Trump Aamuru Iran Ionoe Mabomu Hormuz, Marekani Yashambulia Boti 16

Jeshi la Marekani limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya boti za kijeshi za Iran zilizokuwa zikidaiwa kuweka mabomu ya majini katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, hatua iliyokuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuionya Tehran kuondoa mabomu hayo mara moja.

Katika video iliyotolewa na U.S. Central Command (CENTCOM) kwenye mtandao wa X, ndege za kivita za Marekani zinaonekana kushambulia boti za Iran usiku, huku milipuko mikubwa ikionekana baada ya mashambulizi hayo.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth amesema jumla ya meli na boti 16 za Iran ziliharibiwa katika operesheni hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za kijasusi za Marekani, Iran ilikuwa imepeleka boti ndogo katika njia hiyo muhimu ya kimataifa ya usafirishaji wa mafuta. Kila boti ilidaiwa kuwa na uwezo wa kubeba mabomu mawili hadi matatu ya majini ambayo yangeweza kulipuka na kuharibu meli yoyote ya mafuta inayopita.

Inakadiriwa kuwa Iran inaweza kuwa na kati ya mabomu ya majini 2,000 hadi 6,000, yakiwemo yaliyotengenezwa Iran, China na Russia.

Rais Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social akionya Iran kuondoa mabomu hayo “MARA MOJA”, akisema:

“Ikiwa mabomu hayo yamewekwa na hayataondolewa haraka, Iran itakabiliwa na madhara ya kijeshi ambayo hayajawahi kuonekana.”

Hata hivyo aliongeza kuwa kama mabomu hayo yataondolewa, hiyo itakuwa hatua nzuri ya kupunguza mvutano.

Mlango wa Bahari wa Hormuz ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za biashara duniani, ambapo karibu asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia ya dunia hupitia katika eneo hilo kila siku. Takribani meli 80 za mafuta hupita katika njia hiyo kila siku.

Tayari vita kati ya Marekani, Israel na Iran vimesababisha usafirishaji wa mafuta kupitia njia hiyo kupungua kwa kiasi kikubwa, huku meli nyingi za mafuta zikisimama karibu na Dubai na Oman zikisubiri hali itulie.

Iran yajibu vitisho

Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Iran Ali Larijani amesema Iran haiogopi vitisho vya Marekani.

Alisema:

“Mlango wa Hormuz unaweza kuwa njia ya amani na ustawi kwa wote, au ukawa njia ya kushindwa na mateso kwa wanaochochea vita.”

Kwa sasa, jeshi la Marekani limesema linaangalia uwezekano wa kusindikiza meli za biashara kupitia Hormuz ili kuhakikisha usalama wa usafirishaji wa mafuta duniani.