariki.
“Kwa waandishi wa habari, wahariri na wasomaji wa Nation Media Group, nasema hivi: Urithi wenu utaheshimiwa. Taasisi yenu itaendelea kuimarishwa. Na mchango wenu katika kuunda mustakabali wa ukanda wetu utaendelea kuthaminiwa,” amesema.
Alipoulizwa atawezaje kuendesha chombo cha habari kwa uhuru ikiwa mtangazaji mkuu ni Serikali, Rostam amesema huwezi kuendesha chombo cha habari kwa kutegemea matangazo pekee kutoka kwa Serikali.
“Hatuendi kuathiri uhuru wetu kwa sababu ya matangazo, tunahitaji kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato zaidi ya matangazo kutoka serikalini, hii ndio namna ya kukuza chombo cha habari binafsi kwa uhuru,” amesema.
Amesisitiza haogopi kuona Serikali ikikataa kutangaza na vyombo vya habari vya Nation Media Group, akisema amejiandaa na anaamini ukijenga heshima na wafuatiliaji wengi, ndivyo utapata watangazaji wengi kwa kuwa Serikali na sekta binafsi wote watalazimika kutangaza kwako.
Rostam, ameeleza katika uwekezaji kunahitajika utayari kwa maana ya rasilimali, hivyo hana mpango wa kuua baadhi ya ajira za wafanyakazi ili kupunguza gharama za uendeshaji.
“Kampuni inapaswa kuwa na faida zaidi na zaidi, hivyo huwezi kupata faida kama hauwekezi zaidi. Kwa hiyo niwahakikishie wafanyakazi wa Nation Media Group, nia yetu ni kukua siyo kupungua. Tutazalisha kazi nyingi zaidi sio kupunguza,” amesema.
Vivyo hivyo, ameeleza katika uwekezaji wake, hataua baadhi ya bidhaa kwa sababu ya kufanya vibaya sokoni, badala yake ataongeza ubunifu kuhakikisha zinajibeba au kubebwa na nyingine zitakazofanya vizuri zaidi.
Amejibu hilo, alipoulizwa kuhusu hatima ya Gazeti la Taifa Leo, linalodaiwa kuzalisha hasara, akisema bidhaa moja isiyozalisha faida inapaswa kubebwa na zile zinazozalisha zaidi.
“Ukianza kufanya hivyo, unaenda kuidogosha kampuni. Unapaswa kuwa mbunifu wa kutosha kuhakikisha unaliinua lile gazeti linalochechemea. Ukiona linachechemea unatakiwa kulibeba na kwenda nalo sio kuliacha,” amesema.
Katika hilo, ameeleza yeye ni mwekezaji anayetarajia faida kwa muda mrefu na sio kufaidika kwa haraka, hivyo anahitaji kuwekeza fedha ili kuona faida baadaye.
“Sisi ni wawekezaji ambao tunaangalia muda mrefu hatuangalii kupata faida leo leo. Hivyo huu ni uwekezaji wa muda mrefu,” amesema.
Alipoulizwa iwapo ukaribu wake na viongozi wa Serikali hautaathiri uhuru wa vyombo vya habari anavyomiliki, amesema amekuwa karibu na viongozi wengi katika mataifa mengi, jambo ambalo halina ubaya baya.
Kwa Kenya, amesema anafahamiana na Rais William Ruto, kabla yake alikuwa karibu na Rais mstaafu Yoweri Museveni, pia alikuwa rafiki wa hayati Raila Odinga na alikuwa mgeni rasmi katika harusi ya bintiye.
Lakini, amesema uhusiano wake binafsi na watu au viongozi wa Serikali hauna athari zozote katika biashara yake na kwamba anauchukulia kama uhusiano wa kawaida.
“Huo ni uhusiano binafsi, hautafanya lolote katika masuala ya biashara. Niko karibu na viongozi wa Zambia, Uganda na hivyo ndivyo nimekuwa nikisisitiza, ili kujenga Afrika Mashariki imara unahitaji kujenga uhusiano,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu yeye Mtanzania kuwekeza nchini Kenya, Rostam amejibu mataifa hayo si maadui na wanaodhani kuna uadui hawana maana.
Amesema ni umoja na ushirikiano wa Tanzania na Kenya ndio unaoyafanya mataifa hayo yawe imara, akisisitiza Kenya pekee haiwezi kuimarika pasi na kushirikiana na mataifa mengine.
“Wakenya inabidi mbadilike kidogo, someni alama za nyakati. Tuko imara tukiwa pamoja, msichonacho tunacho, tusichonacho mnacho na kwa pamoja tunaweza kujenga uchumi kama tutajitazama tu wamoja,” amesema.
Amesisitiza Wakenya wanapaswa kuacha kufikiri kuwa Kenya ni kubwa kuliko mataifa mengine ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
“Kenya inapaswa kuelewa, uimara wake unatokana na ushirikiano wake na majirani yake. Tunaifanya Kenya kuwa imara, na Kenya inaifanya Tanzania kuwa imara na sote tunaifanya Afrika Mashariki kuwa imara,” amesema.
Safari ya vyombo vya habari
Rostam ameeleza kuwa safari yake katika tasnia ya vyombo vya habari ilianza zaidi ya miaka 26 iliyopita alipokuwa miongoni mwa wawekezaji waanzilishi wa Mwananchi Communications Limited nchini Tanzania, taasisi ambayo imekuwa nguzo muhimu katika tasnia ya habari nchini.
Amesema mwaka 2003, alimwalika Aga Khan IV kuwa mwekezaji katika Mwananchi Communications Ltd, mwaliko uliokubaliwa na kuimarisha juhudi za kuendeleza taasisi huru za vyombo vya habari katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Rostam amesema mwaka 2006 aliuza hisa zake ili kuruhusu taasisi hiyo iendelee kukua chini ya uongozi wa Aga Khan na maono yake ya muda mrefu.
Amesema kuwa hatua ya leo ni kama mzunguko uliokamilika, kuendelea na juhudi za kuimarisha uandishi wa habari huru na unaoaminika.
Akoizungumzia uwekezaji huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Rose Reuben amepongeza hatua hiyo akisema inaonuesha uwezo wa wawekezaji wa Afrika kuendeleza taasisi kubwa za vyombo vya habari za kikanda.
“Ni jambo la kutia moyo kuona mwekezaji wa ndani akionyesha uwezo wa kumiliki taasisi kubwa kama hii ya vyombo vya habari, hivyo waandishi wa habari wanapaswa kuendelea kuzingatia viwango vya taaluma zao,” amesema.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema ununuzi huo unaweza kuimarisha uwekezaji wa teknolojia katika vyombo vya habari Afrika Mashariki.
Amesema Nation Media Group imekuwa ikiwekeza kwa kiwango kikubwa katika mifumo ya kisasa ya uzalishaji wa habari na anaamini umiliki mpya utaendeleza uimarishaji wa miundombinu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mpito wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa Tanzania), Ali Bakari Othman, ameipokea hatua hiyo kwa matumaini, akisema inaleta fursa ya kuimarisha viwango vya uandishi wa habari na ustawi wa wanahabari katika ukanda huu.
“Jambo la msingi ni kusisitiza ulinzi wa masilahi ya kitaaluma na mazingira ya kazi ya wanahabari,” amesema.