Wanaojifungua wahimizwa kutumia kikamilifu likizo ya siku 90

Dar es Salaam. Wanaojifungua  nchini wamehimizwa kutumia kikamilifu muda wa mapumziko wa miezi mitatu baada ya kujifungua ili waweze kuwa karibu na watoto wao katika kipindi muhimu cha mwanzo wa maisha.

Wito huo umetolewa wakati kukibainika baadhi ya wanawake, hasa walioajiriwa katika sekta binafsi na wanaojiajiri, wamekuwa wakirudi katika shughuli zao za kazi mapema kabla ya kumalizika kwa muda huo wa mapumziko.

Kwa mujibu wa wadau wa sheria na ajira, muda wa miezi mitatu uliowekwa kisheria si wa bahati mbaya, bali unalenga kumpa mama nafasi ya kuimarisha afya yake baada ya kujifungua na kumpatia mtoto malezi ya karibu katika miezi yake ya mwanzo.

Akizungumza leo Jumatano, Machi 11, 2026 na wanawake katika wodi ya wazazi Hospitali ya Mwananyamala, Wakili Loveness Denis amesema bado kuna changamoto ya baadhi ya wanawake kushindwa kutumia kikamilifu muda huo kutokana na shinikizo la kiuchumi au mazingira ya kazi.

Loveness na mawakili wengine kutoka kampuni ya mawakili ya Ernestilla Mafita (EM&CO) walitoa elimu hiyo sambamba na vifaa mbalimbali kwa waliojifungua katika hospitali hiyo ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

Wakili huyo amesema sheria za kazi zinatambua umuhimu wa mama kuwa na muda wa mapumziko baada ya kujifungua, hivyo ni muhimu kwa wanawake kutambua haki hiyo na kuitumia ipasavyo.

 “Ni kipindi muhimu sana kwa maendeleo ya mtoto. Mama anapokuwa karibu na mtoto katika miezi ya mwanzo, inasaidia katika malezi, afya na hata uhusiano wa karibu kati yao, bahati mbaya baadhi ya wanawake wanaamua kurejea kazini mapema kwa sababu ya hofu ya kupoteza kipato au nafasi zao kazini, hasa kwa wale wanaofanya biashara binafsi au wanaojiajiri,” amesema.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa ni muhimu kwa waajiri na jamii kwa ujumla kutambua kuwa likizo ya uzazi ni haki ya msingi kwa aliyejifungua na inapaswa kuheshimiwa.

Aidha, amesema familia zinapaswa kutoa ushirikiano kwa wanawake katika kipindi hicho ili waweze kutumia muda huo kwa malezi ya watoto wao bila presha ya kurejea haraka katika shughuli za kiuchumi.

Baadhi ya wanawake waliozungumza na Mwananchi wamesema changamoto ya gharama za maisha na majukumu ya kifamilia imekuwa ikiwalazimu kurejea mapema katika shughuli zao.

Mkazi wa Dar es Salaam, Rehema Salum, amesema baada ya kujifungua mtoto wake wa pili alilazimika kurejea kwenye biashara yake ya kuuza nguo baada ya mwezi mmoja tu kwa sababu ndiyo chanzo kikuu cha kipato cha familia.

“Nilijua ninahitaji muda zaidi wa kukaa na mtoto, lakini pia nilihitaji kuendelea na biashara ili familia iweze kupata kipato,” amesema Rehema.