BAADA ya kucheza mechi mbili za ugenini kwa dakika 180 ikiambulia pointi mbili, Azam FC imeamkia kwa Dodoma Jiji kufuatia kuichapa mabao 3-0.
Dodoma Jiji iliyotoka kuikazia Simba mechi ya mwisho ya ligi kucheza nyumbani kwa kutoka 0-0, leo Machi 11, 2026 imekutana na kipigo hicho kikali huku kijana wao wa zamani, Zidane Sereri aliyetokea hapo kabla ya kutua Azam, akiwaua chuma mbili.
Mechi hiyo ilianza saa 1:15 usiku ikichezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma uliokuwa na hali isiyo nzuri kutokana mvua iliyonyesha na kufanya sehemu ya kuchezea kuwa na tope lililochanganyika na maji katika maeneo mengi.
Sereri alianza kufungua akaunti ya mabao dakika ya tano baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ akiwa ndani ya boksi na kumchambua kipa wa Dodoma Jiji, Daniel Mgore.
Fei Toto aliyetoka kutumikia adhabu ya kadi nyekundu iliyomfanya akose mechi mbili zilizopita, akaongeza bao la pili dakika ya 12 akiitumia vizuri pasi ya Sereri.
Mabao hayo ya mapema ndani ya dakika 15 za kwanza, yalionekana kuichanganya Dodoma Jiji huku ikiwa inamkosa beki wake wa kati, Abdi Banda anayetumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu.
Licha ya kuruhusu mabao hayo mawili ya mapema, Dodoma Jiji ilijipanga vizuri na kufanya kipindi cha kwanza kuonekana kuwa na ushindani mkubwa, lakini mabao hayo yaliifanya Azam kuwa na faida zaidi.
Kipindi cha pili, Kocha wa Dodoma Jiji, Amaan Josiah akaona aongeze nguvu eneo la ushambuliaji, dakika ya 59, akamtoa Dickson Ambundo na kuingia Yassin Mgaza aliyekwenda kucheza sambamba na Faraji Kayanda.
Mabadiliko hayo hayakusaidia kitu zaidi ya kuinufaisha Azam ambayo dakika ya 70 ilimtoa Idd Seleman na kuingia Jephte Kitambala kisha kushuhudiwa Sereri akipachika bao la tatu dakika ya 71 baada ya walinzi wa Dodoma Jiji kujichanganya wakati wa kuokoa hatari iliyotokana na Ashrafu Kibeku kupiga pasi ya chini ndani ya boksi.
Kwa kuona hivyo wapo nyuma mabao 3-0 nyumbani, Josiah akaona hana cha kupoteza, akafanya mabadiliko ya wachezaji wawili dakika ya 75, akiwatoa Kayanda na Khlefin Hamdoun, kisha kuingia Elius Maguli na Geofrey Kasanga. Hata hivyo, hayakuwa na tija hadi mwisho wa mechi wakalala nyumbani.
Ilishuhudiwa pia Kocha wa Azam, Florent Ibenge, akifanya mabadiliko mengine dakika ya 75, akiwatoa wafungaji wa mabao, Fei Toto na Sereri, wakaingia Sadio Kanoute na Mzee Hassan Mzee, kisha dakika ya 80, Kibeku akampisha Aimar Hafidh.
Kwa kufunga mabao mawili, imemfanya Sereri kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi hiyo ambayo kwa kiasi fulani Azam imewarudisha katika imani ya kuendelea kufanya vizuri kuelekea kuikabili Yanga, Machi 15, 2026 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Azam ushindi huo umeifanya kurejea nafasi ya tatu ikifikisha pointi 27 ikilingana na Simba, lakini tofauti ya mabao inazitenganisha timu hizo za Dar es Salaam. Azam ikifunga mabao 21 na kuruhusu manne, wakati Simba ikiwa na 20, nyavu zake zikitikiswa mara tano.