Na Mwandishi wetu – Dodoma
Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) inaendelea kupanua miundombinu ya kusambaza gesi asilia kwa matumizi ya viwandani na majumbani katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, na sasa mpango ni kufika Morogoro, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji TPDC Mussa Makame akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dodoma kutangaza Miradi ya Maendeleo na fursa za vijana kwa mwaka 2025/2026
Makame amesema Vituo 14 vya kujaza gesi asilia (CNG) vimekamilika na vinahudumia vyombo vya usafiri ambapo lengo ni kuhamasisha matumizi ya gesi asilia, kupunguza utegemezi wa mafuta, na kuchangia katika kupunguza hewa ukaa.
“TPDC inaunga mkono maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na asilimia 80 ya Watanzania wakitumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034”
Aidha Makame amesema hadi sasa, nyumba 2,515 zimeunganishwa na mtandao wa mabomba ya gesi asilia na tathmini ya kufikia maeneo mengine katika mikoa iliyofikiwa na bomba inaendelea ili kupanua wigo wa kuwafikia wateja.
Hata hivyo TPDC inashirikiana na Sekta binafsi kuanzisha miradi midogo ya gesi kimiminika (Mini-LNG) itakayowezesha kufikisha gesi asilia nchi nzima, na kuchangia katika maendeleo endelevu ya nchi.
.jpeg)

