Unguja. Wakati kukiwa na malalamiko na mijadala kuhusu vikosi vya Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuwapiga wananchi na kuwanyang’anya bidhaa katika Soko Kuu la Darajani, Serikali imekiri kuwepo kwa kero hiyo na kutaka kusitishwa kwa matumizi ya silaha kuanzia sasa.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Machi 11, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ Zanzibar, Idrissa Kitwana Mustafa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya siku 100 za Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Idara ya Habari Maelezo Zanzibar. Waziri huyo amesema Serikali inatambua operesheni inayofanywa na vikosi vya idara hiyo, lakini haijatoa agizo la kuwachukulia hatua wananchi kwa kuwapiga au kuwabughudhi. Badala yake vikosi hivyo vinapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata taratibu zilizopo.
“Kwa sasa kuna operesheni, lakini vikosi vyetu wametumia mbinu ambayo si sahihi ya kutembea na silaha, na tayari jambo hilo tumeliona na tunazuia matumizi hayo,” amesema Kitwana.
Hata hivyo, Waziri huyo amesema wakati mwingine ipo haja ya askari kutumia silaha kwa ajili ya usalama wao, ingawa wananchi hawajaizoea hali hiyo na hivyo kuwajengea hofu.
Akizungumzia suala la askari hao kuvaa maski, amesema hufanya hivyo kwa lengo la kuondoa muhali (kuwaonea haya au taabu kuwachukulia hatua watu wanaowafahamu) ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uhuru na weledi.
Amesema askari hao wanaendesha operesheni hiyo kwa kushirikiana na Manispaa, Mji Mkongwe na wizara nyingine kwa lengo la kuhakikisha mji unakuwa safi.
Amesema kwa kawaida askari hufika katika maeneo hayo mapema kabla ya watu wengi kuingia mjini, na pale wanapobaini mtu anataka kuanzisha biashara katika eneo lisiloruhusiwa, huchukua hatua za kumuondoa.
Amesisitiza kuwa hadi sasa hakuna taarifa rasmi za mtu kupigwa katika operesheni hiyo, lakini iwapo itabainika kuwa askari wamefanya hivyo, watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Licha ya kauli ya Waziri kukana tukio hilo, yapo madai kuwa baadhi ya askari wamekuwa wakitumia nguvu kuwapiga wafanyabiashara na kuwanyang’anya bidhaa zao bila kuwarejeshea.
Aidha, zipo picha na video zinazozunguka katika mitandao ya kijamii zikionyesha baadhi ya askari wakidaiwa kuwapiga wananchi katika maeneo ya Darajani Unguja.
“Tumeona video zikisambaa katika mitandao ya kijamii zikionyesha vijana wetu wakiwapiga wananchi. Tunazifuatilia ili kubaini kama ni za mwaka huu au ni za matukio ya zamani yaliyounganishwa na tukio hili. Ikibainika tutachukua hatua,” amesema Kitwana.
Wakitoa maoni yao kuhusu suala hilo, baadhi ya wananchi wamesema wanasikitishwa na vitendo vya askari kuchukua sheria mkononi, wakisema ni kinyume na taratibu za kisheria.
Ali Sultani amesema ameshuhudia askari wakichukua mabegi ya wafanyabiashara bila kuwarejeshea.
“Juzi niliona mtu akichukuliwa mabegi yake akanyanyua mikono juu kumuomba Mungu. Mwingine wakati anachukuliwa vitu vyake aliinama chini na kusujudu. Sasa kwa hali hii tutafika wapi?” amehoji.