Wadau: Sera rafiki chachu Tanzania kung’ara biashara ya Kaboni

Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo wamesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kupiga hatua kiuchumi iwapo itaweka sera rafiki za kuvutia wawekezaji katika sekta ya biashara ya kaboni na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi.

Wamesema ukubwa wa ardhi ya nchi, juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na ukweli kwamba asilimia 34 ya ardhi iliyohifadhiwa kama misitu na maeneo ya wanyamapori, ni fursa kubwa kwa Tanzania kunufaika na biashara ya kaboni kupitia miradi ya upandaji miti na uhifadhi wa misitu.

Hayo yameelezwa leo Jumatano, Machi 11, 2026, katika majadiliano ya wadau yaliyofanyika Dar es Salaam kujadili namna ya kuimarisha mazingira ya biashara ya kaboni nchini.

Majadiliano hayo yalikuwa na mada isemayo: Kuimarisha ustahimilivu wa udhibiti na kuongeza imani ya wawekezaji katika mifumo ya nishati safi ya kupikia inayotegemea kaboni.”

Yaliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) kupitia programu ya nishati safi inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU). Wadau walioshiriki ni pamoja na wawakilishi wa Wizara ya Nishati, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Wizara ya Maliasili na Utalii, Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), wataalamu wa masoko ya kaboni, sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

Akizungumza katika majadiliano hayo, Ofisa Uwekezaji Mwandamizi wa UNCDF, Abraham Byamungu, amesema biashara ya kaboni inazidi kuwa muhimu duniani kwa kusaidia kupunguza uzalishaji wa gesi chafu zinazosababisha mabadiliko ya tabianchi.

Ofisa Uwekezaji Mwandamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Mitaji (UNCDF), Abraham Byamungu (katikati) akiteta jambo na mtaalamu wa biashara ya kaboni, Annika Richter (kushoto) na mtaalamu wa nishati kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Dk Geoffrey Ndegwa.



Amesema sekta hiyo inaweza kusaidia kupunguza uzalishaji huo kupitia miradi ya ufanisi wa matumizi ya nishati, utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa kuhamasisha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034, pamoja na miradi ya uhifadhi wa misitu.

Hata hivyo, amesema ili Tanzania inufaike zaidi, ni muhimu kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi pamoja na kuweka sera na mifumo rafiki kwa wawekezaji.

“Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuvutia wawekezaji katika biashara ya kaboni. Hata hivyo, bado ipo nyuma ukilinganisha na baadhi ya nchi za ukanda huu kama Rwanda, ambayo licha ya eneo dogo imepiga hatua kutokana na maandalizi mazuri na sera rafiki,” amesema.

Ameongeza kuwa Kenya pia imefanikiwa kutokana na kuwashirikisha wadau na kuweka mifumo bora ya kukuza sekta hiyo.

Kwa upande wake, Ofisa Misitu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Lucas Sabida, amesema majadiliano hayo yamewapa wadau fursa ya kujadili namna biashara ya kaboni inaweza kuiletea Tanzania manufaa ya kiuchumi na kimazingira.

Amesema Serikali imeanza kuweka mazingira bora kupitia kuanzishwa kwa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Biashara ya Kaboni (NCMC).

Kwa mujibu wa Sabida, kituo hicho kinaratibu masuala ya biashara ya kaboni ikiwemo usajili wa miradi, utoaji wa mwongozo wa kitaalamu na uratibu wa utekelezaji wa sera, sheria na kanuni za sekta hiyo.

Ameipongeza UNCDF kwa kuandaa majukwaa hayo na kusisitiza kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau kupitia mapitio ya sera na mifumo ili kuondoa vikwazo vinavyoweza kuzuia ukuaji wa sekta hiyo.