Dar es Salaam. Vyama vya upinzani nchini, vimetoa malalamiko yao dhidi ya Serikali kwa Umoja wa Mataifa (UN), vikitaja kuwepo kwa changamoto katika mfumo wa siasa, demokrasia, Katiba na haki.
Wakati vyama hivyo vikieleza hayo, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza dhamira ya muda mrefu ya Tanzania katika kuendeleza utawala wa kidemokrasia, ushiriki wa kisiasa kwa njia za amani na kuheshimu utawala wa sheria.
Malalamiko ya upinzani yametolewa na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT- Wazalendo, kwa mujibu wa taarifa zao kwa umma.
Kwa mujibu wa taarifa ya vyama hivyo kwa umma, malalamiko hayo dhidi ya Serikali yalitolewa jana Jumanne, Machi 10, 2026 vilipoalikwa kwa nyakati tofauti kwa ajili ya mazungumzo na Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), katika Umoja wa Afrika, Parfait Onanga-Anyanga.
Onanga-Anyanga, yupo nchini kwa ziara maalumu itakayohusisha mazungumzo na vyama hivyo vya siasa, Spika wa Bunge, Mussa Zungu, Jaji Mkuu, George Masaju na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mazungumzo hayo, yamejikita katika hali ya kisiasa, utawala bora na kuona namna UN inavyoweza kuunga mkono juhudi za kuimarisha taasisi za kidemokrasia, kusimamia mageuzi na kuendeleza mshikamano kupitia maridhiano.
Aidha, leo Jumatano, Machi 11, 2026, Anyanga amekutana na Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Othuman Chande.
Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chaumma, John Mrema, chama hicho kimefanya mazungumzo na mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu wa UN.
Ujumbe wa Chaumma, uliongozwa na katibu mkuu wake, Salum Mwalimu, aliyeambatana na Katibu wa Sekretarieti na Mkurugenzi wa Itikadi, Mafunzo na Elimu kwa Umma, Edward Kinabo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mazungumzo yalijikita katika ajenda ya hali ya kisiasa na mustakabali wa nchi kufuatia matukio yaliyojitokeza Oktoba 29 na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
“Katika mazungumzo hayo, Mwalimu, amewasilisha maazimio ya kamati kuu ya chama kuhusiana na yote yaliyojiri katika uchaguzi mkuu wa 2025 na matukio ya Oktoba 29,” inaeleza taarifa hiyo ya Chaumma.
Pia, inaeleza Mwalimu, amemweleza Mwakilishi huyo maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa Chaumma imesikitishwa na matukio yote ya Oktoba 29 na isingependa kuona hali kama hiyo ikijirudia.
Katika mazungumzo hayo, Chaumma imetoa rai ya kutaka kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria kwa wale wote watakaobainika kuhusika.
“Chaumma inaamini mazungumzo ndiyo njia sahihi zaidi ya kuliponya Taifa kutoka kwenye mtanziko wa kisiasa wa tangu na baada ya uchaguzi mkuu wa 2025 na kuweka misingi madhubuti ya upatikanaji wa haki na demokrasia ya kweli kupitia kuandikwa kwa Katiba mpya na kuimarishwa kwa mifumo huru na ya kuaminika ya uchaguzi,” inaeleza taarifa hiyo.
Kwa upande wa Chadema, ujumbe wake uliongozwa na Katibu Mkuu wake, John Mnyika, aliyeambatana na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Dk Rugemeleza Nshala.
Kama ilivyokuwa kwa Chaumma, mazungumzo ya Chadema na mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu wa UN, yalijikita kuzungumzia hali ya siasa nchini kufuatia matukio ya Oktoba 29, 2025 na athari zake.
Kupitia mazungumzo hayo, Mnyika alimpatia mwakilishi huyo uamuzi wa Kamati Kuu ambayo ni msimamo wa chama hicho, uliotolewa kwa umma Desemba 11, 2025.
“Chadema inaendelea kusisiza kutaka kufanyike uchunguzi utakaofanywa na chombo huru ili kubaini wote waliohusika kuua, kujeruhi na kupoteza watu Oktoba 29 na siku zilizofuata na kuwawajibisha wote watakaobainika kuhusika,” inaeleza taarifa.
Aidha, chama hicho kimesisitiza kufanyike mabadiliko ya Kikatiba yatakayowezesha kuwepo kwa chaguzi huru na haki nchini.
Kwa upande wa ACT- Wazalendo, ujumbe wake uliongozwa na kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu aliyeambatana na Katibu wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa kimataifa wa chama hicho, Mwanaisha Mndeme.
