Dodoma. Halmashauri ya Jiji la Dodoma imewataka wamiliki binafsi na taasisi zinazomiliki viwanja katika jiji hilo kuviendeleza mara moja, kabla havijarudishwa serikalini na kuuzwa kwa watu wengine kwa mujibu wa sheria.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Machi 11, 2026 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Jiji la Dodoma, Denis Gondwe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Gondwe amesema kwa mujibu wa sheria, mtu anapokabidhiwa kiwanja anatakiwa kukiendeleza kwa kujenga ndani ya kipindi kisichozidi miezi 36, vinginevyo mamlaka husika inaweza kukitwaa na kukigawa kwa mtu mwingine.
“Kuna baadhi ya watu binafsi na taasisi ambao hawajaendeleza viwanja vyao kwa muda mrefu. Hali hiyo imesababisha watu wengine kuvamia maeneo hayo na kusababisha migogoro ya ardhi isiyokuwa ya lazima. Natoa ilani leo kuwa kila mwenye kiwanja ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma akiendeleze kabla hakijachukuliwa kwa mujibu wa sheria na kupewa mtu mwingine,” amesema Gondwe.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999, Sura ya 113, wananchi pamoja na taasisi zote zinazomiliki viwanja wanatakiwa kuviendeleza ndani ya muda usiozidi miezi 36 tangu walipokabidhiwa au kumilikishwa.
Amebainisha kuwa kutoendelezwa kwa viwanja ndani ya jiji hilo kumesababisha baadhi ya maeneo kuwa na mapori makubwa, hali inayochangia wahalifu kujificha na kuhatarisha usalama wa wananchi.
“Mtu akivamia kiwanja cha mwingine hawezi kushughulikiwa na halmashauri pekee, kwa sababu hilo ni kosa la jinai kama yalivyo makosa mengine. Linapaswa kuripotiwa polisi ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake. Hivyo wanaovamia viwanja vya watu waache mara moja,” amesema Gondwe.
Pia ametoa onyo kwa watu wanaojenga nyumba bila vibali vya ujenzi kuacha mara moja na kufuata taratibu za mipango miji zinazowataka kupata kibali kabla ya kuanza ujenzi.
Amesema kumekuwepo na tabia kwa baadhi ya wananchi kuendeleza ujenzi katika maeneo yasiyoruhusiwa bila kuwa na kibali kutoka mamlaka husika, na wakati mwingine wanapoelekezwa kusitisha ujenzi huo hupuuza maelekezo hayo.
Amefafanua kuwa mtu yeyote atakayebainika kuendelea na ujenzi bila kibali cha ujenzi, nyumba yake itabomolewa ili kulinda utekelezaji wa sheria ya mipango miji inayotaka kibali kipatikane kabla ya kuanza ujenzi.
Gondwe amesema pia kwa sasa kuna wimbi la watu wasio na nia njema wanaovamia viwanja ambavyo havijaendelezwa na kujimilikisha maeneo hayo, huku wengine wakiondoa bikoni (beacon) zinazoweka alama za mipaka ya, jambo linalosababisha usumbufu mkubwa kwa wamiliki halali wa viwanja hivyo.
Aidha, kwa wale wanaofanya maendeleo ya kudumu kama kujenga majengo bila vibali vya ujenzi, amesema halmashauri itaendelea na zoezi la ubomoaji kwa sababu wanakiuka Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya mwaka 2007 pamoja na Sheria ya Serikali za Mitaa Namba 8 ya mwaka 1982.
Amefafanua kuwa sheria hizo zinaelekeza kuwa kila jengo linalojengwa ndani ya mamlaka ya mji au jiji lazima liwe na kibali cha ujenzi kutoka mamlaka husika kabla ya kuanza kujengwa.