Katika mazungumzo hayo, Semu ameeleza wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa kisiasa ulijitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akidokeza pia kuwepo kwa ukandamizaji wa demokrasia, uminyaji wa haki na uhuru wa vyombo vya habari.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu akisalimiana na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika, Parfait Onanga-Anyanga leo Jumanne, Machi 10, 2026 walipokutana jijini Dar es Salaam.
“Kumekuwa na wizi wa kura, kukanyagwa kwa haki za kisiasa, vitisho na pamoja na matumizi ya nguvu dhidi ya wananchi wanaodai haki za kidemokrasia yameendelea kutawala nchini,” amedai Semu katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Pia, Semu ametumia mazungumzo hayo, kueleza masikitiko ya ACT Wazalendo na wananchi, akidai kumekuwa na madhila makubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu hususani mauaji ya raia yaliyofanywa na vyombo vya dola wakati wa uchaguzi huo, matukio yaliyoacha maumivu makubwa katika mioyo ya Watanzania kwa kuwapoteza ndugu zao.
Katika mkutano wake na Onanga-Anyanga uliofanyika ofisi za ubalozi wa UN jijini Dar es Salaam, Semu amerejea msimamo wa chama chake wa kutoitambua Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa amani Oktoba 29, 2025 iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Mapendekezo ya chama ni kuundwa kwa chombo huru na cha kimataifa kinachoaminika ili kufanya uchunguzi wa kweli wa vitendo hivyo na kuchukuliwa hatua dhidi ya waliohusika,” amesema Semu.
Kiongozi huyo ametoa rai kwa UN kulipa uzito jambo hilo na kuweka msukumo utakaosaidia utekelezaji wa suala hilo muhimu katika kufikia uwajibikaji na kurejesha amani na utengamano wa Watanzania.
Aidha, Semu ametoa wito pia kwa jumuiya ya kimataifa kufuatilia kwa karibu hali ya kisiasa na kidemokrasia Tanzania na kusaidia juhudi za kuhakikisha haki, uwajibikaji na utawala wa sheria vinazingatiwa.
“Ili kujenga misingi ya kweli ya demokrasia, suluhisho la kudumu la changamoto za kisiasa nchini linahitaji kufanyika kwa mageuzi ya msingi ya kisiasa na kikatiba, hususan kuharakishwa kwa mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya na kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi,” ameeleza.
Taarifa ya Kenani Kihongosi, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM aliyoitoa leo Jumatano, Machi 11, 2026 inaeleza kuwa, chama hicho kimewakilishwa na Katibu Mkuu wake, Dk Asha Rose-Migiro.
“Dk Migiro amesisitiza dhamira ya muda mrefu ya Tanzania katika kuendeleza utawala wa kidemokrasia, ushiriki wa kisiasa kwa njia za amani na kuheshimu utawala wa sheria.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, AshaRose Migiro, amefanya mazungumzo jijini Dodoma na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa iliyopo Addis Ababa (UNOAU), Balozi Parfait Onanga Anyanga, leo Machi 11, 2026 .
“Amebainisha kuwa, Tanzania inaongozwa na misingi ya Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Demokrasia, Uchaguzi na Utawala, pamoja na viwango vya kimataifa vilivyowekwa katika Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa,” inaeleza taarifa hiyo.
Aidha, Katibu Mkuu ameeleza mageuzi ya kisheria yaliyofanyika katika Tume ya Uchaguzi na taasisi nyingine, ikiwemo kutungwa kwa sheria mpya za uchaguzi mwaka 2024, hatua zilizolenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na kuimarisha imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa, Dk Migiro amegusia pia matukio ya vurugu yaliyotokea katika baadhi ya maeneo wakati na baada ya uchaguzi mkuu, yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali, ikiwemo mashambulizi dhidi ya ofisi za CCM.
Aidha, amesema hatua stahiki zilichukuliwa kurejesha utulivu na amani nchini.
Kwa pamoja, CCM na Umoja wa Mataifa wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza mazungumzo na maridhiano miongoni mwa wadau wa kitaifa.
Dk Migiro amemthibitishia Balozi Onanga-Anyanga kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kuimarisha amani, usalama na maendeleo jumuishi.
“CCM imepongeza ushirikiano madhubuti uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Mataifa, na kuthibitisha dhamira yake ya kustawisha mshikamano wa kitaifa, utulivu na demokrasia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” inaeleza taarifa hiyo.